RC MJEMA AZUNGUMZA NA WATUMISHI HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA, MWENYEKITI HALMASHAURI ATISHIA KUJIUZULU


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amezungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na kuwataka wafanye kazi kwa mshikamano, kuheshimiana pamoja na kujali mipaka yao.

Mjema amezungumza na watumishi wa Halmashauri hiyo leo, akiwa ameambatana na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, viongozi mbalimbali wa Serikali, pamoja na chama cha mapinduzi CCM.

Akizungumza na watumishi hao, alisema Halmashauri ambayo haina maelewano, kamwe haiwezi kusonga mbele kimaendeleo sababu watakosa muunganiko ambapo kila mtu atakuwa anafanya kazi kivyake, na hata kama akiagizwa na kiongozi wake haiwezi kufanya kazi kwa ufanisi.

“Kipindi nakuja Shinyanga, niliambiwa kabisa kuna Halmashauri zitakusumbua, hivyo naombeni mbadilike, na mkiendelea kutoelewana Halmashauri hii inaweza kufutwa kabisa,”alisema Mjema.

Katika hatua nyingine Mhe; Mjema akizungumzia Sakata la Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje, pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyi Nice Munissy la kumtuhumu kutomheshimu na kufikia hatua ya kutoelewana, alitaka mgogoro huo uishe kwa kukaa pande zote mbili na kumaliza tofauti zao.

“Katika nafasi za uongozi ngazi ya Halmashauri, Mwenyekiti wa Halmashauri ndiyo msimamizi mkuu wa Halmashauri, na Mkurugenzi yeye ni misimamizi wa maendeleo, hivyo Mkurugenzi asipokuwa na maelewano na Mwenyekiti ambaye ndiye ana madiwani kamwe hamuwezi kusonga mbele kimaendeleo,” alisema Mjema.

Aidha, alisema baada ya kikao hicho kuisha, anatarajia kutosikia tena malumbano kwenye Halmashauri hiyo, bali kila mmoja ajali mipaka yake ya kazi, na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kusukuma gurudumu la maendeleo.

Awali Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ngassa Mboje, akizungumza kwenye kikao hicho, alitishia kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti kwa madai kwa madai ya kutoheshimiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Nice Munissy.

Alisema kwenye Halmashauri hiyo tangu aingie Mkurugenzi huyo mpya hakuna tena kuheshimiana wala maelewano mazuri, na hivyo kuona ni bora aachie ngazi ya uenyekiti ili abaki kuwatumia wananchi wake wa Kata ya Mwalukwa.

"Tangu 2011 nipo kwenye Halmashauri hii, na Wakurugenzi wote waliopita walikuwa wakini heshimu, lakini sasa hivi hakuna heshima, ni bora nikachukua maamuzi ya kuachia ngazi ya uenyekiti nibaki na udiwani wangu kutumikia wananchi," alisema Mboje.

" Kwenye Halmashauri hii naona kuna changamoto kubwa ina kuja kutokea, watumishi hawazumguzi tu kuna shida kubwa sana," aliongeza.

Aidha, katika ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa wakati wa kutembelea miradi ya maendeleo, Mwenyekiti huyo alikuwa akilalamika kuwa amenyimwa gari na Mkurugenzi, sababu ya kutomheshimu, na hivyo kulazimika kupanda kwenye gari la chama.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Nice Munissy, akizungumzia suala la Magari, alisema Halmashauri hiyo ina Magari 24, lakini Magari Sita ndiyo yanafanyakazi, na yaliyosalia yote ni Mabovu.


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza kwenye kikao hicho cha watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje, akizungunza kwenye kikao hicho cha watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nice Munissy akisoma taarifa ya Halmashauri hiyo.

Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa Sophia Mjema.

Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa Sophia Mjema.

Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa Sophia Mjema.

Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa Sophia Mjema.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA.








Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464