Watoto 981 katika Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, wamepatiwa ujauzito ndani ya kipindi cha miezi sita kilichoanzia mwezi Januari mwaka huu.
Kutokana na kitendo hicho cha ukatili wa kijinsia, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis, ameagiza watuhumiwa watafutwe na kuchukuliwa hatua.
Naibu Waziri huyo alibaini hilo akiwa katika ziara ya siku tano wilayani humo iliyomalizika jana, iliyolenga kukagua na kujionea utoaji wa huduma za ustawi wa jamii na masuala ya maendeleo ya jamii.
Katika ziara hiyo pia alizindua Kituo cha Huduma Jumuishi kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa Kijinsia (One Stop Centre) katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kitakachowezesha walengwa kupata huduma kwa pamoja na kwa muda mfupi.
Alisema taarifa hizo haziwezi kufumbiwa macho, badala yake watendaji wanaohusika wafanye kila linalowezekana kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana na haki inatendeka katika kipindi kifupi.
“Jamii haiwezi kutegemea miujiza ya mafanikio ya kizazi kijacho endapo itabaki kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani dhidi ya wanawake na watoto kwa kuangalia watoto wao wanapata mimba katika umri mdogo na kukatisha ndoto zao,” alisema.
SOMA ZAIDI HAPA; CHANZO NIPASHE