DIWANI AWAPONGEZA MABINTI KUJISHUGHULISHA NA BIASHARA KUJIKWAMUA KIUCHUMI


Diwani wa Viti Maalum Manispaa ya Shinyanga Moshi Kanji wa pili kutoka kulia akiwa na mabinti kutoka Shirika la RAFIKI SDO.
 
Na Josephine Chalres- SHINYANGA

Diwani wa viti maalumu Manispaa ya Shinyanga Mhe. Moshi Kanji, amewapongeza mabinti wa shirika la RAFIKI SDO, kupitia mradi wa EPIC ,kwa hatua waliyoifikia, na kuwaasa kuwajibika katika biashara ndogondogo walizozianzisha kwa lengo la kujikwamua kiuchumi ili kuepuka tamaa na vishawishi.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na mabinti hao katika kikao kilichofanyika ofisi ya Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, ambapo amewataka kuwa na matumizi sahihi ya mitaji waliyonayo ili kuendelea kukuza zaidi biashara zao.

"Niwapongeze na niwatie moyo kwa hatua hii ya mwanzo kwani biashara Ni ngumu lakini sasa muiheshimu mitaji yenu ukikopa mtaji Basi tamaa zingine ndogondogo weka pembeni fanya kazi kwani ukifanya kazi vizuri matokeo yake utayaona na utapata faida , angalieni vitu ambavyo vinawapa faida na usiangalie zaidi vitu ambavyo vinawapa faida kidogo ukaendelea kun'gan'gana navyo unaweza kubadilisha na utaona mabadiliko na kupiga hatua kwenda mbele"

Kwa upande wao mabinti ambao ni wanufaika wamewashukuru waendeshaji wa mradi huo kwa kuwasaidia kupata weledi juu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI pamoja na kuwapatia Elimu ya ujasiriamali ili kuepukana na utegemezi.

"Tumepewa Elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa kujifunza namna ya kujipima pia tumefundishwa jinsi ya kutumia dawa Kinga na pia tumefundishwa kuhusu uzazi wa mpango kwenye akiba na uchumi tumeweza kujifunza namna ya kuweka akiba , kukopa na kukuza biashara zetu ili kutokutegemea Sana wazazi na kujiendesha wenyewe bila utegemezi"

Shirika la RAFIKI SDO linadhaminiwa na serikali ya marekani lenye dhumuni la kusaidia makundi maalumu ikiwemo mabinti kuanzia umri wa miaka 15-24 katika kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa kuwapatia Elimu ya mabadiliko ya tabia na ujasiriamali. 
 
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464