OPE YAKABIDHI MRADI WA KUPINGA MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI KISHAPU


Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la OPE bw. Nunya Chege akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mifuko 10 ya Simenti iliyotolewa na Shirika la OPE kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya madarasa shule ya sekondari ya Ng’wanima iliyopo Kata ya Busangwa Wilaya ya Kishapu.

Na Josephine Charles - Kishapu
Shirika lisilo la Kiserikali la Organization of People Empowerment (OPE) limekabidhi Mradi wa kupinga Mimba na ndoa za utotoni kwa viongozi wa Serikali kata ya Busangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga hususani kamati ya maendeleo ya kata hiyo.

Mradi huo uliofadhiliwa na Shirika la Firelight Foundation la Marekani na kutekelezwa na shirika la OPE la mkoani Shinyanga ulianza tangu mwaka 2015 na umehitimishwa Oktoba , 2021 kwa tafrija iliyofanyika katika shule ya sekondari ya Ng’wanima iliyopo Kata ya Busangwa Wilaya ya Kishapu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Afisa Kilimo wa Kata ya Busangwa Bwana Mafwele Mafwele ametoa maagizo kwa Kamati ya Maendeleo ya Kata hiyo kuwa ajenda ya kuendelea kupinga mimba na ndoa za utotoni iwe ni kipaumbele katika vikao vyao.

“OPE wao wamekamilisha mradi huo kilichobaki ni sisi kuendeleza kuutekeleza kwa vitendo,siyo OPE wanaondoka na huku sisi mimba na ndoa za utotoni zinaendelea itakuwa ni aibu kwetu”, amesema Mafwele.

Mafwele ametumia nafasi hiyo kuwaomba Shirika la OPE kupitia kwa Mkurugenzi wake Bw. William Shayo kwamba wakipata mradi mwingine zaidi ya huo wasisite kuwapataia tena kata ya Busangwa kama walivyofanya kwa mradi wa kupinga Mimba na Ndoa za Utotoni.

Awali akisoma taarifa ya mradio huo, Afisa Jinsia na ulinzi wa mtoto kutoka shirika la OPE Bi. Mariam Saguda ameeleza malengo ya mradi huo kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii juu ya mambo yanayochochea matukio ya mimba na ndoa za utotoni kupitia matamsha mbalimbali yaliyohusisha makundi lengwa, kuweka mipango imara ya kuachana na vichocheo hivyo,kuimarisha ustawi wa familia au kaya kupitia mafunzo wanayoyatoa na kushawishi utekelezaji wa sheria na sera mbalimbali zinazomlinda mtoto.

Bi. Saguda ameleeza baadhi ya mafanikio waliyopata kupitia mradi huo ni jamii kupata mwamko mkubwa wa kutoa taarifa za matukio ya mimba na ndoa za utotoni pamoja na matukio mengine ya ukatili wa kijinsia,uelewa wa malezi na makuzi ya mtoto kuongezeka kwa asilimia 35,Kaya 16 za kata ya Busangwa zilipatiwa mafunzo na kuwezeshwa kupatiwa mafunzo ya ufugaji wa kuku ili kuboresha kipato cha familia.

Pia wamefanikiwa kuwapa rufaa na kuwasaidia wahanga sita wa mimba na ndoa za utotoni kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika chuo cha Urambo na Didia lakini pia matukio ya mimba na ndoa za utotoni katika kata hiyo yamepungua kwa wastani wa asilimia 40 kwa mwezi,kuunda mabaraza ya watoto kwa ngazi ya vijiji vya kata zote za Busangwa pamoja na kupata ushirikiano wa kutosha kutoka ngazi ya halmashauri idara ya maendeleo ya jamii ngazi ya kata na vijiji vyote .

Ameeleza kuwa katika utekelezaji wa mradi walibaini baadhi ya changamoto zikiwemo baadhi ya kamati za MTAKUWWA hazikai kwa mujibu wa mwongozo wa sheria jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za kutetea haki za mama na mtoto,kutokuwa na utayari wa kutekeleza shughuli ambazo zinaletwa na mashirika yasiyo ya serikali bila posho,kuibuka kwa janga la Covid-19 kuliathiri kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa mradi na waathirika wa matukio ya ukatili wa kijinsia kushindwa kutoa ushahidi Mahakamani na kesi kumalizwa kimya kimya nyumbani baina ya familia husika.

Wakati huo huo, Shirika la OPE limekabidhi mifuko 10 ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya madarasa shule ya sekondari ya Ng’wanima iliyopo Kata ya Busangwa Wilaya ya Kishapu.


Akikabidhi Mifuko hiyo ya simenti Mkurugenzi wa shirika hilo Bw. William Shayo amesisitiza kuwa Mradi haujafungwa isipokuwa kilichoisha ni nguvu ya kuendelea kusaidia katika harakati za kupinga mimba na ndoa za utotoni na amewaomba kuendeleza harakati hizo za kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Organization of People Empowerment (OPE) William Shayo akizungumza wakati wa kukabidhi Mradi wa kupinga Mimba na ndoa za utotoni kwa viongozi wa Serikali kata ya Busangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga. Picha zote na Josephine Charles
Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Busangwa John Paul Gambishi akizungumza wakati wa hafla ya kufunga Mradi wa kupinga Mimba na ndoa za utotoni kwa viongozi wa Serikali kata ya Busangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga

Afisa Jinsia na ulinzi wa mtoto kutoka shirika la OPE Bi. Mariam Saguda akizungumza wakati wa hafla ya kufunga Mradi wa kupinga Mimba na ndoa za utotoni kwa viongozi wa Serikali kata ya Busangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga
Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Ope Bi. Pendo Msomi akizungumza wakati wa hafla ya kufunga Mradi wa kupinga Mimba na ndoa za utotoni kwa viongozi wa Serikali kata ya Busangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la OPE bw. Nunya Chege akizungumza wakati wa hafla ya kufunga Mradi wa kupinga Mimba na ndoa za utotoni kwa viongozi wa Serikali kata ya Busangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga
Afisa Kilimo wa Kata ya Busangwa Bwana Mafwele Mafwele akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, wakati wa hafla ya kufunga Mradi wa kupinga Mimba na ndoa za utotoni kwa viongozi wa Serikali kata ya Busangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la OPE bw. Nunya Chege akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mifuko 10 ya Simenti iliyotolewa na Shirika la OPE kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya madarasa shule ya sekondari ya Ng’wanima iliyopo Kata ya Busangwa Wilaya ya Kishapu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la OPE bw. Nunya Chege akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mifuko 10 ya Simenti iliyotolewa na Shirika la OPE kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya madarasa shule ya sekondari ya Ng’wanima iliyopo Kata ya Busangwa Wilaya ya Kishapu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la OPE bw. Nunya Chege akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mifuko 10 ya Simenti iliyotolewa na Shirika la OPE kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya madarasa shule ya sekondari ya Ng’wanima iliyopo Kata ya Busangwa Wilaya ya Kishapu.
Picha ya kumbukumbu baada ya Shirika la OPE kukabidhi mifuko 10 ya Simenti na Mradi wa kupinga mimba na ndoa za utotoni wilayani Kishapu.

Picha zote na Josephine Charles - Kishapu

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464