RODJAZZ, MWANAMUZIKI CHIPUKIZI TANZANIA WA KUTAZAMWA 2022

Mwonekano wa kava la EP ya Barua ya Mapenzi

“Ninatarajia kuachia kazi zenye ubora na ubunifu mkubwa ili kuendana na kasi ya soko la muziki ndani na nje ya Tanzania”

Rodgers George maarufu zaidi kama Rodjazz ni jina jipya katika tasnia ya muziki nchini Tanzania na Afrika. Chipukizi huyo anayeimba miondoko ya muziki wa R&B, Bongo Fleva na Afro-Pop ameibuka na EP aliyoipa jina la Barua Ya Mapenzi. Rodjazz ametupa karata yake kwenye gemu ya muziki akianza na nyimbo tano zinazounda EP hiyo huku akiingia kwenye soko kwa mtindo wa kipekee. 


Rodjazz aliachia EP ya Barua Ya Mapenzi mnamo Februari 7, 2022 na kutangaza rasmi kuingia kwenye soko la muziki. EP hiyo ambayo inaundwa na nyimbo kama Oksijeni, Asilimia 100, Rudi, Upo Moyoni na Barua ya Mapenzi tayari inapatikana katika majukwaa yote makubwa ya kusikiliza na kupakua muziki duniani. Majukwaa hayo ni pamoja na YouTube, Audiomack, Boomplay, Spotify, Apple Music, Deezer, Amazon Music, TikTok na mengine mengi.


Kupitia barua ya Mapenzi Rodjazz anaelezea hisia za maumivu ya mapenzi, upendo wa dhati, majuto ya mapenzi na matamanio ya kuwa bora zaidi kimaisha na kimapenzi. Licha ya uwezo wake mkubwa wa uandishi, sauti na melodi nzuri, moja ya jambo lililoteka macho ya wapenzi wengi wa muziki ni picha ya kava ya EP ya Barua Ya Mapenzi. Katika picha hiyo Rodjazz ameibuka na mwonekano wa morani (kijana wa kimasai) aliyetoka kijijini na kwenda mjini kumsaka aliyekuwa mpenzi wake kumkabidhi barua. 


Kwa tafsiri ya haraka ambayo imechagizwa pia na kusikiliza mashairi ya wimbo huo wa Barua ya Mapenzi, Rodjazz anaonekana kumkabidhi barua mpenzi wake wa muda mrefu ambaye wamepotezana kutokana na sababu za mabadiliko ya kimaisha lakini mrembo huyo mwenye mwonekano wa msichana wa kisasa hayuko tayari kupokea barua jambo ambalo linaashiria kwamba amebadilisha uelekeo na hana hisia tena za mapenzi kwa Rodjazz. 


Akizungumza na Serengeti Post, Rodjazz ameelezea ujio wake katika muziki na matarajio yake katika tasnia hiyo yenye ushindani mkubwa. Rodjazz amesema kwamba mbali na kusukumwa na kipaji chake, pia ameona kuna hitaji kubwa la maudhui ya muziki yanayobeba dhana mbalimbali zinazogusa maisha ya kila siku ya binadamu. 


“Jambo kubwa lililonipa msukumo wa kuingia rasmi kwenye muziki ni kiu kubwa niliyonayo ya kutumia kipaji changu cha muziki kutoa mchango kwa jamii yangu, nchi na jamii ya ulimwengu kwa ujumla. Ninaona kuna mambo naweza kuyaweka kibunifu na kuyawasilisha vyema zaidi kupitia muziki. Muziki ni lugha inayoeleweka zaidi na watu wengi duniani bila kujali tofauti za kidini, kijiografia, kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na rangi. Nami nimelenga kutengeneza maudhui yatakayoelimisha, kuburudisha, kukumbusha na kuunganisha watu.” alisema Rodjazz. 


Rodjazz alizungumza kuhusu EP yake ya Barua ya Mapenzi na kueleza ni kwa nini aliamua kuanza na maudhui ya mapenzi badala ya kugusia dhana nyinginezo, alisema.


“Barua ya Mapenzi ni utambulisho wangu wa kwanza kabisa kwenye safari yangu ya kufanya rasmi muziki. Kabla ya kufikia maamuzi ya kutoa Barua ya Mapenzi kumekuwa na vuta nikuvute ya kujiuliza nitoke vipi na kwa nini. Katika mchujo nilizingatia mahitaji ya soko na kuona kwamba ni muhimu na mimi kutupa sarafu yangu kwenye mada ya mapenzi ambayo inawagusa watu wengi zaidi. Wazo la Barua ya Mapenzi lilikuja na nikaamua kulibeba kulifikisha kwa mashabiki.” amenukuliwa Rodjazz. 


Serengeti Post ilitaka kujua undani wa kilichopo kwenye EP hiyo na kuhoji uhalisia wa mwonekano wa Rodjazz ambaye anaonekana kuvaa kama kijana wa kimasai katika kava ya EP na picha nyingine zilizopo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii. Rodjazz alikuwa na haya ya kusema.


“EP ya Barua ya Mapenzi ina jumla ya nyimbo tano na hizi zote zimebeba ujumbe wa mapenzi kama yanavyotokea katika uhalisia wa maisha ya kitanzania na sehemu nyingi duniani. Mfano wimbo wa Barua ya Mapenzi ambao pia ndio jina la EP unaeleza namna ambavyo wapendanao wanaweza kutenganiswha na sababu mbalimbai na kupelekea kushindwa kuwasiliana kwa njia za kawaida za kisasa hadi mmoja kulazimika kufanya juhudi za kutumia barua. Kuhusu mwonekano wangu wa kimasai, huu ni ubunifu wa namna ya kuonesha maisha halisi ya Tanzania na Afrika. Mimi sio mmasai kwa kabila ila katika duru za ubunifu umasai nimeutumia kuonesha namna ambavyo mapenzi yanagusa kila mtu kwanye jamii bila kujali matabaka.” alifafanua Rodjazz huku akitabasamu. 


Akizungumzia matarajio yake kimuziki Rodjazz amekiri kutamani kuwa nyota mkubwa wa muziki hapa nyumbani Tanzania, Afrika na nje ya bara la Afrika. Rodjazz amesema anatarajia kuachia kazi zenye ubora na ubunifu mkubwa ili kuendana na kasi ya soko la muziki ndani na nje ya Tanzania. 


Rodjazz ambaye ana miaka 25 ni mwandishi wa muziki, mwimbaji na mtumbuizaji mwenye kipaji kinachovutia na kushawishi kufuatilia. Kwa sasa kazi zake zinasimaiwa na lebo mpya ya muziki nchini Tanzania inayojulikana kama Bytes Music. 


Unaweza kusikiliza nyimbo zilizoko kwenye EP ya Barua ya Mapenzi na kutoa maoni na ushauri wako kwa Rodjazz.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464