Naibu Katibu mkuu Tanzania Bara kutoka Chama Cha ACT-Wazalendo Jorani Bashange.
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimesisitiza kuwapo kwa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi, pamoja na mabadiliko ya vifungu vya sheria vya vyama vya siasa, ili kuwe na uhuru wa demokrasia hapa nchini.
Naibu Katibu mkuu Tanzania Bara kutoka Chama Cha ACT-Wazalendo Jorani Bashange, amebainisha hayo jana mkoani Shinyanga, alipofanya ziara ya kikazi kwa ajili ya kuimarisha chama, na kutoa maagizo kwa viongozi kusajili wanachama upya kwa mfumo wa dijitali.
Alisema kuwapo kwa Tume huru ya uchaguzi, na mabadiliko ya vifungu vya sheria ya vyama vya siasa, kutasaidia ukuaji wa uhuru wa demokrasia hapa nchini, ambapo vyama vitakuwa vikifanya shughuli zao za kisiasa bila ya kuingiliwa na vyombo vyovyote, pamoja na uchaguzi kufanyika bila ya kukibeba chama chochote.
“Ninapo zungumzia Tume huru na maanisha kwamba, iwe na mfumo wake wa kijitegemea na waajiriwa wake yenyewe kuanzia ngazi zote, siyo siku ya uchaguzi inafika ndipo wanaanza kukodiwa Walimu, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, ambapo wote hawa ni waajiriwa wa Serikali, hivyo hakutakuwa na haki kwenye huo uchaguzi,”alisema Bashange.
“Mfano unakata Rufaa kwenye Tume ya uchaguzi, anaye kwenda kusikiliza Rufaa hiyo ni Katibu Tawala sasa hapo kutakuwa na haki kweli, yani kesi ya Nyani una mpelekea Tumbili, tunataka Tume iwe na mfumo wake yenyewe kuanzia juu mpaka chini ili kusiwe na muungiliano,”aliongeza.
Akizungumzia vifungu vya sheria ya vyama vya siasa, alisema vifanyiwe mabadiliko, ambapo kila kifungu kwenye sheria hiyo kina adhabu na ukienda kinyume tu ni jinai, jambo ambalo amesema lina wanyima uhuru wa kufanya siasa, pamoja na Jeshi la Polisi kuingilia shughuli zao na hata kuzuia mikutano.
Aidha, alisema mambo yote hayo yakifanyiwa kazi, milango ya demokrasia itafunguka hapa nchini na hakutakuwa tena na ukandamizwaji, ambapo na vyama vitafanya siasa kwa uhuru bila ya kuingiliwa na chombo chochote likiwamo Jeshi la Polisi.
Katika hatua nyingine, alisema wana matumaini na Rais Samia Suluhu Hassani katika kuleta mabadiliko ya uhuru wa demokrasia, ambapo mara baada ya kikao cha vyama vya siasa mwaka jana, sasa hivi mabadiliko yameanza kuonekana, ambapo hawazuiwi tena kufanya mikutano, wala kutoingiliwa na Jeshi la Polisi kama zamani, na hata barabarani hawasumbuliwi na magari yao pamoja na kupigiwa salute.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Shinyanga Siri Yasini, alisema kwa sasa wameanza kujiimarisha na kuongeza idadi ya wanachama wapya, na kusajili wanachama wao upya kwa mfumo wa dijitali, pamoja na kuanzisha ACT Kampuni kwa ajili ya kuwezesha wanachama wao kiuchumi, na chama kuendelea kuwa imara.
Pia, alisema Chama hicho mkoani Shinyanga Kamwe hakiwezi kususia uchaguzi wowote, licha kufanyiwa figisu kwenye chaguzi zilizopita ukiwamo uchaguzi mdogo wa Udiwani Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, ambapo Mgombea wao alitolewa dakika za mwisho, licha ya kutagazwa kuwa atagombea nafasi hiyo.
Alisema katika uchaguzi mwingine mdogo ambao utafanyika hivi karibuni katika Kata ya Mwamalili Manispaa ya Shinyanga, mara baada ya aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo Paul Machela kufariki Januari Mwaka huu, kuwa wamejipanga vyema kushiriki kwenye uchaguzi huo, na watahakikisha wanapata ushindi wa kishindo.Baadhi ya wanachama wa ACT-Wazalendo wakiwa kwenye kikao.
Baadhi ya wanachama wa ACT-Wazalendo wakiwa kwenye kikao.
Na Marco Maduhu, SHINYANGA