ASKOFU SANGU AWAASA VIJANA KUTOKUBALI KUTUMIKA KUVURUGA AMANI YA NCHI


Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanawake wakatoliki Tanzania WAWATA Jimbo la Shinyanga, na kushoto kwake ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko.

Na Samir Salum-SHINYANGA

ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamau Liberatus Sangu amewaasa vijana hapa nchini kutokubali kutumiwa kuvuruga amani ya nchi, na badala yake watumie nguvu walizonazo kuujenga ufalme wa Mungu.

Askofu Sangu ametoa rai hiyo leo wakati akiongoza Misa takatifu ya kufunga mwaka wa Kanisa iliyofanyika katika kanisa kuu la Mama mwenye Huruma Ngokolo mjini Sinyanga ambayo imekwenda pamoja na kufunga kongamano la kijimbo la Vijana Wakatoliki wafanyakazi VIWAWA.

Amesema mara nyingi vijana wamekuwa wakitumiwa kufanikisha mipango ambayo imekuwa ikihatarisha hali ya amani katika mataifa mbalimbali jambo ambalo wanapaswa kulikataa na badala yake watumie nguvu na karama walizonazo katika kuujenga ufalme wa Mungu.

“Mara nyingi vijana wanatumiwa vibaya na watu ambao hawana nia njema kwa sababu wana nguvu sasa wanaweza kutumia nguvu zao vibaya,niwasihi vijana tumieni nguvu zenu katika kujenga ufalme wa mungu kwa kuwa chimbuko la haki,amani,upendo na umoja mahali kote duniani” Askofu Sangu

askofu Sangu amewataka Watanzania kutochoka kumwomba Mungu ili aendelee kuimarisha misingi ya haki,amani,upendo na mshikamano hatua ambayo itasaidia kuliepusha taifa na hali ya migogoro na umwagaji damu ambao unatokea katika mataifa mengine kwa sababu tu ya ubinafsi wa watu wachache.

Kwa upande mwingine Askofu Sangu amewapongeza Wanawake Wakatoliki Tanzania WAWATA jimbo la Shinyanga kwa namna ambavyo wamejitoa katika kulilea shirika jipya la watawa la kijimbo la Mtakatifu Bikra Maria Mama mwenye Huruma ambalo limeanzishwa miaka michache iliyopita.

amesema WAWATA wamefanya kazi kubwa katika kulilea na kulitunza shirika hilo hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto zilizopo.

“Nichukue Nafasi hii kuwashukuru sana WAWATA wamekuwa mstari wa mbele sana katika mwaka wote huu na miaka iliyopita katika kulitiunza na kulilea shirika letu la Bikira Maria Mama wa Huruma” Amesema Askofu Sangu

Wakati huohuo askofu Sangu amewaongoza waamini kusali kuliombea taifa ili lipate mvua za kutosha kutokana na hali ya hewa kwa mwaka huu kutokuwa ya kuridhisha ikiwa ni mwendelezo wa kuunga mkono wito wa rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA SULUHU HASAN alioutoa kwa viongozi wa dini hivi karibuni jijini Mwanza.

Kupitia misa ya leo ambapo pia kanisa linaadhimisha Jumapili ya Kristo Mfalme,askofu Sangu pamoja na mambo mengine amewabatiza watoto wadogo wapatao 88.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu akitoa sakramenti ya ubatizo leo katika kanisa kuu la mama mwenye Huruma Ngokolo.
Baadhi ya waamini wakiwa katika ibada ya misa takatifu ya kufunga mwaka wa kanisa iliyofanyika leo katika kanisa la Kuu la mama mwenye huruma Parokia ya Ngokolo Jimbo katoliki Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko,(kulia) akiwa Kanisani.
Askofu wa kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, akipiga picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko.
Askofu wa kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu katika Picha ya pamoja na baadhi ya Vijana walioshiriki kongamano la vijana wakatoliki wafanyakazi VIWAWA, Pamoja na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko.































Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464