REA YATAMBULISHA WAKANDARASI NA KUKABIDHI MIKATABA YA MRADI WA KUSAMBAZA UMEME VIJIJI 216 SHINYANGA

Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Elineema Mkumbo (kushoto) akimkabidhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary Mikataba itakayotumiwa na Wakandarasi kutekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotarajia kunufaisha vijiji 216 mkoani Shinyanga kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 60.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wakala wa Nishati Vijijini (Rural Energy Agency – REA) umetambulisha kwa uongozi wa Mkoa wa Shinyanga Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili na kukabidhi Mikataba itakayotumiwa na Wakandarasi Kutekeleza Mradi huo unaotarajia kunufaisha vijiji 216 kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 60.


Akizungumza leo Jumatano Desemba 1,2021 wakati wa kukabidhi Mikataba hiyo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary , Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Elineema Mkumbo amewataja Wakandarasi watakaosimamia mradi wa usambazaji umeme wilayani Kahama, Shinyanga na Kishapu kuwa ni Suma JKT na Tontan Project Technology Co. Ltd.


Mhandisi Mkumbo amesema kutokana na maelekezo ya Serikali ni lazima vijiji vyote vinatakiwa kupatiwa huduma ya umeme ifikapo Mwezi Desemba mwaka 2022.


“Kwa niaba ya Bodi ya Nishati Vijijini, Menejimenti pamoja na Wafanyakazi wa REA tunakukabidhi Mikataba ya kupeleka umeme kwa uongozi wa Mkoa wa Shinyanga ili uendelee kutusaidia katika usimamizi wa mradi wa kupeleka umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili katika mkoa wa Shinyanga. Kufuatia maelekezo ya Serikali ni lazima vijiji vyote vinapata umeme ifikapo Mwezi Desemba mwaka 2022”,amesema Mhandisi Mkumbo.


“Mradi huu tumeugawa katika mafungu mawili ili kuharakisha utekelezaji wake. Fungu la kwanza linaenda Wilaya ya Kahama ambapo gharama ya mradi ni shilingi Bilioni 39. Fungu la pili ni kwa ajili ya wilaya ya Kishapu na halmashauri ya Shinyanga ambapo gharama yake ni zaidi ya Bilioni 21. Hivyo kwa mkoa wa Shinyanga tuna zaidi ya Bilioni 60 ili kukamilisha upelekaji wa umeme katika vijiji”,ameongeza Mhandisi Mkumbo.


Amebainisha kuwa huwa kuna changamoto zinajitokeza wakati Wakandarasi wanapofika ‘Site’ kwa hiyo wameona wafanye maandalizi ya mapema kuziwahi hizo changamoto kabla hazijafika mbali hivyo wamekutana REA, TANESCO na Wakandarasi ili wajue changamoto ni zipi huku wakizingatia vipaumbele vya serikali.


“Pia ilikuwa ni lazima tuwatambulishe Wakandarasi wetu kwenye Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga. Kwa hiyo tuna Kampuni ya Tontan Project Technology Co. Ltd ambayo itatekeleza mradi katika wilaya ya Kahama na SUMA JKT ambao watakuwa wilaya ya Kishapu na Shinyanga Vijijini”,amesema.


Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary ameelekeza kwamba Mkandarasi anapokwenda eneo lolote la mradi TANESCO lazima wawepo, uongozi wa eneo husika uwepo ili uweze kuainisha sehemu za kipaumbele na kuhakikisha REA inafuatilia.


“Wananchi wanasubiri sana huduma ya umeme kwa sababu umeme ni muhimu kwa maendeleo ya jamii kwani kila kila kazi inayofanyika inahitaji nishati ya umeme. Tunaamini kabisa kwamba umeme ukifika hata kasi ya maendeleo itakuwa kubwa. Serikali inasubiri umeme na tupo tayari kutoa ushirikiano utakaohitajika wakati Wakandarasi wakiwa ‘Site’ ,cha muhimu ni Mkandarasi awe mwepesi kutoa changamoto ambazo zitakazokuwepo kwenye maeneo ya mradi”,amesema Omary.


“Mara nyingi miradi ya umeme inapopita kunakuwa na changamoto ya mradi unapoelekea siyo kwenye mahitaji makubwa na ya lazima ya jamii, nendeni mkazichukue hizo changamoto na mzifanyie kazi,isitokee mradi unapelekwa maeneo ya mbali sana na kuacha vijiji vikubwa vyenye uhitaji mkubwa wa umeme, tuanze na hao wenye athari kubwa za kijamii na kimaendeleo”,amesema.

Amebainisha ili mradi huo ukamilike kwa wakati ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anatimiza wajibu wake ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu changamoto zinazojitokeza.


“Nina hakika kabisa kila mmoja, Mkandarasi, TANESCO, REA, Serikali ya mkoa wote tunataka kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa wakati. Kinachotakiwa ni kila mmoja atimize wajibu wake,kila mmoja awe na wajibu wa kutoa taarifa kwa mwingine iwapo anahitaji msaada ‘Support’ wa changamoto anayokutana nayo”, amesema Mhe. Omary


Msimamizi wa Miradi ya REA - TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Anthony Tarimo amesema mradi huo unatarajia kunufaisha vijiji 216 vya Mkoa wa Shinyanga na sasa wapo kwenye hatua za awali za utekelezaji wa mradi huu ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kuingiza kwenye mradi vijiji 30 vilivyokuwa vimesalia kupatiwa umeme kwenye mipango iliyopita kwani serikali ilishatoa maagizo vipatiwe umeme kupitia Mradi huu mpya.


Naye Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Ukandarasi ya Tontan Project Technology Co. Ltd, Nasra Mwampashe ambao ni Wakandarasi wa Mradi huo wa REA wilaya ya Kahama wenye thamani ya shilingi Bilioni 39 ameahidi kuwa watatekeleza mradi huo kwa ufanisi na weledi mkubwa na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa.


“Tukiwa Wakandarasi tunaishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuamini na kutupatia huu mradi. Tunaahidi kufanya kazi kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu kwa sababu uwezo tunao, nguvu tunayo, vifaa tunavyo na tumejipanga vilivyo kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda tuliopangiwa”,amesema Mwampashe.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Elineema Mkumbo (kushoto) akimkabidhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary Mikataba itakayotumiwa na Wakandarasi kutekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotarajia kunufaisha vijiji 216 mkoani Shinyanga. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Elineema Mkumbo (kushoto) akimkabidhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary Mikataba itakayotumiwa na Wakandarasi kutekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotarajia kunufaisha vijiji 216 mkoani Shinyanga.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary akionesha Mikataba itakayotumiwa na Wakandarasi kutekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotarajia kunufaisha vijiji 216 mkoani Shinyanga kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 60.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary akizungumza wakati Wakala wa Nishati Vijijini (Rural Energy Agency – REA) ukitambulisha kwa uongozi wa Mkoa wa Shinyanga Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili na kukabidhi Mikataba itakayotumiwa na Wakandarasi Kutekeleza Mradi huo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary akizungumza wakati Wakala wa Nishati Vijijini (Rural Energy Agency – REA) ukitambulisha kwa uongozi wa Mkoa wa Shinyanga Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili na kukabidhi Mikataba itakayotumiwa na Wakandarasi Kutekeleza Mradi huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Elineema Mkumbo akizungumza wakati akitambulisha kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili na kukabidhi Mikataba itakayotumiwa na Wakandarasi Kutekeleza Mradi huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Elineema Mkumbo akizungumza wakati akitambulisha kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili na kukabidhi Mikataba itakayotumiwa na Wakandarasi Kutekeleza Mradi huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Elineema Mkumbo (katikati) akizungumza wakati akitambulisha kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili na kukabidhi Mikataba itakayotumiwa na Wakandarasi Kutekeleza Mradi huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Elineema Mkumbo akielezea namna walivyojipanga kutekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili  mkoani Shinyanga.
Msimamizi wa Miradi ya REA - TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Anthony Tarimo akielezea namna vijiji 216 mkoani Shinyanga vitakavyonufaika na Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili.
Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Ukandarasi ya Tontan Project Technology Co. Ltd, Nasra Mwampashe akielezea namna walivyojipanga kutekeleza kwa ufanisi na weledi mkubwa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili wilayani Kahama.

 Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464