Muonekano wa Stand ya Mabasi Mbezi Louis Jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amelielekeza Jeshi la Polisi kuhakikisha kuanzia Sasa Mabasi yote yanashusha na kupakia abiria kwenye kituo kikuu cha Mabasi cha Mbezi Louis.
RC Makalla amesema hayo wakati alipotembelea kituo hicho na kusikiliza kero na changamoto mbalimbali za Wafanyabiashara kituoni hapo.
Amesema Serikali inatambua kituo kimoja pekee Cha Mabasi ambacho ni Mbezi na uwekezaji uliofanyika ni mkubwa hivyo hakuna maana kama kila mmiliki wa mabasi atakuwa na kituo chake kupakia na kushusha abiria.
Aidha RC Makalla ameelekeza uongozi wa Stendi hiyo kuweka utaratibu wa baadhi ya Mabasi kushusha abiria kwenye eneo la kulaza magari ambapo kuna Banda la Mamalishe ili kuchochea biashara. Kuhusu changamoto ndogondogo zilizojitokeza kituoni hapo,
RC Makalla ameelekeza Viongozi wa Halmashauri ya Ubungo na kituo kuzipatia ufumbuzi wa haraka. Mhe.Makalla pia ameelekeza Wafanyabiashara kituoni hapo wapangwe Katika utaratibu mzuri na bora kuendana na hadhi ya kituo.
Wakati huohuo RC Makalla ametembelea Soko la Machinga lililopo pembezoni mwa Stendi hiyo na kutaka Wafanyabiashara wote wahamishiwe sokoni hapo na uchunguzi ufanyike kwa wale waliopatiwa vibanda kwa upendeleo na kujuana ambapo Wafanyabiashara hao wamesema wapo tayari kuhamia sokoni apo na wamechoka kufanya biashara barabarani.
Amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kuweka utaratibu wa Daladala kushusha abiria sokoni apo ili kuchagiza biashara.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464