WANAFUNZI WA KIKE VIJIJINI WAMEIOMBA SERIKALI KUWEKA BEI YA TSHS 500 KWA TAULO ZA KIKE

 




Mwandishi wetu.

Wanafunzi wa kike katika kata ya Pandagichiza Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wameiomba serikali kupunguza kodi katika taulo za kike ili waweze kuzinunua kwa Shs 500 ili ziwasaidie kujistiri kwa upatikanaji wa gharama ya bei nafuu.

Wakizungumza na Shinyanga Press Club blogspot mwanzoni ya wiki ya February,2022 katika utekelezaji wa mradi wa kutokomeza ukatili baina ya Mfuko wa Wanawake Tanzania kwa kushirikiana na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga ili kufahamu changamoto zinazowakabili wasichana  wa vijijini juu ya upatikanaji wa taulo za kike.

Baadhi ya wasichana wa shule za msingi na sekondari kutoka vijiji vya Sayu ,Ng'wamadelanha, Shilabela, pamoja na Pandagichiza wilayani Shinyanga ambao wanawakilisha sehemu kubwa ya wanafunzi wa maeneo ya vijijini kuendelea kukwamishwa na ukosefu wa taulo za kike na vyoo maalum wakati wa hedhi.

Amina Ngasa anayesoma shule ya Pandagichiza alisema wamekuwa wakipatiwa msaada kutoka mashirika mbalimbali lakini zinapokwisha wanarudi kutumia njia za asili kujistiri.

Tunaiomba serikali ishushe kodi za taulo ili tuzinunue kwa kujibana, kuliko hivi sasa zinauzwa Shs 2,000 hadi 3,000 na hatuwezi kuzimudu wakati pamoja na walezi wetu tukiwawaomba wanasema hawana hivyo tunabakia kwenye njia za asili” Alisema Amina

Mariamu Kashinje alisema kuwa shule yao ni ya kata, kuna vyoo vya kujistiri lakini tatizo kubwa ni kukosekana upatikanaji wa taulo za kike na kuwafanya kuwa na hofu wakati wanapoingia katika siku zao.

Mwanafunzi Scholastica Madatula anayesoma darasa la saba katika shule ya msingi Pandagichiza wilayani Shinyanga, anasema kutokana maeneo yao kuwa ya vijijini, hali ya upatikanaji wa taulo za kike ni ngumu na hata wazazi na walezi kushidwa kuzimudu kwa gharama hali inayowafanya  kuendelea kutumia njia za asili kujistiri.

Changamoto ya utoro katika shule za maeneo ya vijijini ina changiwa na ukosefu wa taulo za kike za kuweza kuwasaidia wasichana kuwa na namna bora ya kujistiri kwa kuwa uwezo mdogo wa wazazi juu ya gharama za pedi unawakwamisha kuwahudumia mabinti zao.

Naye mwalimu wa Afya wa shule hiyo, Lucy Maugo anasema hali ya upatikanaji wa taulo za kike ni ngumu na wanachokifanya ni kutoa elimu ya hedhi salama, pamoja na mbinu za kujistiri ili kuepuka utoro pindi mabinti wanapokuwa katika hali hiyo.

Deogratius Mashamba ni mtendaji wa kata ya Pandagichiza wilayani Shinyanga, anasema kata hiyo ina shule nne za msingi na sekondari iko moja na shule hizo za msingi zilizo na vyoo kwa ajili ya matumizi ya hedhi ni sayu, shilabela na sekondari, huku shule ya Pandagichiza na Ng"wamadelanha zikikosa vyoo.

Mratibu wa afya ya uzazi na mtoto mkoani Shinyanga, Joyce Kondoro, anasema  matumizi ya njia za asili wakati wa hedhi kwa kutumia vitambaa kunahitaji usafi wa hali ya juu ili kuzuia vimelea vya magonjwa au bakteria.

“Baadhi ya magonjwa ya yanayoweza kusababishwa na ukosefu wa taulo za kike ni pamoja na UTI, fangasi, kujikuna kutokana na uchafu sehemu za siri unaotokana na mashambulizi ya vimilea vya magonjwa(bakteria)"Alisema Joyce

 


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464