MIGODI YA BARRICK NCHINI TANZANIA MBIONI KUFIKIA DARAJA LA KWANZA LA UZALISHAJI


Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow (kushoto) akiwaeleza Waziri wa Madini,Dk. Doto Biteko, Waziri wa Tamisemi, Innocent Bashungwa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema (wa nne kushoto) jinsi mtambo wa kielekitroniki wa uchumbaji madini chini ardhi unavyofanya kazi wakati wa kutangaza uzalishaji wa dhahabu kufikia wakia 500,000 kwa migodi North Mara na Bulyanhulu mwishoni wa mwaka 2021.
Wataalamu wa uchimbaji madini wa Mgodi wa Bulyanhulu wakionyesha jinsi mtambo wa kielekitroniki wa uchimbaji unavyofanya kazi.
Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mgodi wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga juzi wakati wa kutangaza uzalishaji wa dhahabu kufikia wakia 500,000 kwa migodi North Mara na Bulyanhulu mwishoni wa mwaka 2021. (Kushoto) ni Waziri wa Madini Dk. Doto Biteko na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema.
Waziri wa Madini, Dk.Doto Biteko akizungumza waandi wa habari alipotembelea mgodi wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga jana wakati wa Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Britow (katikati) akitangaza uzalishaji wa dhahabu kufikia wakia 500,000 kwa migodi North Mara na Bulyanhulu mwishoni wa mwaka 2021. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa shinyanga, Sophia Mjema.
Waziri wa Madini,Dk.Doto Biteko na ujumbe wake wakitembezwa katika maeneo ya mgodi wa Bulyanhulu

****
Kampuni ya Barrick Gold Corporation (NYSE:GOLD) (TSX: ABX) – Migodi ya North Mara na Bulyanhulu, iliyokuwa imesimamisha uzalishaji wakati Barrick ilipoichukua na kuwa chini ya usimamizi wake miaka miwili iliyopita, imeweza kufikisha uzalishaji wa zaidi ya wakia 500,000 za dhahabu kufikia mwishoni mwa mwaka 2021, hivyo kufikia vigezo vya uzalishaji vya daraja la juu (Tier one)

Mafanikio haya yamefikiwa wakati migodi yote miwili ikiendelea kuwa na hadhi ya ubora wa kimataifa ISO 45001 katika uzingatiaji usalama na ISO 14001 katika utunzaji mazingira. Kama ilivyo migodi mingine inayoendeshwa na Barrick.

Kwa upande wa North Mara, mgodi uko mbioni kuwa kwenye mfumo wa uzalishaji uliounganishwa kikamilifu kufuatia mpango wa uchimbaji dhahabu katika mashimo ya Nyabirama katika kipindi hiki cha robo mwaka na Nyabigena katika kipindi cha tatu cha robo mwaka wa 2022.Hatua hii inatarajiwa kuuongezea rasilimali mgodi huo na kuuwezesha kuwa na mfumo wa uendeshaji wa shughuli zake unaokidhi mahitaji yake.

Mgodi wa Bulyanhulu nao kwa sasa umeimarishwa upya na kuwa mgodi wenye hadhi ya kimataifa, unaoendeshwa kwa gharama ya chini. Aidha, hatua yake ya kuanzisha uchimbaji wa chini ya ardhi (underground mining) umeuongezea mgodi huo muda mrefu zaidi wa kuendelea na uzalishaji tangu Desemba 2021.

Migodi yote miwili inatarajiwa kuripoti ukuaji mkubwa wa raslimali zake katika kipindi cha mwaka 2021.

Barrick inaendelea kujiimarisha katika maeneo ya Bulyanhulu kutokana na kupata leseni sita za kutafiti madini katika maeneo yanayopakana na mgodi huo. Timu ya wataalamu wa jiolojia na utafiti wa kampuni hiyo inaendelea kutafuta fursa katika sehemu nyinginezo nchini Tanzania

Akizungumza na vyombo vya habari vya hapa nchini hapa leo, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick Mark Bristow, alisema utendaji mzuri wa migodi hiyo umetokana na kuzingatia miongozo ya kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19 na utoaji wa chanjo kwa wafanyakazi wake, asilimia 26.45% kati yao tayari wamechanjwa na 20.25% wamepata chanjo kamili ya UVIKO-19 . Alisema, Barrick inafanya kazi kwa karibu na mamlaka za afya nchini na katika siku za usoni inatarajia kutoa msaada wa mashine nne za kupima Covid -19 (PCR) kwa hospitali zinazozunguka maeneo ya migodi.

Migodi pia iliendelea kuajiri na kuwapatia ujuzi Watanzania. Asilimia 97% ya wafanyakazi ni watanzania , huku 41% wakitoka katika vijiji vinavyoizunguka. Pia imeimarisha ushirikiano na wazabuni wa ndani. Tangu Barrick ilipoingia tena Tanzania mwaka 2019, imetumia Zaidi ya dola bilioni 1.8 katika kodi, mishahara na malipo kwa wafanyabiashara wa ndani. Pia imewekeza dola milioni 6.7 katika miradi ya elimu katika jamii, afya na miundombinu.

Akirejelea Ripoti ya Haki za Binadamu ya Barrick iliyochapishwa hivi karibuni, Bristow alisema masuala ya mazingira na mengine ambayo kampuni hiyo iliyarithi kutoka kwa waendeshaji wa awali wa migodi hiyo, yanaendelea kutatuliwa au yametatuliwa kabisa.

Maendeleo makubwa ya kampuni katika suala hili yalidhihirishwa mwezi uliopita, pale ambapo timu ya Barrick ilitumia ufundi na ubunifu wa hali ya juu kuhakikisha kwamba bwawa la kuhifadhi mabaki ya taka zitokanazo na mchakato wa uzalishaji dhahabu unahifadhi maji yanayoendana na muundo wake wa awali katika mgodi wa North Mara”, Bristow alisema. Utendaji wa bwawa hilo unasaidiwa na mtambo mpya na wa kisasa wa kutakatisha maji.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464