Waziri wa Madini, Dkt.Doto Biteko Desemba akizungumza na wachimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la machimbo la
Nyamalimbe Makarashani lililopo Wilaya ya Geita mkoani Geita.
Wachimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la machimbo la Nyamalimbe Makarashani lililopo Wilaya ya Geita mkoani Geita.
Waziri wa Madini,Dkt.Doto Biteko akipokea maelezo ya hali ya usalama wa wachimbaji dhahabu katika eneo la machimbo la
Nyamalimbe Makarashani yaliyopo Wilaya ya Geita mkoani Geita.
Na mwandishi wetu.
WACHIMBAJI wa madini wametakiwa kuzingatia uchimbaji salama katika
maeneo ya migodi yao ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji madini kwa
tija na migodi iendelee kubaki salama.
Hayo yameelezwa na Waziri
wa Madini, Dkt.Doto Biteko lDesemba 29, 2021 alipokutana na kuzungumza
na wachimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la machimbo la Nyamalimbe
Makarashani lililopo Wilaya ya Geita mkoani Geita.
Aidha,
Dkt.Biteko amewaagiza wakaguzi wa mgodi katika machimbo hayo kuhakikisha
wanaweka utaratibu wa daftari kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu kwa
kusainisha majina ya wachimbaji wanaoingia na kutoka katika machimbo
hayo.
“Wasimamizi wote mnaosimamia hapa, hakikisheni watu
wanaoingia kwenye duara kabla hajaingia kwenye duara kuna daftari juu,
limeandikwa anatoka wapi na umri wake, anapozama na kutoka anasaini
tena,”amesema Dkt.Biteko.
Kuhusu umuhimu wa kulipa kodi,
Dkt.Biteko amesisitiza kila gramu ya dhahabu inayopatikana ipelekwe
kwenye masoko ya madini ili Serikali ikusanye kodi.
Aidha,
amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Geita, Daniel Mapunda kutafuta wanunuzi
wa madini ya dhahabu (Brokers) ili wasaidie kupunguza changamoto za
wachimbaji kwenda umbali mrefu hadi Katoro kwa ajili ya kwenda kuuza
dhahabu zao.
Kuhusu changamoto walizonazo hususani ya nishati ya
umeme katika eneo hilo la machimbo, Dkt.Biteko amewahakikishia kwamba
suala hilo limefanyiwa kazi kwa ushirikiano na Wizara ya Nishati ambao
watafika kwa ajili ya kuwapatia umeme.
Aidha, Dkt.Biteko ameagiza
mialo yote iliyopo katika maeneo ya maduara ya shughuli za uchimbaji
madini yaondolewe ili zihamishiwe kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa kwa
ajili ya kuweka mialo hiyo.
Akizungumzia kuhusu kulinda afya za
wachimbaji, Dkt.Biteko amesisitiza wachimbaji wa Nyamalimbe kuhakikisha
wanalinda afya zao kutokana na maradhi mbalimbali.
Amesema,
sehemu zenye shughuli za uchimbaji wa madini zina neema, lakini pia zina
changamoto endapo mchimbaji hatazingatia taratibu za afya.
Naye,
Jumanne Amani akisoma risala kwa niaba ya wachimbaji wa Nyamalinde
amesema, uwepo wa mgodi katika eneo hilo umeboresha maisha ya wakazi
katika maeneo yanayozunguka mgodi huo na maeneo mengine ya watu
wanaofika kujipatia kipato pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara.
Ameongeza
kuwa, wachimbaji wa mgodi wa mlipuko wa dhahabu wa Nyamalimbe wanaomba
kupatiwa huduma ya umeme katika eneo la mgodi ili kupunguza gharama za
uendeshaji kwa wachimbaji na kuongeza tija.