UKATILI WA KIJINSIA MITANDAONI WAPINGWA

 

 Mwanasheria kutoka Taasisi ya Wildaf Zakia Msangi akizungumza na wanafunzi wa Taasisi ya Uuguzi na Ukunga Mkoani Njombe (NJIHAS) katika mdahalo katika Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia unaofanyika katika Vyuo mbalimbali nchi

 

Mmoja wa wanafunzi kutoka Taasisi ya Uuguzi na Ukunga Mkoani Njombe (NJIHAS) Alpha Edwin akichangia katika mdahalo katika Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia unaofanyika katika Vyuo mbalimbali nchini.

Na Witness Masalu,Njombe

 

Imebainika kwamba kumekua na tatizo kubwa la watu kufanyiwa ukatili  mitandaoni hasa wanawake hivyo kusababisha matatizo ya Kisaikolojia kwa wahanga wa vitendo hivyo.

 

Hayo yamebainishwa kwenye msafara wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia katika Siku 16 za Kupinga Ukatili unaojumuisha Maafisa kutoka Wizara, Taasisi na Wadau mbalimbali wa kupinga ukatili wa kijinsia unaoendelea katika Vyuo mbalimbali nchini 

 

Akizungumza na wanafunzi wa Taasisi ya Uuguzi na Ukunga Mkoani Njombe (NJIHAS) Mwanasheria kutokea Taasisi ya Wildaf Zakia Msangi amesema kumekua na unyanyasaji wa kiwango cha juu hasa katika karne hii ya kidijitali ambapo watu wengi wana simu janja na wanaweza kutuma na kupakua picha za aina mbalimbali. 

 

Bi Zakia aliongeza kuwa jamii inatakiwa ibadilike  na iwe makini na simu janja zao wanazozitumia na kuhakikisha zinatumika katika mambo yenye manufaa na tija na kuwaasa watakaotumia kinyume na hapo na kuwa sio sawa kwani husababisha madhara kwa wengine.

 

"Tumekuwa tukisikia na kuona picha na video katika mitandao ikidhalilisha watu hasa wanawake na Watoto hivyo tuchukue tahadhari kwani  ukishtakiwa kwa kosa hilo hukumu yake ni miaka mitatu au faini ya milioni tano ama vyote kwa pamoja" alisema Bi. Zakia

 

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Christopher Mushi amesema kuwa Serikali inasimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ili kuhakikisha vitendo vya ukatili vinatokomezwa.

 

Ameongeza kuwa katika kutilia mkazo hilo hivi karibuni umezinduliwa mpango wa Uratibu na Uanzishwaji wa Madawati ya Jinsia katika Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu nchini yatakayosaidia kupata taarifa za vitendo hivyo vinavyotokea maneno hayo ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi ya wanaobainika kufanya vitendo hivyo.

 

kwa upande wake Mmoja wa wanafunzi kutoka Taasisi ya Uuguzi na Ukunga Mkoani Njombe (NJIHAS) ,Alpha Edwin amesema sababu inayochochea ukatili wa kijinsia kuendelea hasa kwa wanawake ni wao wenyewe kushindwa kuijua thamani yao na kuweka vitu ambavyo vinachochea wao kudhalilishwa  mitandaoni.

 

"Lakini pia madhara ya ukatili wa kijinsia mitandaoni tunayaona ikiwemo kutengwa na Jamii, kukosa fursa muhimu na hata wengine kuamua kuchukua uhai wao" alisema Alpha

 

Naye Anna Masha aliwaasa wanafunzi wenzake kuachana na makundi ambayo hayafai wakiwa vyuoni ila kuzingatia masomo kwani makundi hayo mengi yamekuwa chanzo cha kufanyiwa au kutokea kwa vitendo vya ukatili hasa udhalilishaji mtandaoni.

 

MWISHO.

 

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464