WANNE WAFARIKI AJALI YA BASI SHINYANGA, MAJERUHI WATANO WAKATIKA VIUNGO, 15 WATIBIWA NA KURUHUSIWA...MWENDOKASI WATAJWA


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Debora Magiligimba, akiangalia basi ambalo limepata ajali likiwa na abiria 43 na kuua watu wanne na kujeruhi 20.

Na Shinyanga Press Club Blog
WATU wanne wamefariki dunia katika ajali ya basi la Kampuni ya Classic lenye namba za usajili binafsi Salum Rashidi Classic (SRC 3), lililokuwa likitokea Kampala nchini Uganda kwenda Jijini Dar es salaam.

Ajali hiyo imetokea saa 10:54 Alfajiri kuamkia leo katika kona ya Didia wilayani Shinyanga na kusababisha vifo vya abiria hao na majeruhi 20 ambao wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba, amewataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Wahida Yusuph mkazi wa Pemba, Joseph Joseph mkazi wa Dar es Salaam, Rehema Haji mkazi wa Unguja na Nasorro Hamisi mkazi wa Zanzibar.

Amewataja majeruhi watano ambao wamekatika viungo vya miili yao, kuwa ni Njama Hassani, Fatuma Kesi, Sada Manga, na Twalibu, wote wamekatika mkono wa kushoto na mmoja mguu wa kulia, pamoja na Mohamed Daudi mkono wa kulia.

Aidha amesema Majeruhi wengine 15 walitibiwa na kuruhusiwa na hali zao zinaendelea vizuri, huku akibainisha kuwa basi hilo lilikiwa na abiria 43 ambapo wengine ni wazima hawakuumia.

"Chanzo cha ajali hii ni mwendo Kasi, ambapo Dereva wa basi anayejulikana kwa jina la Maxison Mkuru alishindwa kukata Kona na kusababisha ajali, na tunamsaka sababu amekimbia," alisema Magiligimba.

“Miili ya Marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani mkoani Shinyanga, na majeruhi wanaendelea na matibabu, na ninatoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani,”ameongeza.

Nao baadhi ya abiria waliokuwa kwenye basi hilo akiwamo Fotuna Wilbert, amesema baada ya kufika kwenye kona hiyo ya Didia basi likiwa katika mwendo kasi, walishaghaa kuona linayumba na kumshinda dereva na kupata ajali.

TAZAMA PICHA ZA JALI HAPA CHINI
Baadhi ya abiria ambao wamenusurika kwenye ajali ya basi, wakiangalia mizigo yao.
Askali Polisi wakiwa na wafanyakazi wa mgodi wa madini ya dhahabu Buzwagi, wakiangalia namna ya kulinyanyua basi hilo.
Zoezi la kunyanya basi likiendelea.
Basi likiwa limenyanyuliwa.

Picha na Marco Maduhu


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464