Na Damian Masyenene, Shinyanga
WIKI iliyopita kuliibuka mijadala mbalimbali baada ya ripoti ya kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya UKIMWI kubainisha ongezeko la matumizi ya vidonge vya kuzuia mimba miongoni mwa wasichana wenye umri kati ya miaka 10 - 24 huku ikitajwa kuwa vidonge hivyo ambavyo huuzwa kwa bei ya chini huchochea maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU).
Akiwasilisha taarifa ya kipindi cha Januari, 2021 hadi Februari, 2022 bungeni Februari 10, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu Bunge ya Masuala ya UKIMWI, Fatma Hassan Toufiq alisema baadhi ya wasichana wanaogopa zaidi mimba kuliko maambukizi ya VVU hivyo kutumia vidonge vya P2 kama njia mbadala ya kuzuia mimba na kuacha kutumia kondomu ambazo zingewakinga dhidi ya maambukizi hayo, magonjwa ya ngono na mimba zisizotarajiwa.
Kamati hiyo ilishauri kuwa ili kukabiliana na hali hiyo dawa za kuzuia mimba (P2) ziuzwe pamoja na kondomu kwa lazima kuwawezesha wasichana kuwa na tabia ya kutumia kondomu hizo bila ya kunyanyapaliwa huku uzoefu ukionesha iwapo watakuwa na hizo kondomu basi wasichana wengi watazitumia ili kupunguza maudhi na madhara ya dawa za kuzuia mimba.
Ripoti hiyo imemuibua Waziri wa Afya na wadau wa afya ya uzazi ambao wamesema kuongezeka matumizi ya dawa hizo kwa vijana kunachangiwa na uelewa mdogo juu ya haki zao za afya ya uzazi ambapo kwa kutotambua haki zao inawawia vigumu kuchukua hatua kuulizia taarifa au huduma za uzazi wa mpango zilizopo kwani wanaogopa kueleweka vibaya na jamii iliyowazunguka.
Mratibu wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) mkoa wa Shinyanga, Gloria Mbia alisema sababu nyingine ni vijana kutokuwa na taarifa sahihi juu ya huduma za afya ya uzazi zinazopatikana bure katika vituo vya afya vya serikali, mazingira ya utoaji huduma hizo katika vituo vya afya sio rafiki na hakuna usiri ambapo watoa huduma wamekuwa na mtazamo hasi juu ya vijana kutumia huduma za uzazi wa mpango hivyo mara nyingi kuwatishia, kuwatukana na hata kuwafukuza.
“Hii huwakatisha tamaa ya kurudi tena na hivyo pale ambapo atafanya ngono zembe huamua kutumia P2 kwa kuogopa mimba ukizingatia upatikanaji wa P2 ni rahisi katika maduka ya dawa, lakini pia huchangiwa na ujana wakiamini kuwa kufanya ngono wakiwa na Kondomu sio tamu na kushawishiana kutumia P2 kujikinga na mimba,” alisema Gloria.
"Insababishwa pia na mabinti kukosa uhuru wa majadiliano na wenza wao kuhusu ngono salama ambapo mfumo dume unawanyima nafasi mabinti kujadili na kufanya maamuzi ya njia sahihi kwahiyo wanaona bora ajilipue kwa ngono zembe alafu atameza P2 peke yake baadae na atakuwa amemfurahisha mwanaume wake na atapendwa zaidi hivyo hawana maamuzi juu ya miili yao," alisisitiza.
Alishauri elimu kwa vijana juu ya afya ya uzazi itolewe kubadili mitizamo ya jamii na watoa huduma kuhusu matumizi ya bidhaa za uzazi wa mpango kwa vijana kwani ni kundi linalohitaji huduma hiyo sana kutokana na mihemko ya mwili katika umri wao huku Serikali ikitakiwa kuona umuhimu wa kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma hizo katika vituo vya afya.
Meneja utetezi wa taasisi ya Tanzania Communication and Development Center (TCDC), James Mlali alisema kitendo cha mabinti kupenda kutumia vidonge vya kuzuia mimba na kuacha matumizi ya kondomu ni jambo la kusikitisha kwa sababu vidonge hivyo ni vya tahadhari na matumizi yake yanapaswa kutumiwa kwenye mazingira ya dharura huku akishauri vijana waelimishwe na kushauriwa wasianze ngono katika umri mdogo wajizuie kwa kujielekeze katika kujiendeleza kielimu na kiuchumi.
“Wanafanya makosa sana kuacha kutumia njia za kawaida na kuamua kutumia njia hiyo ya dharura (vidonge) kama njia yao ya kuzuia mimba kutungwa, inabidi wapewe elimu na taarifa sahihi na hapa ni eneo la vyombo vya habari na wadau kutoa mchango wao kwa kuwaelimisha vijana na jamii, hata watu wanaotumia vidonge vya kawaida vya uzazi wa mpango kama anaona uhusiano alionao hana imani nao sana dual protection kama Kondomu inashauriwa,” alisema Mlali.
Mtaalam wa afya, Flora Gaguti alisema njia nzuri ya kukabiliana na jambo hilo ni kufundisha vizuri elimu rika mashuleni kwani vijana wanapitia vishawishi vingi kwenye zama hizi za utandawazi huku akishauri dawa hizo zisitolewe kiholela na kusisitiza elimu ya madhara ya kutumia P2 kwani mabinti wanaweza kujikuta wakipoteza uwezo wa kubeba tena mimba.
Waziri wa afya, Ummy Mwalimu
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram Februari 15, mwaka huu, Waziri wa afya, Ummy Mwalimu alitoa msimamo akionyesha kulipokea suala hilo akikiri kuwa linafanywa na watoto wa kike walio shuleni huku akiweka wazi kuwa serikali haitoziwekea vikwazo dawa hizo na wanatamani upatikanaji wake usiwe na changamoto (zipatikane haraka na kwa kila mwenye uhitaji aliepata dharura).
Waziri Ummy alisema Serikali inatambua kuwa kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi ya vidonge hivyo hasa kwa watoto wa shule ambao kwa sasa inaonekana wanaogopa zaidi mimba kuliko Ukimwi huku akionya kwani matumizi holela ya P2 yanaweza kuzalisha matatizo mengine makubwa ya kiafya kwa wasichana/wanawake ikiwemo Ugumba na Saratani.
“Tunaendelea kuliangalia suala hili kwa mapana yake, wakati tunaendelea kulijadili ndani ya Serikali na wadau, hatua ya haraka tutakazochukua ni kuongeza kasi ya utoaji elimu ya juu ya madhara ya matumizi holela ya dawa hizi (P2),” alisema Ummy.
Akichangia hoja hiyo Mwanamitindo maarufu nchini, Flaviana Matata alishauri elimu ya masuala ya uzazi itolewe kwa mapana zaidi shuleni kwani uwazi utasaidia kupunguza matatizo huku akisisitiza utoaji taarifa usiwe mfinyu kwani unabana taarifa muhimu zaidi ambapo mabinti wakiwa na ufahamu wa mambo mengi kuliko inavyodhaniwa.