Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo na Novemba Mosi, 2021 itakuwa siku yake ya mwisho baada ya kuitumikia kampuni hiyo yenye wateja katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika taarifa yake Vodacom imeeleza kuwa Bodi ya wakurugenzi iko katika mchakato wa kumpata mrithi wa Hendi, ambaye ameitumikia kampuni hiyo kwa miaka mitano, na pindi atakapopatikana na kuidhinishwa atatangazwa.
“Katika
miaka mitano ya Hendi, Vodacom imeendelea kuwa kuongoza katika soko
katika utekelezaji wa mikakati ya kidijitali ambayo imesaidia nchi kuwa
na mifumo jumuishi ya kifedha kupitia ubunifu wa huduma za kifedha kwa
njia ya simu,” amesema Jaji Thomas Mihayo ambaye ni Mwenyekiti wa bodi.
Jaji
Mihayo aliongeza kuwa Hendi ambaye anakwenda kuwa mkuu wa biashara wa
Vodafone nchini Hispania, amekuwa ni msukumaji mkuu katika kufanikisha
uwekezaji wa kuwafikia mamilioni ya Watanzania ambao awali hawakufikiwa
na huduma za simu (hawajaunganishwa).
Akizungumzia kuondoka
kwake Hendi amesema anafurahi fursa inayomsubiri Hispania lakini
anatambua isingewezekana kama si fursa aliyoipata Tanzania katika
kipindi cha miaka mitano, miwili na nusu akihudumu kama Mkurugenzi
Mtendaji.
“Nimefanya kazi na timu nzuri na ninaacha wazawa ambao ni viongozi waandamizi wanaofanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Ninafurahi kuhudumu katika taifa hili kubwa. Uzoefu wangu hapa nchini ndiyo imefanikisha hatua hii, Kwa kweli najivunia. Naondoka Tanzania kama balozi wa nchi,” amesema Hendi.
Miongoni mwa mafanikio aliyoyapata Hendi katika kipindi chake ni kampuni hiyo kutajwa miongoni mwa kampuni 100 bora zaidi barani Afrika kulingana na mtaji wa soko mnamo 2020, Kufanikisha kuorodheshwa kwa kampuni hiyo katika soko la hisa la Dar es Salaam.
https://www.mwananchi.co.tz/mw/habari/kitaifa/bosi-vodacom-tanzania-aachia-ngazi--3499202
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464