Mwakilishi wa asasi ya Marafiki Nancy Foundation, Ezra Manjerenga akimjulia hali mmoja ya akina mama waliojifungulia katika kituo cha afya Bugisi kilichopo katika wilaya ya Shinyanga.
Na Damian Masyenene - Shinyanga
Ubora, unafuu wa huduma za afya na motisha kwa akina mama wajawazito zinazotolewa katika kituo cha afya Bugisi kilichopo Chembeli kata ya Didia wilaya ya Shiyanga umefanya idadi ya akina mama wanaojifungulia kituoni hapo kuongezeka kila mwezi na kuzidi kuwavutia wanawake kwenda kupata huduma.
Kwa msaada wa asasi ya Marafiki Nancy Foundation kituo hicho kimekuwa kikitoa huduma za virutubisho muhimu kwa mama na mtoto wakati wa ujauzito, huduma ya kioo (Utra Sound) kuangalia maendeleo ya ujauzito na kutambua matatizo yanayohusiana na ujauzito pamoja na kutoa motisha ya Khanga kwa akina mama wanaojifungua ili kuwahamasisha kujifungulia katika kituo hicho ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mama, Baba na Mtoto katika Kituo cha Afya Bugisi, Dk. William Zakayo alisema kuna mwitikio mzuri kwa akina mama kufika kituoni hapo kupata huduma za afya ambapo kabla ya kuanza huduma hizo mwaka 2017 walikuwa wanapokea akina mama 30 hadi 35 kwa mwezi lakini sasa kuna ongezeko kubwa hadi kufikia akina mama 60 hadi 85 kwa mwezi mmoja..
Alisema akina mama wajawazito waliokuwa wanapokea akina mama 50 hadi 60 kwa mwezi lakini sasa wanapokea kuanzia 70 hadi 80 wakati mwingine 100 kwa mwezi mmoja kutokana na huduma bora na za bure ikiwemo Utra Sound na Khanga zinazotolewa katika kituo cha afya Bugisi.
“Wadau hawa (Nancy Foundation) wametusaidia kuleta chachu na hamasa kwa akina mama wanaofika kupata huduma za afya, sasa tunambulika kwa huduma zetu tunapokea wateja wengi kutoka maeneo ya vijijini wanaokuja kuanza huduma na kujifungua hapa,” alisema Dk. Zakayo.
“Kutokana na virutubisho muhimu kwa mama na mtoto wakati wa ujauzito vinavyotolewa na wadau mbalimbali akina mama wajawazito wanaohudumiwa hapa hawapati changamoto ya upungufu wa damu na wanapatiwa huduma bora za afya,” alisema.
Baadhi ya akina mama akiwemo Esther Salu, Sophia Jisinza na Thereza Lutonja walisema huduma za afya ya mama na mtoto wanazopata kituoni hapo zimekuwa msaada kwao kuwanusuru na changamoto za uzazi ambapo waliishukuru asasi hiyo kwa huduma bora wanazotoa kwa akina mama, watoto na wagonjwa wengine na kuahidi kuhamasisha wenzao kujifungulia kwenye vituo vya afya ili kuokoa uhai wa mama na mtoto.
Afisa Mtendaji wa kata ya Didia, Jackson Maganga alitoa wito kwa wadau kuendelea kukisaidia kituo hicho kwani kimeleta manufaa makubwa ikiwemo kupunguza idadi ya akina mama wanaojifungulia nyumbani huku akiwaomba akina mama wanufaika wa huduma za Nancy Foundation kuwa mabalozi na kuhamasisha akina mama kujifungulia kwenye vituo vya afya.
Mmoja wa wadau wa afya ya uzazi, Dk. Justice Minofu kutoka Shirika la Doctors With Africa aliwashauri akina mama kuachana na tabia ya kujifungulia nyumbani kwani inahatarisha maisha ya mama na mtoto akisisitiza kuwa huduma bora za afya zinapatikana hospitali pekee.
Akizungumzia namna wanavyoshiriki kusaidia kuboresha huduma za mama na mtoto hasa kwa wanawake waishio maeneo ya vijijini, Mwakilishi wa asasi ya Marafiki Nancy Foundation nchini Tanzania, Ezra Manjerenga alisema wanashiriki kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto katika kituo hicho tangu mwaka 2017 ili kuongeza idadi ya akina mama wanaofika kituo cha afya kupata huduma za afya na kuachana na tabia ya kujifungulia nyumbani hali ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.
“Hili ni wazo lililotokana na uwepo wa changamoto za uzazi kwahiyo marafiki wakaamua kutumia changamoto alizopitia mtoto huyo na kuanzisha huduma za kujitolea kwa ajili ya kuchangia huduma ya mama na mtoto katika kituo cha afya Bugisi kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga,” alisema Manjerenga.
Msimamizi wa Kituo cha Afya Bugisi, Sister Kathleen Costigan alisema msaada unaotolewa na asasi hiyo ni msaada mkubwa kwa akina mama walio mbali na huduma za hospitali huku akitumia fursa hiyo kuwahamasisha wanawake kufika kituoni hapo kwani wanatoa huduma bora za afya.