Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy
Gwajima akizungumza katika kongamano Maalum kwa ajili ya mapambano ya kutokomeza Ukeketaji
lilichofanyika mkoani Mara katika Wilaya ya Tarime.
Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy
Gwajima akicheza ngoma ya kijadi kutoka wilaya ya Tarime.
Wadau mbalimbali wakifatilia kongamano Maalum kwa ajili ya mapambano ya kutokomeza Ukeketaji lilichofanyika mkoani Mara katika Wilaya ya Tarime.
Baadhi ya wanafunzi wa kike kutoka mkoani mara walishiriki kongamano maalum ya kupinga ukeketaji .
Na WMJJWM- Tarime Mara
Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy
Gwajima, amewapongeza Ngariba waliokuwa wanajihusisha na vitendo vya
ukeketaji baada ya kuacha kufanya vitendo hivyo na kisha kugeuka kuwa
wanaharakati wa kukemea vitendo vinavyo dhalilisha utu wa mtoto wa kike
na kumuachia maumivu makali.
Akifunga
Kongamano Maalum kwa ajili ya mapambano ya kutokomeza Ukeketaji
lilichofanyika mkoani Mara katika Wilaya ya Tarime, Dkt. Gwajima
alisema, kitendo cha Ngariba hao kuacha suala la Ukeketaji na kujiunga
na Serikali katika mapambano hayo ni ujasiri wa hali ya juu na jambo la kupongezwa.
“Mmewasikia
wenyewe wakijieleza hapa, kwamba wapo baadhi yao walikata shauri na
kuacha kuendelea kukeketa, lazima tuwapongeze sana kwa hatua hii. Lakini
baadhi yao wanatishiwa hata kutengwa na jamii zao baada ya kuacha
vitendo hivyo vya kikatili, tuseme kama Serikali na wadau tutakuwa nao
bega kwa bega kuwatetea kwa nguvu zote bila kuchoka” alisema Waziri Dkt.
Gwajima.
Dkt. Gwajima
alisema dhana ya kwamba, mtoto kumvusha rika kutoka usichana kwenda kuwa
mama au mtu mzima sio lazima akeketwe zipo njia mbadala za kumvusha
binti rika ikiwepo kuwapatia mafunzo yakujitambua bila kumuathiri mwili
wake.
Ameongeza kuwa,
zipo athari wanazo kumbana nazo Mabinti wanaokeketwa ikiwepo athari za
kisaikolojia na msongo wa mawazo, kwani, vitendo hivyo hufanywa bila
ridhaa ya wahusika, kupata maumivu makali, kutokwa damu nyingi, kuuguza
kidonda, changamoto za kujifungua na uwezekano wa kupoteza maisha.
“Madhila
mengine kusababisha maambukizi ya magonjwa ya ngono, Virusi vya UKIMWI
pamoja na magonjwa ya njia ya mkojo (UTI), lakini pia uwepo wa kovu la
ukeketaji linalo kusababisha mimba kinzani na unaweza kusababisha
fistula”. alisisitiza Dkt. Gwajima, na kuongeza kuwa,
“Mtoto
anaweza kupata changamoto wakati wa kujifungua ambapo zinaweza
kumsababishia mtindio wa ubongo, na kupata mateso katika maisha yake
yote. aliongeza Waziri Dkt. Gwajima.
Awali
kabla ya kufunga mafunzo hayo, wakichangia mada zilizowasilishwa katika
Kongamano husika, Mangariba hao waliiomba Serikali iwalinde, ili
wasikutwe na madhila kutoka ndani ya Jamii zao.
“Tunapo
acha shughuli za Ukeketaji ni kama tumetangaza vita na wazee wa Mila,
lakini pia Jamii zetu, hivyo Mhe. Waziri, tunaomba sana, tunapo
salimisha zana za Ukeketaji, basi Serikali itungalie namna inavyoweza
kutuwezesha ili tuwe na mitaji na kufanya shughuli mbadala, lakini zaidi
sana, tunaomba tulindwe dhidi ya wanaotutishia, alisisitiza mmoja ya
Ngariiba.
Nao viongozi wa
Dini ambao walikuwa Sehemu ya Kongamano hilo, wameitaka Serikali
kubadili mtazamo wa elimu na kutaka elimu husika izidishwe kwa watoto wa
kiume kwani pamoja na kuwachukuwa Wasichana na kuwapeleka katika
makaazi salama kwa wale wanaokimbia vitendo hivyo, kazi bado ipo kwa
wavulana ambao hawana Elimu ya madhila ya ukeketaji kwa mwanamke
“Ndugu
Viongozi na Washiriki wa Kongamano hili, kwa sasa tumewekeza angalau
kwa watoto wa kike, lakini kuna kundi kubwa la wavulana, hawa tumewaweka
nyuma, niiombe Serikali na Wadau, tulitazame kundi hili, alisema”
Sheikh Khalfan Shaban Mtongori.
Kila
mwaka, mwezi Februari, Tanzania huungana na mataifa mengine Duniani
kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukeketaji kwa Wanawake na
Watoto.
Picha ya pamoja baina ya viongozi wa wizara ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum na kundi la ngariba kutoka wilaya ya Tarime.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464