MIAKA 60 YA UHURU NA MAFANIKIO AFYA YA UZAZI NA UZAZI WA MPANGO, WADAU WAFUNGUKA

   Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Dorothy Gwajima


Na Damian Masyenene
DESEMBA 9 mwaka huu Tanzania Bara imesherehekea miaka 60 ya uhuru huku wizara mbalimbali zikionyesha mafanikio katika sekta na idara zilizomo ndani ya wizara hiyo kuonyesha hatua zilizopigwa tangu mwaka 1961 Tanganyika ilipopata uhuru wake

Akibainisha mafanikio ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Novemba 8 mwaka huu katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Waziri Dk. Dorothy Gwajima alieleza kuwa miaka 60 baada ya uhuru idadi ya Kliniki za afya ya uzazi imeongezeka na sera ni kuwa katika kila kituo cha huduma za afya kuwe na huduma za afya ya uzazi na mtoto.

Alisema taasisi ya chakula na lishe (TFNC) kwa kushirikiana na sekta nyingine imesaidia kupunguza upungufu wa damu kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa (miaka 15-49) kutoka asilimia zaidi ya 50 hadi kufikia asilimia 28 mwaka 2018 huku ikihamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa watoto wenye umri chini ya miezi sita kutoka asilimia 24 hadi kutikia asilimia 59 mwaka 2018.

Akitaja mafanikio kwenye huduma za afya ya uzazi alisema asilimia 93.4 ya wajawazito walihudhuria kliniki mahudhurio manne au zaidi hadi kufikia Machi, 2021 huku kukiwa na ongezeko la asilimia 83.1 kwa akinamama kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mwaka 2020 ambayo ni zaidi ya lengo la Mpango Mkakati wa Nne wa Sekta ya Afya (HSSP IV) la asilimia 65.

Pia idadi ya akinamama waliojifungua na kurudi kiliniki siku mbili baada ya kujifungua imefikia asilimia 62 ambapo mwitikio huo ni muhimu katika uhakikisha usalama wa mama na mtoto, kwa kuwa asilimia 60 ya vifo vitokanavyo na uzazi hutokea kipindi cha baada ya kujifungua kutokana na matatizo ya kupoteza damu, kifafa cha mimba na maambukizi ya bakteria.

“Vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 94 kwa vizazi hai 1000 mwaka 1992 hadi vifo 36 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2020 na vifo vya watoto wachanga ndani ya siku 28 (neonatal mortality) vimepungua kutoka vifo 32 kwa kila vizazi hai 1000 (2004/05) hadi vifo 20 kwa kila vizazi 1000 (2020),” alisema Dk. Dorothy.

Vile vile, vifo vya wajawazito vimepungua kutoka vifo 870 kwa kila vizazi 100,000 (1990) kufikia vifo 321 kwa kila vizazi hai 100,000 (2020) ambapo mafanikio hayo yanajieleza kwa kuongezeka kwa umri wa kuishi wa Mtanzania kutoka miaka 36 mwaka 1961 hadi miaka 66 mwaka 2020 ambayo inaashiria kuimarika kwa mifumo ya utoaji huduma za afya nchini.

Baadhi ya wadau wa sekta ya afya wakizungumzia mafanikio hayo walipongeza serikali kwa kuboresha huduma za afya nchini kwa kuongeza vituo vya afya, elimu kwa umma, uimarishaji wa chanjo, afya ya uzazi hususan kwa vijana wa rika balehe na uzazi wa mpango kwa wananchi ili kupunguza changamoto ya mimba zisizopangwa na watoto wa mitaani wasio na malezi bora.

Mratibu wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (SPC) Estomine Henry alishauri kuwa ni vyema serikali ikaendelea kuimarisha elimu na huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa wananchi ambao wamekuwa wakihadaiwa na uzushi na elimu potofu kuhusu huduma hizo na wengine kujikuta wakizichukia na kuzihusisha na dhana potofu ikiwemo maradhi kwa akina mama.

Meneja Miradi Shirika la Thubutu Africa Intiatives (TAI) Paschalia Mbugani alisema kuna mwitikio chanya juu ya afya ya uzazi mkoani Shinyanga kupitia elimu wanayoitoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali huku wananchi wakiwa na kiu ya kufahamu na kueleza kiundani changamoto za uzazi wa mpango na umuhimu wake na namna upuuziaji unavyoleta madhara.

“Mfano kuna kesi moja tulikutana nayo wilayani Shinyanga mama wa miaka 52 alipata ujauzito wakati alishafunga kuzaa ni baada ya kutumia njia za asili za mafundo kiunoni ule ujauzito ulikuwa ni aibu ikabidi afichwe nab inti zake, lakini kupitia hii elimu tunayotoa watu wengi wanabadilika na kuamini njia za kisasa ambazo ni salama,” alisema Paschalia.

Mmoja wa wanawake wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango mkazi wa Ndala mjini Shinyanga (jina linahifadhiwa) alisema marafiki wamekuwa na ushawishi mkubwa kwa kueneza minong’ono isiyofaa kuhusu matumizi ya njia hizo na kuleta hofu kwa wengine ambao wamejikuta wakiacha kutumia huku akiomba elimu sahihi kutolewa kwenye kliniki za wazazi.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464