HALMASHAURI WILAYA YA SHINYANGA YAWAFUKUZA WATUMISHI SITA


Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngasa Mboje akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Februari 23,2022. Picha na Kadama Malunde
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Nice Munissy akizungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika leo Jumatano Februari 23,2022.

 

Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakiwa katika kikao.
 
Na Kadama Malunde - Shinyanga

Baraza la Madiwani Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga limewafukuza kazi Watumishi Sita kutokana na makosa mbalimbali ya kiutumishi.

Uamuzi huo umetangazwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngasa Mboje wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Februari 23,2022.

Mboje amesema Baraza la Madiwani limewafukuza watumishi hao baada ya kupitia utetezi wao na baadhi yao hawajaonekana kutokana na kutokuwepo kwenye maeneo yao ya kazi.

“Baraza la Madiwani limewafukuza kazi watumishi sita wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kutoka Idara ya Afya watumishi wawili wamefukuzwa kazi na kutoka Idara ya Utawala waliofukuzwa kazi ni wanne”,amesema Mboje.

Mbali na watumishi hao sita kufukuzwa kazi, pia watumishi wengine wawili Baraza hilo limeagiza wakatwe asilimia 15 ya mishahara yao na watafanya hivyo kwa muda wa miaka mitatu.

Watumishi Idara ya Afya waliofukuzwa kazi ni Daktari Fidelis Benedict Mushi wa Kituo cha afya Nindo na Andrew Israel Mwakisambwe ambaye ni Mteknolojia Maabara Kituo cha Afya Salawe.

Watumishi wanne kutoka Idara ya Utawala waliofukuzwa kazi ni Maafisa Watendaji wa Vijiji ambao Charles Dominick Mayunga (Bukene), Mercy Gasper Kyando (Kilimawe), Omary Hamis Omary (Igembya) na Robert Surika Mbuti (Mwabagehu).

CHANZO - MALUNDE 1 BLOG

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464