JUMUIYA YA WAZAZI CCM YASHAURIWA


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati akizungumza na Jumuiya ya Wazazi CCM.


Na Suzy Luhende, Shinyanga

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati ameishauri jumuiya ya wazazi CCM mkoani Shinyanga kuendelea kuhamasisha watu waendelee kujiunga kwenye jumuia hiyo na ndani ya chama cha mapinduzi ikiwa ni pamoja na kuzingatia malezi bora, afya, elimu kilimo na kuhamasisha masuala ya kiuchumi.

Ushauri huo ameutoa alipokuwa mgeni rasmi kwenye kikao cha kawaida cha baraza la wazazi mkoa wa Shinyanga, ambapo aliishauri jumuia hiyo kuendelea kuhamasisha wananchi na wanachama wajiunge kwenye jumuia hiyo kwa kuwa jumuia hiyo ndiyo inayolea vizuri wanachama na ndiyo inazingatia malezi bora, afya, mazingira na kuhamasisha masuala ya kiuchumi.

Sengati Amesema kuwa jumuia ya wazazi ina umoja na inafanya kazi zake kwa utashi wa kutosha, hivyo ataendelea kushirikiana na jumuia hiyo kwa karibu ili kuhakikisha Inasonga mbele na inafanya vizuri katika kazi zake za kulisukuma guruduma la maendeleo na kufuata ilani ya chama cha mapinduzi CCM.

"Kama nitaendelea kuwepo mkoa wa Shinyanga nitaendelea kushirikiana na jumuia hii kwa lolote, pia kwenye taarifa yenu mmesema mnaanzisha ujenzi wa nyumba za makatibu hivyo katika michango yenu na mimi nitachangia ili kuhakikisha makatibu wetu wanakuwa na nyumba za kuishi"amesema Sengati.

Pia katika kikao hicho kulikuwa na tukio la kupatiwa hati kwa baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakiisaidia kwa karibu jumuia hiyo, ambapo pia aliishukuru uongozi kwa kufanya ubunifu huo, kwani kufanya hivyo ni kuwatia moyo viongozi wanaoisaidia jumuia hiyo ikiwa kwa mawazo kwa michago.

"Binafsi nimejisikia vizuri sana kupokea hii hati naamini hata wengine mliopata hati hizi mmejisikia vizuri, msisite kunishirikisha kwa lolote nitatoa ushauri kama kuna chochote kitakuwa kinahitajika mnione kwa sababu mmeanza na mimi kwa upendo mkubwa, hivyo tuendeleze upendo siku zote kwenye jumuia na ndani ya chama cha mapinduzi CCM pia tuendelee kumuunga mkono Rais wetu Suluhu Samia kwa kazi anazifanya "amesema Sengati.

Amesema Rais Samia amefanya Mambo makubwa ametoa Sh 500 milioni kwa kila kila Jimbo kwa ajili ya kutengenezea barabara anaendelea kutekeleza na kazi zingine, hivyo kinachotakiwa ni kusimamia kikamilifu miradi inayoanzishwa, pia kuhamasisha wananchi waweze kuwa na kilimo cha kisasa chenye tija kuwa na ufugaji wa kisasa na vijana wetu waweze kupata ajira ili wananchi waendelee kukiamini chama.

Kwa upande wake katibu wa jumuia ya wazazi mkoa wa Shinyanga Masanja Salu alimshukuru mkuu wa mkoa kwa kuitikia wito wa kuwa mgeni rasmi katika kikao hicho, pia alikiomba chama cha mapinduzi CCM kiendelee kuzishike mkono jumuia zake ili ziendelee kufanya vizuri zaidi.

Nae mjumbe wa Baraza kuu Taifa wazazi Benard Shigela kutoka mkoani Shinyanga amesema ili jumuia ya wazazi iendelee kufanya mazuri na makubwa ni lazima kuwa na umoja na ushirikiano, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha wanachama wajiunge na jumuia hiyo huku ikifuata irani ya chama cha mapinduzi CCM.



Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati akizungumza na Jumuiya ya Wazazi CCM

Kikao cha jumuiya ya wazazi CCM




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464