SHULE YA WATU WENYE ULEMAVU-BUHANGIJA,YAKABILIWA NA UHABA WA WAALIMU

 

 Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu mkoa wa Shinyanga(SHIVYAWATA) Richard Mpongo akizungumza na mwandishi wa habari hii.


 Picha ya watoto  wenye mahitaji maalum shule jumuishi-Buhangija.


Watoto wenye mahitaji maalum kutoka Shule jumuishi -Buhangija -Manispaa ya Shinyanga.
 

 Suzy Butondo,Shinyanga

Wanafunzi viziwi wanaosoma shule jumuishi ya Buhangija iliyoko manispaa ya Shinyanga mkoani hapa wanakabiliwa na uhaba wa walimu, watumishi wasio walimu ikiwa ni pamoja na kutokuwa na uzio, ambao utasaidia watoto hao wasiwe wanatoroka shuleni hapo.

Hayo ameyasema Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu mkoa wa Shinyanga Richard Mpongo wakati akizungumza na Mwananchi jana ofisini kwake, alisema  serikali imesema watoto wote wenye ulemavu wa aina yeyote waende shule na kweli wameenda, lakini kuna changamoto ya kutokuwa na walimu wa kutosha na wafanyakazi wa shule hiyo.


Mpongo amesema walimu wakiajiliwa wa kutosha katika shule hiyo wanafunzi wanapata elimu bora, hivyo ni vizuri serikali iliangalie suala hilo na iwajengee uzio ili wasitoroke toroke na kusababisha kupotea hapo shuleni, kwani Wameshawahi kutoroka watoto wawili na walihangaika kuwatafuta, ambapo walipatikana wakiwa wilaya ya Shinyanga wakitafuta kurudi nyumbani walikotoka.

Pia Mpongo ameishukuru serikali kwa kuanzisha sensa  ya kuwatambua watoto wenye ulemavu, hivyo watoto wengi watakuwa shuleni lakini walimu wenye utaalamu wako watano tu na wanahitajika walimu tisa ili wawe 14 ili watoto hao waweze kufundishwa vizuri na kuweza kuelewa.


"Sasa hivi watoto wenye ulemavu viziwi wapo 84 katika shule hiyo hawafundishwi ipasavyo kwa sababu ya upungufu wa walimu wapo shuleni hapo wanakuwa  tu si kwa ajili ya kupata elimu, ni vizuri serikali ikaliona hili ikaajili walimu wenye utaamu na wapelekwe kwenye shule zenye watoto viziwi  "amesema Mpongo.


Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Buhangija Pactanied Mwita na Kabla Martin wamesema wanaishukuru serikali kwa kuwaletea vifaa mbalimbali vya kujifunzia tofati na awali Sasa hivi hawana changamoto kubwa Ila wanaomba iwapelekee walimu ili waweze kupata elimu bora.


Mwalimu wa lugha ya viziwi katika shule ya Buhangija ambayo ni shule mchanganyiko Royce Daudi amesema katika shule hiyo kuna jumla ya wanafunzi viziwi 84 , darasa la awali wanafunzi 12  darasa la kwanza wapo 18, darasa  la pili 12, darasa la tatu 16, darasa la nne 8, darasa la tano 5, na darasa  la sita wapo 6,.


Royce amesema katika shule hiyo pia haina madawati ya kutosha kwa ajili ya kukaa watu wenye ulemavu wanaupungufu wa magodoro, hawana mashuka ya kutosha, hivyo ameiomba serikali iliangalie suala hilo ili watoto hao waweze kupata elimu bora na si bora elimu tu.

Aidha mwalimu mkuu wa shule hiyo Fatuma jilala aliishukuru serikali na wadau mbalimbali kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zikiwemo za miundombinu na mazingira kuwa rafiki kwa walemavu.

Kwa upande wake afisa elimu maalumu manispaa ya Shinyanga Edward Mdagati alisema kweli shule ya Buhangija inaupungufu wa walimu wa wanafunzi  wenye ulemavu viziwi, hivyo serikali inaendelea na mchakato wa kuweza kuajili walimu wenye taaluma hiyo.

"Kweli walimu ni wachache hivyo serikali imejipanga kila zinapotoka ajira hatukosi mwalimu mmoja wa taaluma ya watu wenye ulemavu na walimu wanapoenda chuo tumekuwa tukiwahamasisha waende wakasomee taaluma ya kufundishwa watu wenye ulemavu, hata hivyo Kuna Baadhi ya walimu wakiajiliwa katika shule za kawaida tunafanya mpango ili wahamishiwe kwenye shule zetu maalumu"amesema Mdagati.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464