MABINTI 84,000 WALIO KWENYE UMRI BALEHE WAFIKIWA NA ELIMU YA AFYA YA UZAZI KUJIKINGA NA MAGONJWA YA ZINAA

Miongoni mwa mabinti 30 waliowezeshwa kupata elimu ya afya na ujuzi katika Chuo cha St. Francis Vocation Training Center (SFS VTC) kilichopo kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga.

Damian Masyenene
WASICHANA wadogo na akina mama wenye umri kati ya miaka 17 hadi 24 ambao wamekuwa kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa ikiwemo Virusi Vya Ukimwi (VVU) wamewezeshwa elimu ya afya ya uzazi ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na ngono zembe inayohatarisha maisha yao.

Elimu hiyo iliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la FHI360 kupitia katika mradi wa Epic imewafikia mabinti 84,000 kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi na kuondokana na ngono zembe na udhibiti wa janga la VVU/Ukimwi hapa nchini.

Akizungumza na mabinti 30 wanaoendelea kupata ujuzi katika Chuo cha St. Francis Vocation Training Center (SFS VTC) kilichopo kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoa wa Shinyanga, Ofisa mabinti balehe na akinamama vijana kutoka shirika hilo Agnes Junga alisema hadi sasa wamewafikia mabinti balehe na akinamama vijana 84,000 na kuwapatia ujuzi mbalimbali na tabia hatarishi, kati ya hao vijana 56,000 wamewezeshwa kiuchumi ambapo kati yao 13,000 wameshaanzisha biashara zao na kuendesha maisha.

Mratibu wa Mafunzo hayo Charles Maganga amelipongeza shirika la FHI 360 kwa kuona umuhimu wa kuthamini watoto wa kike na kuwapeleka chuoni kupata mafunzo ambayo yatawasaidia katika maisha yao ya baadae.

Alisema kwa ujuezi wanaowapatia mabinti hao watakuwa na uwezo wa kufanyakazi popote iwe kwenye sekta binafsi au serikali kupitia fani ya Umeme, Uchomeleaji na ufundi magari, udereva, Kompyuta, ufundi cherehani, saluni na mapambo.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo Ester Obadia alisema walichaguliwa kujiunga na masomo katika chuo hicho kupitia vikundi vya wasichana vinavyosimamiwa na Shirika la FHI 360 na wanatarajia kutumia mafunzo hayo kwaajili ya kujiari na kujiingizia vipato.

Nae Mary Edward alisema walikuwa wakiishi katika mazingira magumu na kusababisha kuingia kwenye tabia hatarishi lakini kwa mafunzo hayo yatawasaidia kujitegemea na kujiepusha kujiingiza kwenye vishawishi vinavyoweza kuwaingiza kwenye mazingira hatarishi ya ngono.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la KIWOHEDE Justa Mwaituka alisema kupitia mradi wao wa miaka mitatu wa kusomesha wasichana wamekuwa wakisaidia kuwezesha Wanawake na Wasichana Balehe ili kufikia usawa wa kijinsia.

Mdau wa masuala ya ukatili wa kijinsia na VVU kutoka AGPAHI, Dk. Jane Kashumba alishauri wazazi kufanya ufuatiliaji wa watoto wao hasa mabinti wanapokuwa kwenye umri wa kubalehe ili wawape elimu sahihi na kuwasaidia kuvuka salama kuliko kuwatelekeza na kugutuka pale watoto wanapoingia kwenye vishawishi na kuleta matatizo ambayo yanaleta athari kwa mtoto.

Dk. Kashumba alisema jamii inapaswa kurudi kwenye tamaduni zao za malezi na makuzi na kujenga mahusiano mazuri na watoto, kwani kwa sasa wazazi na walezi wengi wanafikiri mtoto akishafika sekondari basi anajitegemea.

“Tuache usasa usio na maana ambao unawaharibu na kuwapotosha ubongo watoto, watoto wanaachwa huru zaidi na kulelewa na wafanyakazi wa nyumbani ambao huwafundisha mambo yasiyo sahihi, kwahiyo tusiache Watoto wajilee wenyewe tutawaweka kwenye hatari za maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo Virusi Vya Ukimwi (VVU),” alishauri.

Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima bungeni Aprili, 2020 idadi ya watu wanaopima afya zao ili kutambua hali zao za maambukizi ya VVU imekuwa ikiongezeka kila mwaka kutoka jumla ya watu 6,800,000 mwaka 2015 hadi kufikia 12,392,268 Desemba 2019, sawa na ongezeko la asilimia 82.2.

Aidha, vituo vya kutolea huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU vimeongezeka kutoka vituo 5,600 mwaka 2015 hadi vituo 6,397 Desemba 2019. Vilevile, vituo vya kutolea huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU vimeongezeka kutoka vituo 5,600 mwaka 2015 hadi vituo 6,397 Desemba 2019.

 "Ongezeko hili limetokana na mikakati iliyowekwa na Wizara ya kuhakikisha watu wengi zaidi hasa wanaume wanajitokeza kupima VVU, kutambua hali zao na kupata huduma stahiki," ilisema taarifa hiyo.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464