KAMATI YA BUNGE, VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA, YATEMBELEA MGODI WA MWIME KUONA MATUMIZI YA ZEBAKI KWA WACHIMBAJI WADOGO


Kamati ya Bunge,Viwanda, Biashara na Mazingira wakiangalia shughuli za utafuta madini ya dhahabu katika Mgodi wa Mwime Manispaa ya Kahama.

Na Marco Maduhu, KAHAMA.

KAMATI ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira, imefanya ziara ya kutembelea Mgodi wa machimbo ya dhahabu uliopo Mwime Manispaa ya Kahama, ili kuona matumizi ya Kemikali ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo na athari zake.
 
Kamati hiyo imefanya ziara leo, ikiwa imeambatana na wajumbe wake chini ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mbunge wa Jimbo la Mfindi Kusini David Kihenzile, pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Seleman Jafo.

Akizungumzia malengo ya ziara hiyo Mwenyekiti wa kamati Mhe Kihenzile, alisema wamefanya ziara hiyo ili kuona namna ya utunzaji wa mazingira kwenye migodi midogo ya madini, pamoja na wanavyochukua tahadhari dhidi ya matumizi ya kemikali ya Zebaki ili kutowaathiri afya zao, wakati Serikali ikiendelea na utaratibu wa kutafuta njia mbadala ya ukamataji dhahabu na kuachana na Zebaki.

Alisema wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu hapa nchini, wamekuwa wakitumia sana Kemikali ya Zebaki kukamatia dhahabu, bila ya kuzingatia usalama wa afya zao, na kusababisha kupata madhara ya kiafya na hata kuathiri vizazi na vizazi.

"Sisi kamati ya bunge, viwanda, biashara na mazingira, tumekuja katika Mgodi huu wa machimbo ya dhahabu Mwime, kuona namna ya utunzaji wa mazingira na matumizi ya Zebaki, na kile ambacho tumekiona hapa tutapeleka mrejesho kwa Spika wa Bunge Job Ndugai," alisema Kihenzile.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Seleman Jafo, alisema wakati Serikali ikiendelea na utafiti wa kutumia njia mbadala ya kukamatia dhahabu na kuondokana na matumizi ya Kemikali ya Zebaki, amewataka wachimbaji wavae vifaa kinga wakati wa matumizi hayo ya Zebaki ili kutoathiri Afya zao.

Aidha, alisema katika Hospitali ya Ocean Road Jijini Dar es salaam, inaonyesha Takwimu kubwa ya wagonjwa wenye Saratani wanatoka Kanda ya Ziwa, na hiyo inawezekana sababu ya matumizi ya Kemikali ya Zebaki kwenye uchimbaji wa madini.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo, aliwaagiza wataalam wa Mazingira, wafike kwenye migodi midogo ya madini ya dhahabu, na kutoa elimu kwa wachimbaji hao namna ya utunzaji wa mazingira, pamoja na kuchukua tahadhari ya matumizi ya kemikali ya Zebaki.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu, Mkoa wa kimadini Kahama Joseph Andrew, alisema wachimbaji wengi hawana elimu ya utunzaji mazingira, wala namna ya kujikinga na athari za Kemikali ya Zebaki.

Alisema, Shughuli nyingi ambazo wanazifanya kwenye mgodi huo ni kwa njia za Kienyeji, ikiwamo uchomaji wa madini, na kuiomba Serikali iwapatie elimu ya kutosha ili kuokoa Afya zao.

"Wachimbaji wadogo hawana elimu ya kujikinga na Kemikali ya Zebaki, kwanza haipatikani virahisi sababu inauzwa kama Bangi, lakini mimi nikihitaji inapatikana, na wachimbaji wengi wameshazoea kuitumia hivyo hivyo bila hata ya kuvaa vifaa kinga, sababu madhara yake siyo virahisi kutokea haraka," alisema Andrew.

Mbunge wa Jimbo la Kahama Jumanne Kishimba, ambaye ni mjumbe wa Kamati hiyo, alitoa ushauri kwa Serikali watafute dawa za kumeza kama pipi, ili mchimbaji akisikia kupatapata madhara ya Zebaki ana kwenda dukani ana nunua na kutafuna kama pipi na kuokoa afya yake.

Aidha Serikali imeanza kutafuta mbadala wa matumizi ya kemikali ya Zebaki kukamatia dhahabu kwa wachimbaji wadogo, ambapo hadi ifikapo mwaka 2025 matumizi ya Kemikali hiyo yawe yameshapungua kabisa, sababu inaelezwa hadi kufikia mwaka 2030 Zebaki haitakuwepo tena.


Mwenyekiti wa Kamati ya Mbunge, Viwanda, Biashara na Mazingira David Kihenzile, akizungumza na wachimbaji wa madini ya dhahabu Mwime Manispaa ya Kahama.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Seleman Jafo, akuzungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Mwime Manispaa ya Kahama.
Mbunge wa Jimbo la Kahama Jumanne Kishimba ,akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Mwime.

Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu, Mkoa wa kimadini Kahama Joseph Andrew, akizungumza kwenye ziara ya Kamati hiyo ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira.

Wachimbaji wadogo wa ,Madini ya dhahabu Mwime Manispaa ya Kahama wakiwa kwenye mkutano.

Wachimbaji wadogo wa ,Madini ya dhahabu Mwime Manispaa ya Kahama wakiwa kwenye mkutano.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge , Viwanda, Biashara na Mazingira, wakiwa kwenye Mgodi wa Mwime.

Wajumbe wa Kamati ya Bunge , Viwanda, Biashara na Mazingira, wakiangalia shughuli za usagaji mawe ya dhahabu katika Mgodi wa Mwime.

Wajumbe wa Kamati ya Bunge , Viwanda, Biashara na Mazingira, wakiangalia shughuli za uoshaji udongo wa madini ambao umesha sangwa na Makarasha.

Wajumbe wa Kamati ya Bunge , Viwanda, Biashara na Mazingira, wakiangalia shughuli za ukamatiji madini ya dhahabu kwa kutumia Kemikali ya Zebaki.

Muonekano wa Kemikali ya Zebaki ikiwa ndani ya Kalai, ambalo hutumika kukamatia Madini ya dhahabu.

Awali wajumbe hao wakiangalia shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu, na usalama wake.

Wajumbe wa Kamati ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira, wakiangalia Mawe ya dhahabu ambayo yametolewa ndani ya Shimo.

Akina mama wakiendelea na shughuli za upongaji mawe ambayo yana madini ya dhahabu.

Awali wajumbe wa kamati ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira, wakiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Seleman Jafo, katika Mgodi huo wa Mwime wakifanya ziara ya kukagua shughuli za utunzaji mazingira kwenye mgodi wa Mwime pamoja na matumizi ya kemikali ya Zebaki.
 
Picha zote na  Marco Maduhu, KAHAMA

































































Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464