USHIRIKINA WAZUA HOFU HOSPITALI YA WILAYA NKASI, MADAKTARI WAVUTWA MIGUU, WAZIMIWA TAA.




NA MWANDISHI DIRAMAKINI


Uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa umelalamikia vitendo vya kishirikina vinavyofanywa hospitalini hapo.

Hali hiyo inatajwa kuhatarisha usalama kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo na kuzua hofu.


Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Martha Chacha ameyabainisha hayo wakati akitoa taarifa kwenye kikao kazi kilichojumuisha wataalamu,viongozi wa ngazi ya jamii na wakunga wa jadi leo.


Amedai kuwa, hali iliyopo sasa inatisha ambapo watendaji wa hospitali hiyo wamekuwa wakitishwa na mauza mauza yaliyopo katika hospitali hiyo hasa nyakati za usiku.


Mganga huyo amesema kuwa, vitendo hivyo vya kishirikina vimekuwa vikififisha ari ya kufanya kazi kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo kwa maana ya wauguzi, manesi na wengineo wawapo zamu za usiku.


Pia anasema, ukwamishwa kufanya kazi zao kwa kukumbana na mauza uza kama vile kuvutwa miguu na kitu kisichoonekana,kuzima taa na kuziwasha wakiwa wanatoa huduma mbalimbali kwa wagonjwa.

Mganga huyo amesema kuwa, watumishi wengi wa hospitali hiyo ukataa kupangwa zamu za usiku na kuifanya kazi yao kuwa ngumu kiasi cha wengine kufikiria kuomba uhamisho kwenda kufanya kazi katika maeneo mengine.


Hivyo amewaomba wazee wa eneo hilo kukaa na kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo kwa haraka ili waendelee kutoa huduma kwa jamii katika hospitali hiyo.


Pia amewataka wananchi kuendelea kuitumia hospitali hiyo ya wilaya na kudai kuwa toka waanze kutoa huduma kwa muda wa mwaka mmoja sasa kasi ya wagonjwa wanaokwenda kupata huduma katika hospitali hiyo ni ndogo ukilinganisha na idadi ya wagonjwa waliopo.


Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi wa hospitali hiyo, Crementina Kaishozi kwa upande wake amewataka wakunga wa jadi kuacha mara moja kuwazalisha akina mama wajawazito bali kazi yao iwe ni kuwasindikiza wateja wao hospitalini.


SOMA ZAIDI HAPA 
CHANZO DIRA MAKINI
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464