BITEKO AFUNGUKA SHERIA KULINDA RASILIMALI ILIVYOLETA MAPINDUZI SEKTA YA UZIDUAJI, AKEMEA MASUALA YA RUSHWA


Waziri wa Madini Dotto Biteko, akizungumza kwenye Mdahalo.

Na Marco Maduhu, DODOMA

WAZIRI wa Madini Dotto Biteko, ameeleza namna Sheria ya kulinda Rasilimali za Nchi ya mwaka 2017 ilivyoleta mapinduzi katika Sekta ya uziduaji kwa kuongeza Pato la Taifa, kuvutia wawekezaji, pamoja na Wazawa kunufaika na Rasilimali zao ikiwamo kutoa huduma ndani ya migodi (Local Content).

Waziri Biteko amebainisha hayo jana Jijini Dodoma kwenye mdahalo wa kujadili, namna gani Serikali inavyoweza kuweka ulinganifu katika kuongeza mapato ya Serikali na kuvutia wawekezaji, kufuatia kuwepo na Sheria ya kulinda Rasilimali za Taifa, mdahalo ulioadaliwa na Taasisi ya HakiRasilimali ambayo imejikita kwenye Sekta ya uziduaji Madini,Oil na Gesi.

Biteko alisema, Sheria hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa Wazawa kunufaika na madini yao pamoja Serikali kuongeza mapato, ambapo wachimbaji wadogo wamepewa nguvu zaidi kushiriki kwenye uchumi wa madini, pamoja na wananchi kutoa huduma kwenye migodi na siyo kutumia tena makampuni kutoka nje ya nchi.

“Baada ya kurekebisha sheria hii Serikali tumepata manufaa makubwa sana na mapato yameongezeka na tumepata rekodi ambayo hatujawahi kuipata, mwaka juzi kwenye Sekta ya madini tulikusanya Sh. bilioni 526, na kabla ya mwaka huu wa fedha tumekusanya Sh. 586, na Sekta ya madini ikaongoza kwenye uziduaji kwa mara ya kwanza na ikawa sekta ya kwanza kwa kukua mwaka 2019 kwa kukua kwa asilimia 17 ”alisema Biteko.

“Lakini kwenye kuleta fedha kutoka nje ya nchi Sekta hii ikaongoza vilevile ikaleta asilimia 51.9 ya fedha zote zinazoletwa ndani ya nchi, mauzo kutoka ndani kwenda nje Sekta ikaongoza pia, tumeendelea na kusimamia sekta ya madini, lakini changamoto hatuwezi kuzimaliza kama ilivyo katika maisha yetu,”aliongeza Biteko.

Akizungumza kwa upande wa uwekezaji, alisema kwa mara ya kwanza hapa nchini ndani ya miaka 15 iliyopita haijawahi kufungua mgodi mkubwa hata mmoja, lakini baada ya marekebisho hayo ya sheria, kwa sasa wawekezaji wamekuja nchini na kufungua migodi mikubwa ukiwamo mgodi wa Nyanzaga wa dhahabu ambao utawekeza dola za kimarekani Sh,milioni 499 na kuajiri watu 1,200. na utaajiri watu kwenye maeneo yasiyokuwa rasmi watu 300 hadi 500.

Pia, alisema kuna Mgodi mwingine upo Songwe, wenye utawekeza dola la kimarekani Sh,milioni 196 na utaajiri watu 120 , na mradi mwingine upo Kambanga ambao utachimba madini ya Nicon, ambao wenyewe utawekeza dola za kimarekani Sh. milioni 112 na ajira 1200, na mradi huo utakuwa na maisha ya miaka 30, na Serikali itapata asilimia 59 mwekezaji asilimia 41, na kwa maisha yote hayo Serikali itapa fedha dola la kimarekani Sh.bilioni7.59.

Akizungumzia masuala ya Wazawa kutoa huduma kwenye Migodi (Local Content), alisema baada ya marekebisho ya sheria hiyo, kwa sasa Serikali imebana huduma za kwenye makampuni ya migodi, nyingi zitolewe na Watanzania na siyo watu kutoka nje nchi, ambapo kwa sasa hawawezi kutumia makampuni ya nje bila ya kutoa Taarifa kwenye Wizara hiyo na kujiridhisha kama huduma inayohitaji haipo Tanzania.

“Katika Mgodi wa Geita Goldmine hua unatumia Dola za Kimarekani Sh.milioni 600 kwa mwaka kufanya manunuzi ya vifaa na huduma, je fedha hizi zinakwenda wapi, na ndiyo maana Serikali tunataka Wazawa wawe wanatoa huduma kwenye migodi mikubwa ya madini, ili fedha hizi zibaki kwa Watanzania na kunufaika na Rasilimali zao,” alisema Bitteko.

Katika hatua nyingine Biteko, alisema katika kufanikiwa katika Sekta ya Madini ni kupambana na vitu vitatu moja kuondoa Rushwa, Pili Mwekezaji apewe lesseni kwa wakati pale anapoomba leseni, na tatu ni kutabilika kwa Kodi, na kubainisha kuwa Serikali imeondoa Kodi nyingi sana katika Sekta hiyo ya madini.

Aidha mwaka 2017 Bunge la Tanzania lilipitisha Miswada ya sheria ya ulinzi wa Rasilimali za Taifa, ambazo zililenga kudhibiti usafirishaji wa makinikia kwenda nje ya nchi, viwango vya Tozo vya Mrabaha vilipanda kutoka asilimia 3 hadi 6, pamoja na Serikali kupata asilimia 16 za hisa kutoka kwenye makampuni makubwa ya uchimbaji madini, lengo likiwa ni upataji wa mapato.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe akizungumza suala la kuvutia wawekezaji kwenye mdahalo huo, alisema wameweza kuandaa andiko la kuweka mazingra wezeshi ya ufanyaji biashara, kwa kuhakikisha wanapunguza changamoto ili kuvutia wawekezaji, kwa kuondoa urasimu na ukiritiba usio wa lazima, ambao ulikuwepo na kupelekea kuzuia wawekezaji wa ndani na nje.

Aidha, alisema pia wanaangalia jinsi Rasilimali za Madini, Oil na Gesi zitakavyo wanufaisha Watanzania, kwa kushiriki katika miradi katika utoaji wa huduma, na kubainisha moja ya mradi wa Oil kutoka Hoima Uganda hadi Tanga ambapo wanatoa Fursa kwa Sekta binafsi za Wazawa kutoa huduma ya vifaa vikwamo vya ujenzi.


Waziri wa Madini Mhe, Dotto Biteko, (katikati) akiwa kwenye Mdahalo, (kushoto kwake) ni Naibu Waziri wa Nishati Mhe, Stephen Byabato, na (kulia) ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe, wakwanza kulia ni Racheal Chagonja Mkurugenzi wa HakiRasilimaliM na kushoto ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi Ezekiel Kamwaga.

Washiriki wakifuatilia mdahalao huo.

Washiriki wakifuatilia Mdahalo huo.

Na Marco Maduhu, DODOMA



















Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464