MWANRI ATAKA KILIMO CHA PAMBA CHENYE TIJA



Balozi wa zao la pamba nchini Tanzania Aggrey Mwanri

Suzy Luhende, Shinyanga

Balozi wa zao la pamba nchini Tanzania Aggrey Mwanri, amewataka wataalamu wa kilimo kusimamia wakulima, ili waweze kulima kilimo chenye tija ambacho kitazingatia kanuni bora za kilimo cha zao hilo, na kuweza kulima hekta 80 sawa na ekari 20, 000 za pamba ,na kupata mavuno ya tani 100,000 kwa wilaya ya Kishapu.

Hayo ameyasema jana katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kuhamasisha kuongeza tija katika zao la pamba wilayani humo, kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya sekondari ya Kishapu, ambapo alisema huu ni wakati wa mabadiliko kwa wakulima wanatakiwa kulima kilimo chenye tija ambacho kitamkomboa mkulima na kuachana na kilimo cha kupanda mbegu kwa kumwaga.

Balozi Mwanri amesema wakulima wamekuwa wakitumia Nguvu nyingi kwa kulima mashamba makubwa ambayo hayana faida, hivyo ni vizuri wabadilike wayafanyie usafi mashamba yao na kiyapalilia kwa wakati na kupunguzia miche, waondoe maotea, masalia na mabaki ambayo yamekuwa yakisababisha njaa kwa familia nyingi.

Mwanri amesema akiwa na timu ya bodi ya pamba na maafisa ushirika wamefanikiwa kufikia vijiji 25 na kuhudhuliwa na jumla ya wakulima 2,323, ambapo lengo lilikuwa ni kufika jumla ya vijiji 82 katika wilaya ya Kishapu, lakini kwa vijiji ambavyo hawakuvifikia wataalamu wa kilimo watavifikia na kutoa elimu kabla ya msimu wa kilimo wa 2021/2122 kuanza.

"Tani 100, 000 zinawezekana pale mkulima atakapolima kwa kutumia sentimita 60 kwa sentimita 30 na kupanda Miche 44,444 katika heka moja, kuweka mbolea za samadi na virutubisho vingine ili kuweza kuboresha mashamba ni vizuri mkalima heka tatu na kuachana na kulima mashamba kumi ambayo hayana tija na inatakiwa ipaliliwe vizuri"amesema Balozi Mwanri.

Ziara ya balozi Mwanri ilianza tarehe 24/8/ 2021 katika wilaya ya Kishapu ambapo walitembelea vijiji 25, hata hivyo mkoa mzima wanatarajia kupata tani 130, 000 ambapo Kahama itatoa tani 15, wilaya ya Shinyanga tani 15 na Kishapu ambako ndiko kwenye pamba nyingi tani 100, 000.

Kwa upande wake Renatus Luneja ambaye ni mkaguzi wa pamba kutoka Mwanza bodi ya pamba (TCB) alisema bodi hiyo imejipanga vizuri kupeleka mbegu mapema kwa mkulima, hivyo maafisa ugani wote ambao hawana usafiri wa pikipiki watapewa pikipiki na kujaziwa mafuta ili kuweza kuwafikia wakulima kwa wakati na viongozi wasimamie pembejeo zitakazolewa na kutoa elimu kwa wakulima.

Naye afisa kilimo umwagiliaji na ushirika wilaya ya Kishapu George Kessy alisema wilaya imejipanga vizuri kutoa elimu kwa wakulima na kusimamia kanuni za kilimo bora cha pamba na itaimalisha vikosi kazi vya kusimamia kuanzia ngazi ya Kijiji, kata na ngazi ya wilaya na kila mkulima anatakiwa kulima ekari tatu, na kila ekari moja Kuna uwezekano wa kupata kilo 2500 badala ya 1500.

Diwani wa kata ya Kishapu Joel Ndetoson amesema wananchi walikuwa wakilima kwa holela kwa sababu walikuwa hawana elimu, ndiyo maana walikuwa wanalima kwa holela lakini kwa Sasa wakielimishwa wote ninaimani watabadilika watalima kwa tija na tani 100, 000 zitafika.

Baadhi ya wananchi Mary Mlyambinga kutoka kata ya Mihama na Mgaka Pastory wamesema watashirikiana na maafisa ugani kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima kwani mkakati ulioandaliwa na serikali ni mzuri umelenga kumkomboa Mwananchi na kumuondoa kwenye umasikini.


Balozi wa zao la pamba nchini Tanzania Aggrey Mwanri

Kiongozi mbalimbali, maafisa ugani watendaji wa kata na maafisa ushirka wakiapa kwamba watasimamia zao hilo ili kufikisha tani 100,000.

Afisa kilimo wa mkoa wa Shinyanga Wilson Mng'ong'ng'o akiwahimiza wakulima kulima kwa kuzingatia kanuni na taratibu.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464