RAIS SAMIA AKAZIA NCHI KUENDELEA KUKOPA, AGUSIA UTEUZI WA MAWAZIRI- PRESHA INAPANDA PRESHA INASHUKA


RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema lazima nchi iendelee kukopa, kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwamo ujenzi wa vyumba vya madarasa, kwa kuwa fedha za tozo haziwezi kutosheleza mahitaji ya miradi hiyo.

Samia amebainisha hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.

Amesema kuna mahitaji wa madarasa mengi katika sekta ya elimu, ambayo kwa kutegemea fedha ya tozo itachukua muda mrefu kukamilisha mahitaji hayo.

"Lakini ndugu zangu tulichopata hapa leo zaidi ya fedha hizi za Uviko-19, kuna fedha ya tozo ambayo na yenyewe ilipoanza ilipigiwa kelele eee, tukasema ngoja tupunguze tukapunguza, baada ya kupunguza kelele zimeshuka” amesema Rais Samia.

“Lakini wapigaji kelele hao wa sasa hivi waliuliza kuna fedha ya tozo kwa nini tunakwenda kukopa” ameongeza

Aidha amesema mpaka sasa fedha zilizopatikana kwenye tozo zimejenga madarasa 5,00 lakini uhitaji wake ni zaidi ya madarasa 10,000 kwa shule za msingi pekee.

"Takwimu zilizotolewa na Mawaziri hapa zinatosheleza kwamba pamoja na kwamba tuna fedha za tozo mahitaji ya madarasa shule za msingi ni 10,000 mpaka sasa hivi, tumeweza madarasa 5,00 kwa fedha za tozo, tunafika lini? Amehoji Rais Samia na kusisitiza “Lazima tukope tuweke miundombinu”.

Amesema kuna uhitaji mkubwa wa madarasa kwa siku zijazo ambapo mwaka huu tuna watoto Laki Tisa na mwakani itakuwa zaidi ya milimo moja, hivyo kutegemea fedha ya tozo itachelewesha kufikia malengo kwa wakati

“Tuna madarasa mbele yanahitajika, tunayajenga kwa fedha za tozo kweli?, ambayo mpaka sasa imetusaidia madarasa 5,00, hatuwezi kwenda na fedha ya tozo”

"Kwa hiyo inashangaza kuona mtu mwenye uelewa anasema kuna fedha ya tozo lakini kaenda kukopa ya nini au kwa nini tunaendelea kutoza tozo wakati fedha ya mkopo ipo” amesisitiza


Katika hatua nyingine Rais Samia ameleza kushangazwa na kauli za Spika wa Bunge Job Ndugai kusimama hadharani na kukosoa mkopo wa Shilingi Trilioni 1.3 kutoka shirika la Fedha Duniani (IMF) wenye lengo la kuchochea mapambano dhidi ya UVIKO -19 wakati taarifa mbalimbali zinapitia kwenye bunge lake.

Amesema kinachosumbua sasa ni homa ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

"Tuna serikali ya kukopa kopa tangu uhuru ,Tumekopa kopa na maendeleo tuliyopata yanatokana na kukopa kopa..kukopa siyo kioja. Tutakopa mikopo isiyo na riba ili tupate maendeleo". amesema Rais Samia.

"Mtu na akili yake anasimama na anahoji kuhusu mikopo na tozo, sio lolote ni homa ya 2025, kwa mtu ambaye nilimtegemea kushirikiana naye kwenye maendeleo, sikutegemea kama angesimama na kusema maneno hayo. Huwezi kufikiria mtu mliyemuamini, mshika mhimili, aende akasimame aseme yale. “Ni stress ya 2025", amesisitiza Rais Samia.

"Kinachotokea sasa ni 2025 Fever, wasameheni...Haya ninayofanya sasa sifanyi kwa ajili ya mwaka 2025, nafanya kwa ajili ya maendeleo ya nchi...Tunachotazama sasa ni maendeleo kwa watanzania... Kelele za wanaopiga kelele hazinisumbui..mimi sivunjiki moyo, mimi nina moyo wangu, moyo wangu siyo wa glasi,ni wa nyama ulioumbwa na Mungu, hivyo sivunjiki moyo...Nishikeni mkono twende sote.

"Nilipopewa mamlaka haya kuna mtu alikuja na kunipa pole na hongera akasema mtu atakayekusumbua kwenye kazi hii ni mtu mwenye shati la kijani mwenzako siyo wa upinzani na hili wanalotazama sasa ni la 2025.na ndicho nachokiona ameongeza” rais Samia.


"Wakati mmenikabidhi huu mzigo, nilianza kusikia lugha zinasema serikali ya mpito, serikali ya mpito bungeni huko kwa kina Kassim. Nikarudi kwenye Katiba kuangalia serikali ya mpito imeandikwa wapi...sikuona. Nikasema 'anhaa, twendeni"- Rais Samia

Pia amesema hivi karibuni atatoa Listi mpya ya Mawaziri na kuondoa wale ambao anaona hawaendani na kasi yake, bali wampishe. 
 
"Hivi karibuni nitatangaza mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri kwa wale ambao nitaona wanafaa kuendana nami kuwaletea maendeleo watanzania, nitaendana nao, na kwa wale ambao Ndoto zao ni 2025 nitawaweka kando ili wapate muda zaidi na kujiaandaa ili tukutane nao huko 2025." amesema Rais Samia.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464