MTANDAO WAKWAMISHA KESI YA MBOWE MAHAKAMANI



MAHAKAMA YA Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kumuunganisha Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa kwa tuhuma za kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi kutokana na mawasiliano mabaya kwenye Ukumbi wa mahakama ya mtandao ( Video Conference) kati ya Kisutu na Gerezani Ukonga walipo Washtakiwa.

Mapema leo Agosti 5, mwaka 2021, kesi hiyo ambayo imepangwa kusikilizwa kwa ajili ya mtandao ilikuja kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kumuunganisha Mbowe na wenzake baada ya yeye kusomewa mashtaka peke yake, lakini ilishindikana baada ya Mbowe na wenzake kushindwa kupata mawasiliano mazuri kutoka mahakamani.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka unawakilishwa na Wakili wa Serikali Pius Hilla, Christopher Msigwa na Grace Mwanga huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili wa utetezi Peter Kibatala, Jonathan Mndeme, John Malya na Frederick Kihwelo.

Wakati Mahakama inaendelea, washtakiwa Mbowe na wenzake walikuwa wakionekana kwenye video ya ukumbini hapo lakini wao walikuwa hawaoni kitu ndipo Mbowe akalalamika kuwa, kuwa haoni picha ya mahakamani."Mheshimiwa hatuwaoni, tunawasikia sauti tu lakini hatuwaoni," amedai Mbowe

Wakati marekebisho yakiendelea kufanyika wakili Simba alishauri kuahirishwa kwa kesi iwapo mawasiliano yatashindikana kutengemaa ushauri ambao ulikubaliwa na pande zote mbili.

Baada ya dakika kadhaa za juhudi za wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano kushindikana, washtakiwa waliulizwa kama wako tayari kuendelea kusomewa mashtaka katika hali hiyo lakini Mbowe alikataa na hivyo pande hizo mbili zikakubaliana kurudi mahakamani kesho, kwa makubaliano ya washtakiwa wawepo mahakamani.

Nje ya mahakama kabla ya kuanza kwa kesi, hali ya ulinzi iliimarishwa na kuonekana kuwa shwari bila vurugu zozote ambapo wafuasi wa Chadema walionekana katika maeneo ya nje ya mahakama wakitaka kuingia mahakamani hapo lakini wafuasi wachache asilimia kubwa wakiwa ni viongozi ndiyo walipata nafasi ya kuingia ndani ya ukumbi wa mahakama mtandao.



SOMA ZAIDI HAPA ;CHANZO MICHUZI BLOG











Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464