Balozi Liberatha Mulamula
Na Mwandishi Wetu
Serikali imesema Ziara aliyoifanya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Rwanda imeleta tija kwa kufungua fursa kwenye sekta ya elimu, usafirishaji, uwekezaji, pamoja na viwanda huku ikibainisha ziara hiyo imeimarisha ujirani mwema kati ya Tanzania na Rwanda na kurahisisha gharama za usafirishaji wa bidhaa za Rwanda kupitia Bandari ya Tanga na Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula wakati akitoa taarifa kwa wanahabari kuhusu kilichojiri katika ziara ya ya Rais Samia aliyealikwa na Mwenyeji wake Rais Paul Kagame.
Amesema katika ziara marais wote walitliana sahihi mikataba ya hati za makubaliano katika maeneo manne ikiwemo elimu, tehama, uhamiaji na usimamizi wa bidhaa za dawa na kwamba walijadili namna ya kuwawezesha wananchi kufanya biashara kwa pamoja na uhuru wa kuingia nchi hizi.
"Ziara imeleta tija marais wote wametia sahihi hati za makubaliano katika sekta ya usimamizi wa dawa wamekubaliana kuboressha bidhaa za dawa hasa katika kipindi hiki cha janga la Corona pamoja na ujenzi wa viwanda kufungua fursa za kibiashara," amesema Balozi Mulamula.
Amebainisha kuwa katika sekta ya elimu Serikali ya Rwanda imeamua Lugha ya Kiswahii kifundishwe kiingizwe katika mitaala ya shule hivyo imemuomba Rais Samia kuipatia wataalamu wa kutengeneza mitaala na kufundisha.
Amesisitiza kuwa akiwa nchini Rais Samia alipata fursa ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza magari aina ya Volkswagen na kwamba kiwanda hicho kinahitaji soko nchini pamoja na kutemelea Kiwanda cha kutengeneza Juisi ya Mananasi. na kwamba Rais Samia amepanga kuanzisha kiwanda hicho nchini.
Ameongeza kuwa Rais Samia alitembelea eneo lililotokea Mauaji ya Kimbali yaliyotokea Rwanda na kusema akifrudi nchini atahamasisha Watanzania kutochezea amani, badala yake waimarishe umoja, mustakabali wa kisiasa na uzalendo.
Balozi Liberata amefafanua kuwa kupitia ziara Serikali imejifunza namna bora ya kuimarisha na kuendeleza maeneo ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali.
Katika ziara ya Kiserikali Rais Samia aliambatana n ujumbe wa viongozi wa Sekta za kimkakati akiwemo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Leonard Chamuriho, Geofrey Mwambe, Saada Nkuya, Profesa Kitila Mkumbo na Dkt. Faustine Ndungulile.
Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini, Masnja Kadogosa, Msajili wa Bodi ya Maziwa, pamoja na watendaji wa taassis nyingine za Serikali.