Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mabinti balehe na akina mama vijana wenye umri kati ya miaka 17 hadi 24 mkoani Shinyanga wameeleza kunufaika na mafunzo mbalimbali yanayotolewa na Mradi wa EPIC unaotekelezwa na Shirika la Family Health International (FHI 360) kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
Hayo yamebainishwa leo Septemba 28,2021 na mabinti wanaosoma katika Chuo cha Ufundi Stadi Veta Mwakata ( St. Francis Vocation Training Center – SFS VTC) wakati waandishi wa habari walipotembelea chuo kujionea shughuli zinazofanywa na mabinti balehe na akina mama vijana.
Mabinti hao na akina mama vijana wamesema mafunzo wanayopata katika chuo hicho yakiwemo ya fani ya umeme, ufundi magari na uchomeleaji yamewafanya kujiamini na kujikubali kuwa wanaweza kufanya kazi zinazofanywa na wanaume ili kujipatia kipato na kubadili maisha yao.
“Tunalishukuru Shirika la FHI 360 kupitia Mpango wake wa DREAMS katika mradi wa EPIC kwa ufadhili wa USAID na PEPFAR kwa kutuwezesha kuja kupata mafunzo haya ambapo baada ya kumaliza kozi tutaweza kujiajiri ama kuajiriwa na kuondokana na hali ya utegemezi hivyo kujiepusha na vishawishi mbalimbali”,amesema Esther Obadia kutoka kata ya Bugarama Halmashauri ya wilaya ya Msalala.
Esther amesema yeye na wenzake 29 walichaguliwa kujiunga na masomo katika chuo hicho kupitia vikundi vya wasichana vinavyosimamiwa na Shirika la FHI 360 na wanatarajia kutumia mafunzo hayo kwa ajili ya kujiari ili kupata vipato.
Naye Mary Edward kutoka kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga amebainisha mafunzo hayo yatawasaidia kujitegemea na kuachana na utegemezi na kuomba omba hivyo kujiepusha kujiingiza kwenye vishawishi vinavyoweza kuwaingiza kwenye mazingira hatarishi yanayopelekea maambukizi mapya ya VVU.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo wa Chuo cha St. Francis Vocation Training Center – SFS VTC Mwakata), Charles Maganga ameishukuru na kuipongeza FHI 360 kwa kuona umuhimu wa kuthamini watoto wa kike na kuwapeleka chuoni hapo kupata mafunzo ambayo yatawasaidia katika maisha yao.
“Mabinti hawa wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi popote iwe kwenye sekta binafsi au serikali. Tunao wanafunzi wa kike 30 waliofadhiliwa na USAID na PEPFAR kupitia mradi wa EPIC ambao wanasoma Fani ya Umeme, Uchomeleaji na ufundi magari, udereva, Kompyuta, ufundi cherehani, saluni na mapambo kwa kipindi cha miezi mitatu", amesema Maganga.
“Fani za umeme, uchomeleaji na ufundi magari zilizoeleka kusomwa na wanaume pekee lakini sasa tuna mabinti wengi zaidi. Hali hii inaonesha rasmi kuwa hakuna kazi inayoweza kufanywa na wanaume pekee au wanawake pekee, na ni ukweli usiopingika kuwa wanawake wana uelewa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi. Naomba serikali iwape kipaumbele vijana hawa kwa kuwapa ajira kwenye miradi mingi inayoendeshwa na serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan”,amesema Maganga.
Afisa Mabinti Balehe na Akina Mama Vijana kupitia mpango wa DREAMS katika mradi wa EPIC, Agnes Junga amesema mabinti balehe na mama vijana hao wanaosoma katika chuo cha SFS VTC Mwakata ni wale wenye umri wa miaka kati ya 15 hadi 24 walio nje ya mfumo rasmi wa shule ikiwa ni sehemu ya kuwaondoa kwenye mazingira hatarishi ili kupunguza hatari ya kupata maambukizi mapya ya VVU kwa kufanya ngono.
Junga amesema wanatekeleza mradi huo katika halmashauri tano za wilaya mkoani Shinyanga ambazo ni Shinyanga, Manispaa ya Shinyanga na Kahama, Ushetu na Msalala. . Miongoni mwa huduma wanazotoa ni elimu ya mabadiliko ya tabia, VVU na UKIMWI, ujasiriamali, Uwezeshaji kiuchumi (kuweka akiba na kukopa) pamoja ufadhili wa masomo na kwa mwaka huu 2021 wamefadhili mabinti 30 kusomea fani ya umeme,ufundi magari, Kompyuta, ufundi cherehani na saluni.
Amefafanua kuwa lengo la mpango wa DREAMS ni kuwaepusha mabinti balehe na akina mama vijana na tabia hatarishi. Hii ni kwa kuwapa mafunzo mbalimbali na mpaka sasa wamefanikiwa kuwafikia na kuwapa elimu ya mabadiliko ya tabia mabinti 84,000, kuwezesha kiuchumi mabinti 56,000 ambapo kati yao 13,000 wameanzisha biashara zao kujikwamua kiuchumi.
Amesema Shirika la Family Health International (FHI 360) kupitia mradi wa EPIC, wafadhili wa mradi USAID na PEPFAR pamoja na asasi za kiraia wanachangia na kusaidiana na serikali katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI kwa makundi yaliyoko kwenye athari za kupata maambukizi ya VVU hasa mabinti.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mwanafunzi Esther Obadia kutoka kata ya Bugarama Halmashauri ya wilaya ya Msalala akielezea kuhusu fani ya umeme na matarajio yake baada ya kumaliza kusoma Kozi ya Umeme katika chuo cha SFS VTC.
Mary Edward kutoka kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga akielezea kuhusu Faida ya kusomea ufundi umeme.
Mabinti balehe na akina mama vijana wenye umri kati ya miaka 17 hadi 24 mkoani Shinyanga wanaosomea Fani ya Umeme wakiendelea na mazoezi kwa vitendo katika Chuo cha Ufundi Stadi Veta Mwakata (SFS VTC).
Mabinti balehe na akina mama vijana wenye umri kati ya miaka 17 hadi 24 mkoani Shinyanga wanaosomea Fani ya Ufundi Magari wakiendelea na mazoezi kwa vitendo katika Chuo cha Ufundi Stadi Veta Mwakata (SFS VTC).
Joyce Michael akiendelea na kazi ya uchomoleaji vyuma katika Chuo cha Ufundi Stadi Veta Mwakata (SFS VTC).
Mratibu wa Mafunzo wa Chuo cha St. Francis Vocation Training Center – SFS VTC Mwakata), Charles Maganga akiishukuru na kuipongeza FHI 360 kwa kuona umuhimu wa kuthamini watoto wa kike na kuwapeleka chuoni hapo kupata mafunzo ambayo yatawasaidia katika maisha yao.
Afisa mabinti balehe na kina mama vijana kupitia mpango wa DREAMS katika mradi wa EPIC, Agnes Junga akielezea kuhusu mpango wa DREAMS katika mradi wa EPIC unaotekelezwa na Shirika la FHI 360 kwa ufadhili wa USAID na PEPFAR.
Mabinti balehe na akina mama vijana wenye umri kati ya miaka 17 hadi 24 mkoani Shinyanga wanaosomea Fani ya Umeme wakiendelea na mazoezi kwa vitendo katika Chuo cha Ufundi Stadi Veta Mwakata (St. Francis Vocation Training Center – SFS VTC) wakipiga picha ya kumbukumbu.
Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Soma pia:
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464