KESI YA SABAYA KUANZA KUSIKILIZWA LEO KUUNGURUMA SIKU 14 MFULULIZO



MASHAHIDI 10 wa upande wa Jamhuri leo wataanza kutoa ushahidi katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili.

Sabaya na wenzake wanadaiwa kutumia silaha kupora Sh 3,159,000 jijini Arusha.

Mahahidi hao wanatarajiwa kutoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkadhi Mkoa wa Arusha mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mkoa wa Geita, Odira Amworo aliyekwenda huko kuisikiliza kesi hiyo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Tumaini Kweka alisema watakuwa na vielelezo 10 vitakavyowashilishwa mahakamani hapo.

Hakimu Amworo aliwataka mawakili Dancan Oola na Mosses Mahuna wanaomtetea Sabaya na wakili Silvester Kahunduka anayemtetea mshitakiwa wa pili, Silvester Nyengu na Jestone Jastin anayemtetea mshitakiwa wa tatu, Daniel Mbura wajiandae kwa ajili ya kuisikiliza kesi hiyo kwa siku 14 kwa kuwa yupo Arusha kwa ajili ya kesi hiyo tu.

Kweka anasaidiwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi Mkoa wa Arusha, Abdallah Chavula na Mwendesha Mashitaka Mfawidhi Mkoa wa Mbeya, Mbaraka Mgaya na wote walimweleza Hakimu Amworo kuwa wako tayari kusikiliza kesi hiyo katika muda huo.

Katika hati ya mashtaka inadaiwa kuwa, Februali 9 mwaka huu mtaa wa Bondeni jijini Arusha, washitakiwa kwa pamoja wakiwa na silaha walimpora Bakari Msangi fedha na kabla ya kufanya hivyo walimpora simu mbili na kumpiga kwa ngumi, mateke, makofi, kichwa na kumtishia kwa silaha.

Katika shitaka la pili ilidaiwa Sabaya na wenzake Nyegu na Mbura walivamia dula la Mohamed Saad kwenye mtaa wa Bondeni jijini Arusha, waliingia kaunta ya duka hilo na kupora Sh 2,769,000.

Ilidaiwa kabla ya kumpora walimpigia kwa ngumi, mateke, makofi, kichwa na kumtisha kwa silaha.

Chavula alisoma shitaka la tatu la unyang'anyi wa kutumia silaha lilinawakabili Sabaya, Nyengu na Mbura wakidaiwa kuwa, Februali 9 mwaka huu mtaa wa Bondeni jijini Arusha kwa pamoja wakiwa na silaha walimpora Ramadhani Rashid simu moja ya mkononi aina ya Tecno na fedha Sh 35,000.

Ilidaiwa kabla ya kufanya uhalifu huo waliwalaza chini watu wote waliokuwa katika duka hilo na kuwapiga kwa ngumi, mateke, kichwa na makofi na kuwalazimisha kumwonyesha mmiliki wa duka hilo Mohames Saad.

Katika mashitaka mengine manne, Sabaya na wenzake wengine watano walidaiwa kuongoza genge la uhalifu, uhujumu uchumi, utakatishaji fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka na kuomba rushwa ya Sh milioni 90.

Mshitakiwa wa pili, Enock Togolani Mnkeni (41) mkazi wa Arusha, mshitakiwa wa tatu Watson Mwahomange (27), mshitakiwa wa nne, John Odemba Aweyo na Silvester Nyengu.


 Chanzo Habari Leo.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464