Waziri wa Katiba na Sheria (Kushoto) Mh.Profesa Palamagamba Kabudi akifungua jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara lililoko katika Mji Mdogo wa Mugumu
Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe.Profesa Palamagamba Kabudi amesema umefika,wakati sasa wa
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuongeza kasi
ya kusimamia makosa ya uharibifu wa mazingira kwa ukubwa wake badala ya kazi
hizo kufanywa na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira ( NEMC)
pekee kwakuwa uharibifu wa mazingira ni kosa ni uhujumu uchumi.
“Mazingira
yetu yanazidi kuharibiwa sana, kuharibu mazingira ni kosa la jinai. Tunakata
miti bila huruma. Umefika wakati sasa jukumu la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka
katika kusimamia na kutunza mazingira lionekane wazi ili watu wajue kuwa
kuharibu mazingira ni kosa la jinai na ni uhujumu uchumi.
Mhe.
Kabudi ameyasema hayo katika hafla ya ufunguzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka wilaya ya Serengeti zilizofanyika mjini Mugumu leo tarehe 21 Septemba,
2021 ambapo alisema sasa kuna umuhimu wa kuipitia Sheria kuu “Penal Code” ili kuhakikisha baadhi ya makosa yanayohusiana na
uharibifu wa mazingira na maliasili yanaingizwa.
Alisema
uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilaya ya Serengeti litasaidia
kusogezwa kwa karibu kwa huduma za
mashtaka kwa wananchi pamoja na kuipunguzia serikali gharama za uendeshaji kesi na pia
itasaidia kupambana na ujangili katika wilaya ya Serengeti.
Mhe.
Kabudi alisema uhifadhi wa maliasili za nchi yetu unahitaji ukali wa
sheria ili kudhibiti vitendo viovu na kutaka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka
kuyachukulia kwa uzito makosa hayo kwa kuwa yanahujumu uchumi ambapo alitaka
maeneo yote yenye maliasili kuwa na Mawakili wa Serikali ili kupambana na
makosa ya uharibifu wa mazingira.
Aidha,
Mhe. Kabudi alitumia fursa hiyo kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua
ya kupata ofisi na wadau wote waliohisani na kuhakikisha kuwa jengo la Ofisi ya
Taifa ya Mashtaka linajengwa.
Naye
Mkurugenzi wa Mashtaka Ndg. Slyvester Mwakitalu alisema uwepo wa jengo la Ofisi
ya Taifa ya Mashtaka wilayani Serengeti utasaidia kuboresha utendaji kazi na
kuongeza kasi ya utendaji kwakuwa mazingira ya utendaji kazi utakuwa
umeboreshwa.
Alisema
ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilaya ya Serengeti ni jambo la
kujivunia kwakuwa ni jengo la kwanza kujengwa tangu kuanzishwa kwa Ofisi yaTaifa
ya Mashtaka mnamo mwezi Februari 2018. Aidha. Aliwashuru wadau wa Makampuni ya
GRUMET kwa kufadhili ujenzi wa jengo hilo na kuwaomba wadau wengine pia
kujitokeza kufanya hivyo wanapoombwa kuhisani ujenzi.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mhe. Vincent Mashinji akizungumza katika hafla hiyo
alisema uwepo wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilaya ya Serengeti utasaidia
kuboresha huduma na utaipunguzia serikali gharama za uendeshaji wa kesi na
upelelezi ambapo aliahidi kuongeza ushirikiano katika utendaji wa kazi.
Aidha, Mhe. Mashinji aliwataka wakazi wa Serengeti kutii sheria bila shuruti na kuitumia ofisi hiyo kwa kutoa ushirikiano mzuri pale wanapohitajika kutoa ushahidi hali ambayo itapelekea kesi kuisha kwa wakati.Mwonekano wa mbele wa Jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti Mjini Mugumu Mkoani Mara
Viongozi mbalimbali wakiendelea kufuatilia na kutazama burudani wakati wa ufunguzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashataka Seregenti Mara
Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi akitoa tuzo ya zawadi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Grumet Fund Bw. Noel Mbise ikiwa ni sehemu ya kkutambua mchango wao kwenye ujenzi wa jengo hilo wakati wa ufunguzi wa Jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464