WIZARA YA AFYA YAFAFANUA AFYA YA DK. BULUGU, AIHUSIANI NA CHANJO YA UVIKO-19


Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema taarifa zinazosambaa kuwa jana (Agosti 12, 2021) Dk Sospeter Bulugu alipata madhara ya chanjo ya UVIKO-19 na kupelekea kushindwa kusoma hotuba yake wakati wa Mdahalo wa Kisayansi kuhusu ugonjwa huo, zipuuzwe kwani ni uzushi.

Mganga Mkuu wa Serikali leo imetoa ufafanuzi kuwa wakati wa mdahalo huo ambao mgeni rasmi alikuwa Waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima, Bulugu akiongea mada yake alipatwa na kizunguzungu, hali iliyotokana na kushuka kwa sukari kwenye damu ‘Hypoglycemia’ hivyo wataalamu kulazimika kumpatia huduma ya kwanza.

Pia Wizara imeutaka umma kupuuza madai kuwa Waziri wa Afya, alitaka kuficha jambo kuhusu madhara ya chanjo kwa kuvitaka vyombo vya habari visichukue tukio wakati akitekeleza majukumu yake ya maadili ya kitaaluma, kwani ni kinyume na maadili pale panapokuwa na mteja anayepokea huduma za afya ambaye hajaridhia kwa hiari yake kwamba huduma hiyo iwe wazi.

Kwenye video fupi inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii ikionesha tukio hilo imesikika sauti ya Waziri Dk Gwajima ikihoji iwapo Dk Bulugu alikuwa amepata chanjo ambapo baada ya kuthibitika kuwa hajawahi kupata chanjo ya UVIKO-19 sauti yake ilisikika tena ikisema, “basi amepatwa na kushuka kwa sukari hasa ukizingatia tangu kuanza kwa mkutano huo hakukuwa na mapumziko ya chai”.

 

SOMA ZAIDI HAPA


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464