HALMASHAURI YA SHINYANGA YAKUSANYA MIL. 406 ,MBUNGE AHMED SALUM APONGEZA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Nice Munissy akitoa taarifa ya hali ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwezi Oktoba, 2021 na upelekaji wa fedha za miradi ya maendeleo ya robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwenye kikao  cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 406,135,290.2 sawa na asilimia 212.4 ya maksio ya mwezi wa mapato ya ndani na kufikisha jumla ya shilingi 1,450,545,616.64 sawa na asilimia 63 ya maksio ya shilingi 2,294,068,499.80 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Novemba 12,2021 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Nice Munissy wakati wa Kikao cha Kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo Iselamagazi kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo.

Akitoa taarifa ya hali ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwezi Oktoba, 2021 na upelekaji wa fedha za miradi ya maendeleo ya robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Munissy ameeleza kuwa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kila mwezi inakadiria kukusanya kiasi cha shilingi 191,172,374.98 na kwa kipindi cha mwezi Oktoba 2021 wamefanikiwa kukusanya shilingi Milioni 406.

“Mwezi Oktoba, 2021 Halmashauri imekusanya kiasi cha shilingi 406,135,290.2 sawa na asilimia 212.4 ya maksio ya mwezi wa mapato ya ndani na kufikisha jumla ya shilingi 1,450,545,616.64 sawa na asilimia 63 ya maksio ya shilingi 2,294,068,499.80 kwa mwaka wa fedha 2021/2022”,amesema Munissy.

Aidha amesema katika kipindi cha mwezi Oktoba 2021, halmashauri ya wilaya ya Shinyanga imepokea kiasi cha shilingi 2,692,494,351.32 fedha kutoka serikali kuu, kati ya fedha hizo mishahara ni shilingi 1,738,583,050.00, fedha ya maendeleo ni shilingi 1,917,123,693.80 na matumizi mengineyo ni shilingi 601,836,353.32.

“Katika Mapato ya mwezi Oktoba 2021, halmashauri ya wilaya ya Shinyanga imetenga kiasi cha shilingi 39,914,278 ikiwa ni asilimia 10 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu”,amesema.

Katika hatua nyingine ameeleza kuwa katika soko la madini ya Mwakitolyo jumla ya mauzo kwa mwezi Oktoba ni gramu 14,159.40 zenye thamani ya shilingi 1,490,816,984.68 na ada ya huduma ni shilingi 4,472,450.96 na kwamba halmashauri hiyo imekusanya shilingi 247,202,500.00 katika Machimbo ya dhahabu ya Nyandolwa kwa kipindi cha mwezi Oktoba 2021.

Hata hivyo, Munissy amesema Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga katika kipindi cha mwezi Julai hadi Oktoba 2021 kupitia mapato yake ya ndani imepeleka jumla ya shilingi 480,211,574.20 katika miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, elimu, mifugo na kilimo.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja Miradi ya ukamilishwaji wa zahanati,ukamilishaji wa nyumba ya watumishi katika zahanati,ukamilishaji wa madarasa katika shule za sekondari na msingi, ukamilishaji wa skimu za umwagiliaji,ukamilishaji wa vyoo katika shule za sekondari na msingi na ulipaji fidia eneo la ujenzi wa maegesho ya malori Tinde.

Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa uzio mnada wa Tinde, ujenzi wa choo mnada wa Lyabukande, ujenzi wa machinjio ya Mwakitolyo na Nyandolwa na ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi/Madini eneo la uchimbaji la Nyandolwa, ukamilishaji wa nyumba za walimu na ukamilishaji wa ofisi ya utawala katika shule za sekondari.

Mkurugenzi huyo pia amesema Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga imepokea jumla ya shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 65 vya madarasa kupitia fedha za ‘ Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO -19’.

“Mpaka sasa ujenzi upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na matarajio ni kukamilisha vyumba vyote 65 vya madarasa kabla au ifikapo Novemba 30,2021”,amesema Munissy.

Mkurugenzi huyo ametumia fursa hiyo kuwashukuru Madiwani na Wakuu wa Idara kwa ushirikiano wanaoendelea nao katika kuhakikisha wanatekeleza mipango mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Solwa Mhe. Ahmed Salum amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nice Munissy kwa jinsi anavyojitahidi kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ya wilaya hiyo.


"Kutokana na mapato haya mazuri tunayoendelea nayo kupitia usimamizi mzuri wa Mkurugenzi wetu kijana  Nice Munissy pamoja na ushirikiano mzuri kutoka kwa madiwani mambo yanaenda vizuri kwenye halmashauri yetu..Hivi sasa tuna machimbo mapya ya dhahabu ya Nyandolwa na huenda tukawa na Nyondolwa B, mapato yataongezeka maradufu hivyo naamini kabisa jimbo hili la Solwa linaenda kuwa Washington",amesema Ahmed.


"Mhe. Mwenyekiti tumepata mkurugenzi Mpya, damu yake bado ni changa, mimi kama mbunge niwaombe sana waheshimiwa madiwani tumpe ushirikiano mzuri mkurugenzi wetu, ameonesha nia njema ya kufanya kazi katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. Wakuu wa Idara tuendelee kumpa ushirikiano ili afanye kazi yake kwa ufanisi, mimi binafsi ninampa ushirikiano, hata nyinyi wakuu wa Idara mnapohitaji ushirikiano pia msisite kunitafuta, mimi na madiwani tunaendelea kushirikiana", ameongeza Ahmed.


Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngasa Mboje amesema halmashauri ya wilaya ya Shinyanga inaendelea vizuri huku akizishukuru taasisi mbalimbali zinazoshirikiana na halmashauri katika utatuzi wa changamoto mbalimbali.

"Kama alivyokwisha kusema Mkurugenzi wa Halmashauri na Mbunge wa Jimbo la Solwa, halmashauri inakwenda vizuri kwa sababu tunao uwezo wa kusukuma maendeleo, Mama yetu Mhe. Samia Suluhu ametupatia shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, tunakwenda kwa kasi, wengi wamefikia hatua flani, kuna madarasa yaliyofungwa Renta kwa hiyo ile Deadline tunakwenda nayo kwa kasi. Sisi viongozi tuna wajibu wa kusimamia fedha hizi ili tuweze kutimiza lengo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan",amesema Mboje.

"Lakini sisi kama halmashauri kulingana na mapato ya halmashauri yetu, asilimia 40 yetu hatujabaki nyuma,mnaona taarifa zetu za mapato na matumizi, tumetenga fedha kila mwezi kwa ajili ya kusukuma maendeleo hata kwenye maboma, tunataka kuondoa changamoto zilizopo katika sekta ya afya na elimu..Tunazishukuru sana taasisi zinazoshirikiana na serikali katika kutatua changamoto,kama Mkurugenzi atahitaji msaada basi taasisi hizo naomba zimpe ushirikiano",ameongeza

Ngasa pia amesema kutokana na kwamba Mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga yanategemea madini ya dhahabu ipo haja ya halmashauri hiyo kubadilisha nembo ya halmashauri kwa kutoa nembo ya almasi na kuweka dhahabu huku akimuomba Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kufanyia kazi jambo hilo kwa kubadilisha nembo.


Akitoa salamu kwenye kikao hicho, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa wa Shinyanga (Serikali za Mitaa), Baraka Bulongo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha kwa ajili ya miradi ya Maendeleo huku akitaka Madiwani na watendaji kuanzia ngazi ya vijiji kusimamia kikamilifu fedha hizo.


“Tunamshukuru Mhe. Rais Samia kutuletea fedha za miradi ya maendeleo. Naomba tuwe na usimamizi wa karibu kwa kushirikiana, tukishirikisha maafisa watendaji wa vijiji na kata ili miradi ifanyike vizuri na kumalizika kwa wakati”,amesema Bulongo.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngasa Mboje akizungumza kwenye wa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kilichofanyika leo Ijumaa Novemba 12,2021 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo Iselamagazi. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngasa Mboje akizungumza kwenye wa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kilichofanyika leo Ijumaa Novemba 12,2021 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo Iselamagazi. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Nice Munissy. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Solwa Mhe. Ahmed Salum akifuatiwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambaye ni Diwani wa Kata ya Iselamagazi Mhe. Isack Sengelema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngasa Mboje akiongoza kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Isack Sengelema
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Nice Munissy akizungumza kwenye kikao cha Kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo Iselamagazi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Nice Munissy akizungumza kwenye kikao cha Kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Solwa Mhe. Ahmed Salum akifuatiwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Isack Sengelema na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngasa Mboje
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngasa Mboje akiandika dondoo muhimu wakati Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Nice Munissy akizungumza kwenye kikao cha Kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Solwa Mhe. Ahmed Salum akifuatiwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Isack Sengelema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Nice Munissy akitoa taarifa ya hali ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwezi Oktoba, 2021 na upelekaji wa fedha za miradi ya maendeleo ya robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mbunge wa Jimbo la Solwa Mhe. Ahmed Salum akizungumza kwenye kikao cha Kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Isack Sengelema,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngasa Mboje (katikati) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Nice Munissy (kulia) wakifurahia jambo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Isack Sengelema akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa wa Shinyanga (Serikali za mitaa), Baraka Bulongo akitoa salamu kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela akitoa salamu katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga
Wageni waalikwa na watendaji wa halmashauri wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Wageni waalikwa na watendaji wa halmashauri wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464