Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga,Bw.Hussein Mussa akitoa taarifa ya robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 kwa vyombo vya Habari Mkoa wa Shinyanga.
Na mwandishi wetu,
Miradi sitini (60) ya ujenzi wa madarasa yenye thamani ya Shs billion 4 mkoani Shinyanga imetekelezwa kikamilifu baada ya ofisi ya Takukuru Mkoa wa Shinyanga kuzuia mianya ya rushwa katika hatua zote za utekelezaji wa miradi hiyo.
Hayo yameelezwa leo Januari 25,2022 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Bw. Hussein Mussa alipokuwa akifanya mkutano na waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga katika kuwasilisha taarifa ya robo ya pili ya mwaka 2021/2022 katika kipindi cha Oktoba hadi desemba -2021.
Mkuu wa Takukuru alieleza kuwa Ofisi yake ilifatilia miradi sitini (60) ya ujenzi wa madarasa uliotokana na fedha za Mpango wa Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya Uviko-19 kwa kipindi cha oktoba hadi desemba-2021.
“Mapungufu yalibainika katika ukaguzi wa miradi hii ambavyo yangeweza kusababisha mianya ya rushwa yamefanyiwa kazi kwa kufanya vikao na wadau ambao ni wasimamizi na watekelezaji wa miradi husika pamoja na kutoa elimu kwa lengo la kuomba mianya ya rushwa” Alisema Hussein Mussa.
Kwa upande mwingine, ofisi ya Takukuru kupitia dawati la uchunguzi ilipokea malalamiko 42 kwa kipindi cha robo ya pili, oktoba -desemba cha mwaka wa fedha ya mwaka 2021/2022 ambapo taarifa zinazohusu rushwa zilikuwa ni 20 na zisizohusu rushwa zilikuwa ni 22.
Pia ofisi ya Takukuru Mkoa wa Shinyanga ilieleza hali ya kesi zinazoendelea mahakamani ni 23 ambapo kati ya hizo, kesi mpya ni mbili (2) ambazo zilifunguliwa katika kipindi cha oktoba-desemba,2021
“Kwa mujibu wa taarifa 42 tulizopokea, idara zilizolalamikiwa ni serikali ya mitaa(16),ardhi(9),biashara(6),elimu(2),maji(2),uhamiaji(2),polisi(2),madini(1),vyama vya ushirika(1) na sekta binfasi(1)”. Alisema Hussein
Aidha ,Ofisi ya Takukuru Mkoa wa Shinyanga ilifanikiwa kutoa elimu kwa umma dhidi ya mapambano dhidi ya rushwa kwa vijana wa skauti 200 wa wilaya ya Kahama kupitia kampeni maalum ya TAKUSKA ambapo ni TAKUKURU na SKAUTI wameungana ili kutoa elimu kwa vijana wa skauti na kuwajengea katika msingi ya kuwa na uadilifu, uzalendo na uwajibikaji kwa Taifa lao.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464