DIWANI WA CHAMAGUHA ALIYEKUWA MWENYEKITI WA MTAA APETA UMEYA SHINYANGA , AKIMBWAGA GULAMHAFEEZ ALIYEWAHI KUSHIKA KITI HICHO MIAKA 10


Picha ya Diwani wa Chamaguha Elias Masumbuko, ambaye amepitishwa na Madiwani kuwa Meya wa Manispaa ya Shinyanga.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MADIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Shinyanga, wamempitisha Elias Masumbuko kuwania kiti cha Umeya Manispaa ya Shinyanga, kuziba nafasi ya aliyekuwa Meya wa Manispaa hiyo David Nkulila ambaye alifariki Agosti mwaka huu kwa matatizo ya Moyo.
Masumbuko ni Diwani wa Chamaguha Manispaa ya Shinyanga, ambapo kabla ya kushinda udiwani kwenye uchaguzi Mkuu mwaka jana, alikuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Sanjo kwenye Kata hiyo zaidi ya miaka 15, akichuana na Gulamhafeez Mukadam ambaye alishashika nafasi hiyo ya Umeya ndani ya miaka 10.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Agnes Bashem, alisema uchaguzi huo wa kupitisha jina la Meya wa Manispaa ya Shinyanga, kuziba nafasi ya Marehemu Nkulila umefanyika katika Ofisi za CCM wilaya.

Alisema wajumbe waliopiga kura ni 24 kati ya 25, ambapo Elias Masumbuko ambaye ni diwani wa Chamaguha ameshinda kwa kura 14, dhidi ya Gulamhafeez Mukadam diwani wa Mjini ambaye amepata kura 10, na alishawahi kushika nafasi hiyo ya Umeya.

“Mara baada ya uchaguzi huu wa kura za maoni kumpata Meya wa Manispaa ya Shinyanga kupitia Chama Cha Mapinduzi, Jina la Elias Masumbuko litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, kisha madiwani watampigia kura za Ndiyo au Hapana",alisema Bashemu.

Uchaguzi huo wa Kura za maoni wa kupitisha jina la Meya Manispaa ya Shinyanga, umefanyika baada ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, iliyokutana katika kikao maalum Novemba mwaka huu Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma, na kuwateua Gulamhafeez Mukadam na Elias Masumbuko kugombea kiti cha Umeya Manispaa hiyo.

Aidha Mwaka 2020 David Nkulila alichaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Shinyanga baada ya vikao vya juu vya CCM kurudisha jina lake na kuondoa jina la Gulamhafeez Mukadam.

David Mathew Nkulila alichaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Novemba 24 Mwaka jana, na alitumikia nafasi ya Meya kwa kipindi cha miezi 10 hadi umauti ulipomkuta usiku wa kuamkia Agosti 23,2021 wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kutokana na kuugua maradhi ya Moyo.


Picha ya aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Shinyanga Miaka 10, Gulmhafeez Mkudam, ambaye ameshindwa nafasi ya Umeya na Elias Masumbuko katika uchaguzi wa kupiga kura uliofanywa leo na Madiwani wa CCM Manispaa ya Shinyanga.








Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464