Baadhi ya majengo ya shule ya sekondari Geita yaliyoungua moto.
Geita. Serikali imelazimika kuifunga kwa muda wa siku 14 Shule ya Sekondari Geita kutokana na matukio ya kuungua moto mara tatu mfululizo.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano ya
Julai 14,2021 baada ya kuungua moto jana usiku ikiwa ni mara ya tatu ndani ya
siku saba. Awali, moto huo ulisababisha uharibifu wa mali, lakini kwenye tukio
la jana usiku wanafunzi watatu wamejeruhi.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemery
Senyamule ametangaza uamuzi huo baada ya moto kuteketeza bweni na kujeruhi
wanafunzi watatu.
Katika tukio la kwanza lililotokea Julai
5,2021, moto uliteketeza magodoro na masanduku ya wanafunzi, la pili likatokea
Julai 6 kwa kuteketeza maabara mbili za sayansi.
Tukio la tatu limetokea usiku wa kuamkia
leo na kuunguza vyumba viwili katika bweni la Sokoine na kuunguza magodoro huku
mwanafunzi watatu wakijeruhiwa na kulazwa Hospitali ya mkoa wa Geita.
Mkaguzi msaidizi wa zimamoto mkoani hapa
Peter Nkwambi, amesema katika tukio hilo mkuu wa shule alipata mshtuko na
kukimbizwa katika hospitali ya mkoa.
Geita ni miongoni mwa sekondari kongwe
nchini ambayo awali ilikuwa ikimilikiwa na Chama cha Ushirika cha Nyanza kabla
ya kuwa chini ya umiliki wa sekondari. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin
Gondwe ni miongoni mwa wanafunzi waliohitimu shuleni hapo.