Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Thomas Rutachunzibwa (wa pili kushoto) na Meneja mahusiano wa Sanku, Gwao Omari (kushoto) wakikata utepe kuzindua mashine ya kuongeza virutubishi katika kiwanda cha Kipipa Millers kilicho Sabasaba wilayani Ilemela.
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
KATIKA jitihada za kukabiliana na tatizo la utapiamlo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa linalosababisha udumavu, ukondefu na uzito pungufu kwa watoto hususan walio chini ya miaka mitano na changamoto ya upungufu wa damu kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua, Serikali kwa kushirikiana na wadau wamezindua programu ya urutubishaji unga wa mahindi.
Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Juni 2021, mkoa wa Mwanza ulikuwa na jumla ya watoto wenye udumavu asilimia 0.6, watoto waliozaliwa hai wenye uzito chini ya kilo 2.5 ni asilimia 6, watoto wenye uzito pungufu ni asilimia 9, ambapo asilimia 76 ya akina mama walipewa vidonge vya kuongeza damu ili kupambana na tatizo la upungufu wa damu wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua.
Afisa Lishe mkoa wa Mwanza, Sophia Lugome
Programu hiyo ilizinduliwa Septemba 2, mwaka huu katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Mwanza, ambapo lengo ni kuongeza matumizi ya vyakula vilivyoongezwa viini lishe vyenye madini ya chuma, zinki, Vitamini B12 na foliki asidi kupitia kwa wazalishaji wadogo ambao wanawezeshwa mashine, vinu, virutubishi na vifungashio.
Kwa mujibu wa Afisa Lishe mkoa wa Mwanza, Sophia Lugome
sababu zinazochangia kuendelea kuwepo tatizo la utapiamlo mkoani hapa ni wazazi kutofuata ushauri wa wataalam wa afya kama vile matumizi ya njia za uzazi wa mpango, kutozingatia ulaji unaofaa kwa watoto hasa kwa kufuata makundi matano ya vyakula ili kupata mlo kamili na watoto kulishwa vyakula vya aina moja.
Akinukuu utafiti wa kitaifa wa lishe (TNNS) wa mwaka 2018, ameeleza kuwa hali ya udumavu kitaifa ni asilimia 30, mkoa wa Mwanza ukiwa na asilimia 29.3, ukondefu ukiwa asilimia 1.7, uzito mdogo asilimia 8.5 na upungufu wa damu kwa watoto chini ya miaka mitano ni asilimia 52 na akina mama wenye umri wa kuzaa (miaka 15-49) ni asilimia 42.
Ametaja mikakati inayofanyika kupunguza tatizo la utapiamlo mkoani hapa ni kuendelea kuhamasisha wazazi kuhudhuria kliniki ya huduma ya mama, baba na mtoto kwa pamoja ili wapate elimu ya malezi na makuzi bora ya mtoto, kutoa elimu ya lishe kwenye kliniki, kuendelea kutoa matone na vyakula dawa na kuelimisha jamii kuhusu vyakula bora vyenye lishe inayofaa kwa watoto ili kupata lishe bora na kuwakinga na magonjwa mbalimbali.
Mkakati mwingine ni kuwasisitiza akina mama kuwanyonyesha watoto walio chini ya miezi sita maziwa ya mama pekee pamoja na kuwapa nyongeza ya chakula baada ya miezi sita ili kupunguza uwezekano wa watoto walio chini ya miaka mitano kuwa katika hatari ya kupata utapiamlo kwani kwa sasa mkoa huo una asilimi 58 ya unyonyeshaji sahihi.
“Lishe ni suala la msingi katika makuzi na malezi ya mtoto ndani ya siku 1000, ukosefu wa lishe bora huwasababishia watoto kupata hali ya utapiamlo ambayo viashiria vyake ni udumavu, ukondefu na uzito mdogo au uliokithiri. Pamoja na jitihada ambazo serikali inafanya na wadau wa maendeleo, bado tatizo la utapiamlo nchini ni kubwa hali ni mbaya zaidi kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na akina mama wajawazito na wanaonyonyesha,” amesema Sophia.
Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dk.Thomas Rutachunzibwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Thomas Rutachunzibwa alisema akina mama wengi wanafika kliniki ujauzito ukiwa umefikisha miezi mitano hadi sita hivyo kuchelewa huduma muhimu yakiwemo matone ya vitamin na damu ambayo humsaidia mtoto kukua vyema hususan utengenezaji wa ubongo (mfumo wa fahamu).
“Ubongo huanza kuumbika baada ya wiki sita, sasa mama akichelewa ndiyo hayo matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi na mfumo wa fahamu huwepo, hivyo urutubishaji wa vyakula utawaokoa watoto wengi nchini kwani tatizo la watoto wenye vichwa vikubwa linatia huruma na ni mzigo kwa wazazi,” amesema.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kitengo cha lishe, Peter Kaja alisema kutokana na uhalisia kwamba Watanzania wengi wanatumia chakula cha mafuta, unga wa mahindi na ngano na chumvi Serikali imevipa kipaumbele vyakula hivyo kwa kuwataka wazalishaji wenye viwanda kuhakikisha ni lazima kabla ya kuuza bidhaa hizo ziwe zimeongezewa virutubisho muhimu ambavyo ni vitamin B12, madini chuma, madini ya zinki na foliki aside ili wananchi wengi wapate lishe.
Kaja alisema changamoto ya watoto na akina mama wajawazito kukosa viini lishe husababisha matatizo ya watoto kuzaliwa na vichwa vikubwa, mgongo wazi na wanawake kupungukiwa damu wakati wa kujifungua na kusababisha vifo vingi vitokanavyo na uzazi.
Meneja Uhusiano wa taasisi ya Sanku inayojihusisha na kuondoa changamoto za lishe duni Afrika, Gwao Omari alisema mradi wa virutubisho kwenye unga wa mahindi waliouzindua unalenga kuwawezesha wazalishaji kwa kuwapa mashine, vinu, mifuko ya kufungashia na virutubisho katika mikoa sita ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Kagera, Geita, Simiyu, Mara na Shinyanga ili kuongeza upatikanaji wa unga salama uliorutubishwa ikiwemo kwenye shule ambako ndiko kuna watumiaji wengi.
Alisema wameshafunga mashine 20 mkoa wa Mwanza, 23 Kanda ya Ziwa na 600 nchi nzima huku wakilenga ifikapo mwaka 2025 wawe wamefunga mashine 2,000 ili kuhakikisha teknolijia na virutubisho vinapatikana nchini wakati wote.
Mkurugenzi wa kampuni ya Kipipa Millers kilichopo wilayani Ilemela kinachozalisha unga wa mhogo na mahindi ulioongezwa virutubisho vya Vitamini B12, foliki aside, madini ya zinki na chuma, Jofrey Peter amesema kwa sasa wanazalisha tani tatu hadi nne kwa siku na chakula hicho ni bora kwa watu wote wakiwemo wajawazito, wanaume na watoto kwani kinasaidia kuimarisha afya ya mwili na akili.
Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Thomas Rutachunzibwa akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Thomas Rutachunzibwa (wa pili kushoto) na Meneja mahusiano wa Sanku, Gwao Omari (kushoto) wakikata utepe kuzindua mashine ya kuongeza virutubishi katika kiwanda cha Kipipa Millers kilicho Sabasaba wilayani Ilemela.
Meneja mradi wa TechnoServe, Gertrude Kawau akieleza namna wanavyoshiriki kusaidia teknolojia ya uzalishaji wa vyakula vyenye virutubishi
Meneja Uhusiano wa taasisi ya Sanku inayojihusisha na kuondoa changamoto za lishe duni Afrika, Gwao Omari akieleza namna kampuni hiyo inavyoshiriki kuwawezesha wazalishaji mashine, vinu na virutubishi ili kupambana na lishe duni
Wadau wa afya wakifuatilia mijadala kwenye kikao hicho
Kikao kikiendelea
Washiriki wakifuatilia hoja mbalimbali kuhusu utapiamlo na umuhimu wa virutubishi ili kujenga afya ya jamii
Unga wa sembe unaozalishwa na kampuni ya Kipipa Millers ambao umeongezwa virutubishi vya madini ya chuma na zinki, vitamini B12 na Foliki asidi.