VIJANA 25,390 KUTOKA KATA 37 SHINYANGA WAFIKIWA NA ELIMU YA AFYA YA UZAZI, WADAU WAPONGEZA WATAKA HATUA ZAIDI

 
 Meneja Miradi wa Shirika la Thubutu Africa Initiatives (TAI), Paschalia Mbugani akizungumzia namna wanavyowafikia vijana ili kuwawezesha kupata elimu ya afya ya uzazi

Na Damian Masyenene

KATIKA kuhamasisha vijana kutumia njia za kisasa za kujikinga na mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya ngono, jumla ya vijana 25,390 kutoka kata 37 za wilaya ya Shinyanga mkoani humo wamefikiwa na elimu ya afya ya uzazi kwa kipindi cha Januari hadi Juni, mwaka huu.

Vijana hao ni 6,818 kutoka Manispaa ya Shinyanga ambao ni wa kike 3,512 na wa kiume 3,306 kutoka katika kata 10, huku halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakiwa ni vijana 18, 572, wakiwemo 9,263 wa kike na 9,309 wa kiume kutoka kata 27 za halmashauri hiyo.

Akizungumzia namna wanavyowawezesha vijana hao, Meneja Miradi wa Shirika la Thubutu Africa Initiatives (TAI), Paschalia Mbugani amesema kupitia mradi wa USAID Tulonge Afya -jukwaa la vijana (SITETEREKI) wanatoa elimu inayohamasisha matumizi sahihi ya kondomu na kwa kila tendo, vijana wa kiume kujifunza namna njia za kisasa za afya ya uzazi zinazotumiwa na wasichana ili waweze kuwasaidia na kuwashawishi wenza wao kutumia njia hizo kujikinga na magonjwa ya ngono na ujauzito usiotarajiwa.

Alisema mradi huo unawalenga vijana wa kike na kiume wenye miaka 15-24 ambao hawako shuleni ili kubadili tabia zao kiafya kutoka tabia hasi kwenda chanya kwa kuhamasisha mabadiliko ya tabia na mienendo kwa kuwahamasisha kutumia njia za kisasa zitakazowawzesha kujikinga na ujauzito usiotarajiwa na magonjwa ya ngono.

“Mwitikio ni mzuri kwa kuwa elimu inatolewa na vijana wenzao ambao ni waelimishaji rika waliopatiwa mafunzo, pia wanapata elimu juu ya afya ya uzazi kwa uwazi na uhuru zaidi na vijana wa kike wanahamasishwa kutambua tabia hatarishi zinazowesha kuwafanya kupata maambukizi ya VVU, pia kupima VVU kwa hiari ikiwa wako hatarini na kuanza kutumia ARV mapema ikiwa watathibitika kuwa na maambukizi,” amesema.

Mbugani ameeleza kuwa vijana wengi wa kiume walikuwa hawajui matumizi sahihi ya Kondomu lakini kupitia elimu hiyo wamejifunza kwa vitendo, huku vijana wa kike wakiondokana na dhana kwamba njia za kisasa za kuzuia mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya ngono ni kwa ajili ya wanawake walioolewa tu na sio wasichana kama wao.

“Pia kwenye jamii kuna dhana nyingi potofu kuhusu madhara ya njia za kisasa za afya ya uzazi (uzazi wa mpango), kwa mfano wapo wanaoamini kwamba njiti huwa zinapotea mwilini au kusogea kutoka ilipowekwa, wapo wananoamini mtu akiwekewa kitanzi/kipandikizi anaweza kubena ujauzito na mtoto akazaliwa ameshika kitanzi na kuna wanaodhani kwamba njia za uzazi wa mpango zinasababisha kansa ya mlango wa kizazi na ugumba, kupitia elimu hii vijana wanapata taarifa sahihi kuhusu njia hizo,” amefafanua. 

 

Mratibu wa Women Fund Tanzania (WFT) mkoani Shinyanga, Glory Mbia

Mmoja wa wadau wakubwa wa masuala ya haki za wanawake na watoto mkoani Shinyanga, Glory Mbia alisema huduma za afya ni haki ya msingi ya binadamu na vijana wakiwa ni kundi tete zaidi kutokana na umri wao wana haki kupata huduma na elimu ya afya ya uzazi, ambapo aliisihi Serikali na wadau wengine kupitia wataalam wa afya na wa kijamii kuwekeza kwa vijana ili waweze kupata taarifa sahihi na kufanya maamuzi sahihi yenye tija kwa afya zao.

Glory ambaye pia ni Mratibu wa Women Fund Tanzania (WFT) mkoani hapa, alisema vijana wa kike wako kwenye hali tete zaidi kwani mfumo dume uliopo umewaondolea uwezo wa kufanya maamuzi hata juu ya miili yao na kujikuta hata maamuzi kutumia au kututumia huduma uzazi wa mpango ni mpaka mwanaume aruhusu jambo hili.

"Hili limeendelea kukandamiza haki yao ya msingi ya kupata huduma za afya. Hivyo niwasihi wadau wote kuhakikisha wanaume wanahusishwa katika utoaji elimu hii ili kuvunja hayo matabaka juu ya maamuzi ya huduma za afya kwa mtu binafsi kwenye mwili wake," alishauri.

Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2021/22, wizara imeendelea kupiga hatua katika kuongeza watumiaji wa njia za uzazi wa mpango ambao ni muhimu katika kulinda afya ya mama, kuimarisha makuzi ya mtoto, na kumwezesha mama kushiriki katika shughuli za kuongeza uchumi wa familia na nchi, ambapo matumizi ya Uzazi wa Mpango yamewezesha familia kupanga uzazi wa watoto na kufanya uzazi uwe salama, malezi kuwa rafiki, mtoto kuwa na afya njema na taifa salama.

Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021, takwimu zinaonesha kuwa akina mama 4,926,183 kati ya akinamama 13,841,430 sawa na asilimia 36 walikuwa wanatumia huduma za uzazi wa mpango za kisasa. Aidha, upatikanaji wa dawa na bidhaa za uzazi wa mpango ulifikia asilimia 92 ya mahitaji halisi. 



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464