UNDANI UGONJWA ULIOMUUA MEYA MANISPAA YA SHINYANGA DAVID NKULILA


Meya wa Manispaa ya Shinyanga David Nkulila Enzi za Uhai wake.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA.

MEYA wa Manispaa ya Shinyanga David Nkulila, ambaye alikuwa diwani wa Ndembezi kupitia chama cha mapinduzi CCM, amefariki dunia kwa tatizo la ugonjwa wa Moyo, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani mkoani Shinyanga.

Msemaji wa familia Mary Joseph, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo juu ya kifo cha Meya huyo, alisema kifo cha mpendwa wao kimetokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa 11 alfajiri.

Amesema Marehemu mjomba wake, alikuwa akisumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa Moyo kwa muda mrefu, ambapo alikuwa akilazwa mara kwa mara hospitalini kupatiwa matibabu na kuruhusiwa, lakini siku za hivi karibuni hali yake ilianza kuwa mbaya zaidi na hatimaye kufariki dunia.

“Marehemu ni Mjomba wangu, na kifo chake ni pigo kubwa katika familia yetu, amefariki kwa ugonjwa wa Moyo, ameacha watoto wanne, na mazishi yake yatafanyika siku ya jumatano hapahapa mjini Shinyanga katika Makaburi ya Dodoma,”amesema Joseph.

Naye, Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Ester Makune, amesema kifo hicho kimemshitua sana, sababu walikuwa na mipango mizuri ya kuiletea maendeleo Manispaa hiyo, na kuipeleka kuwa hadhi ya jiji.

Aidha, Diwani wa Kambarage Hassani Mwendapole, amesema kiongozi huyo alikuwa mwenye maono, shupavu, mpenda maendeleo, mzalendo, mchapakazi, mwenye misimamo na malengo, na kubainisha kuwa pengo lake hakuna atakaye weza kuliziba.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Ndembezi Pendo Sawa, amesema kifo cha Meya huyo ni pigo ndani ya chama, sababu alikuwa msema kweli, na mtekelezaji wa ilani ya CCM kwa vitendo.

Historia fupi ya Marehemu David Nkulila

David Mathew Nkulila alizaliwa tarehe 16/04/1964, Tabora mjini, mkoa wa Tabora.

David Mathew Nkulila alianza darasa la kwanza katika shule ya Msingi Bunda mwaka 1974, na baadae Shule ya Msingi Mkendo mwaka 1975, alihamia Shule ya Msingi Old Shinyanga mwaka 1976 na baadaye Shule ya Msingi Mwenge-Shinyanga mwaka 1977 hadi alipohitimu darasa la saba mwaka 1980 katika shule hiyo.

Baba yake mzazi na Marehemu Nkulila alikuwa mtumishi wa serikali hali iliyopelekea Marehemu Nkulila kuhama Shule moja kwenda nyingine ili kumfuata baba yake sehemu alipohamishiwa.

Marehemu David Mathew Nkulila alipata elimu yake ya Sekondari katika Shule ya Sekondari ya Kilimo Kilosa (Kilosa Agricultural Secondary School) kati ya mwaka 1981-1984. Shule hii ya Sekondari ya Kilimo Kilosa ni maarufu hapa nchini kwa kauli mbiu yake ya "Elimu na Kazi"

Baada ya kuhitimu kidato cha nne Marehemu Nkulila alijiajiri na kazi ya Kilimo ambayo ndiyo ilikuwa kazi yake ya msingi hadi mauti yalipomkuta leo 23/08/2021.

Historia yake ndani ya Chama Cha Mapinduzi na majukumu ya kisiasa

Marehemu David Mathew Nkulila ana uzoefu wa kutosha katika masuala ya siasa. Marehemu Nkulila alijiunga na Chama Cha Mapinduzi(CCM) mwaka 1995. Ndani ya CCM Marehemu Nkulila amewahi kushika nyadhifa mbalimbali.

⏩ Marehemh Nkulila amewahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Siasa ya wilaya ya Shinyanga Mjini kati ya mwaka 2013-2017

⏩ Katibu wa CCM Kata ya Ndembezi kati ya mwaka 2007-2012.

⏩ Katibu wa CCM Kata ya Ngokolo.

⏩ Katibu wa CCM Tawi la Bugoyi kati ya mwaka 2003-2007.

Nafasi alizozitumikia

⏩ Marehemu Nkulila amekuwa diwani wa Kata ya Ndembezi kwa vipindi vitatu mfululizo toka mwaka 2010 hadi leo tarehe 23/08/2021 mauti yalipomkuta.

⏩ Marehemu Nkulila amekuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kati ya mwaka 2013-2015.

⏩ Marehemu Nkulila amekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabambasi kati ya 2004 - 2019.

⏩ 2000-2003 Mwenyekiti wa kamati ya WES mtaa wa Mabambasi.

⏩ Amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) kwa zaidi ya miaka 10.

Kazi alizozifanya akiwa Diwani wa Kata ya Ndembezi

Marehemu David Mathew Nkulila kwa kipindi chake chote akiwa kama diwani wa Kata ya Ndembezi alifanikiwa kuwawakilisha vema kwa uadilifu mkubwa wakazi wa Kata ya Ndembezi.

(a)Alisimamia upimaji wa ardhi (viwanja) katika Mitaa ya Ndembezi na Butengwa. Awali mitaa hii ilikuwa na hadhi ya vijiji na ardhi ilikuwa haijapimwa.

(b) Alisimamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara katika viwango vya lami na changarawe ikiwemo mitaro, makalvati, vivuko na madaraja.

(c) Alisimamia ujenzi wa machinjio ya kisasa yaliyopo katika mtaa wa Butengwa.

(d)Alisimamia ujenzi wa Zahanati ya Kata ya Ndembezi iliyopo katika mtaa wa Butengwa. Kwa sasa ujenzi huo upo katika hatua ya boma. Eneo hili la ujenzi wa Zahanati lilipatikana kufuatia juhudi zake akishirikiana na ofisi ya Mtendaji wa kata ya Ndembezi.

(e) Alisimamia utolewaji wa mikopo ya bila riba inayotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kutoka 10% ya mapato yake ya ndani kwa makundi ya vijana, wanawake na walemavu.

Mambo aliyoyapenda (Hobby)

Marehemu Nkulila alipenda kusoma vitabu, majarida na magazeti, Mitandao ya Kijamii na alipenda sana kuendesha baiskeli.

Msemaji wa Familia Mary Joseph akielezea sababu za Kifo cha Mjomba wake David Nkulila.

Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Ester Makune, akielezea namna alivyohuswa na Msiba huo.

Diwani wa Kambarage Hassani Mwendapole, akielezea namna alivyoguswa na Kifo cha Meya David Nkulila.

Katibu wa CCM Kata ya Ndembezi Pendo Sawa, akielezea namna msiba wa Meya huyo ulivyokigusa chama.

Mwananchi Edward Kilanga, akielezea namna alivyoguswa na kifo cha Meya wa Manispaa ya Shinyanga David Nkulila.

Baadhi ya Madiwani Manispaa ya Shinyanga, wakiwa msibani.

Wananchi wakiwa msibani.

Wananchi wakiwa msibani.

Wananchi wakiwa msibani.

Na Marco Maduhu- Shinyanga.

















Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464