KATIBU MKUU WA JUMUIYA YA WAZAZI CCM ATAKA SHULE YA SEKONDARI KANAWA IONGEZE IDADI YA WANAFUNZI, UFAULU

Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Gilibet Kalima  (aliyevaa miwani) akiwa na viongozi wa Jumuia ya Wazazi mkoa wa Shinyanga pamoja na viongozi wa Chama CCM Kishapu na mkoa wa Shinyanga.

Na Suzy Luhende,Shinyanga
Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Gilibet Kalima amewataka walimu wa shule ya Sekondari Kanawa iliyoko kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kuendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kufaulu vizuri na kuhakikisha wanaongezeka kutoka 162 na kufikia 500.

Hayo ameyasema leo alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi wilayani Kishapu ambapo aliwataka walimu na viongozi wa shule hiyo watumie mbinu mbalimbali ili kuhakikisha wanafunzi wanaongezeka na kuongeza ufaulu zaidi.

"Nimeona taarifa yenu mnajitahidi sana watoto wanafaulu vizuri matokeo ya kidato cha pili na kidato cha nne ni mazuri kinachotakiwa ni kuhakikisha mnakuwa na malengo na kufanya matangazo ya shule yenu ili wazazi wajue kuwa hata wakileta watoto wao watafaulu vizuri kwa sababu walimu wanafundishwa vizuri", amesema Kalima.

"Endeleeni kuhamasisha ili kuhakikisha Kanawa inarudi vizuri"kwani matangazo mazuri ni pale watoto wanapofaulu vizuri wekeni mkakati wa kuitangaza shule yenu ili wanafunzi waongezeke", amesema Kalima.

"Kutokana na uchakavu wa majengo ya shule hii naahidi kuchangia Sh 1 milioni ambayo itatoka kwenye mfuko wa ofisi yetu kwa ajili ya kufanya ukarabati wa majengo haya mmenitia moyo kwa ushirikiano wenu mzuri", aliongeza Kalima.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya Sekondari Kanawa Donbosco Nyanda akisoma taarifa ya shule hiyo amesema shule hiyo ina wanafunzi 162 kidato cha kwanza wapo 15, kidato cha pili 31,kidato cha tatu 56,kidato cha nne 60.

Nyanda amesema changamoto inayosababisha wanafunzi wasiongezeke ni uchakavu wa majengo ya madarasa ambayo yakikarabatiwa na kupakwa rangi wanafunzi wanaweza kuongezeka, kwa sababu shule hii wanafunzi wanafaulu vizuri, wazazi wengi wanashindwa kuleta watoto wao kwa sababu ya majengo kuchakaa.

"Wanafunzi wanaosoma shule hii wanafaulu vizuri tu kwani mwaka 2018 walihitimu 131 mwaka 2019 walihitimu 85 na mwaka 2020 walihitimu 86 waliochaguliwa mwaka 2018 ni 74 mwaka 2019 waliochaguliwa 76 mwaka 2020 waliochaguliwa 55"amesema Nyanda.

Mwenyekiti wa Baraza la wazazi CCM mkoa  wa Shinyanga Alhaji Salm Simba alimshukuru katibu kwa kutembelea mkoa wa Shinyanga na kumuomba kuwa atakapopata nafasi tena aje kuwatembelea na kwamba  maagizo yote aliyoyaacha atayafanyia kazi yeye na viongozi wake.

Katika ziara hiyo pia alikagua kiwanda cha Shinyanga Best Iron cha kutengeneza makarasha kilichopo mjini Shinyanga kinachomilikiwa na Kashi Salula ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji wazazi mkoa alimpongeza kwa juhudi za kukiendeleza kiwanda hicho katika wilaya ya Kahama alitembelea shule ya sekondari ya jumuia ya wazazi ya Wigehe.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464