Wanawake wa kata ya Masengwa Halmashauri ya wilya ya Shinyanga wakishikiri mafunzo kutoka shirika la WEADO.
Afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Aisha Omary akizungumza na jukwaa la wanawake kata ya Masengwa.
Afisa maendeleo ya jamii kata ya Masengwa akizungumza na wanafunzi kabla ya uchaguzi wa baraza la watoto.
Afisa miradi wa WEADO Salome Shangari akitoa mafunzo kwa jukwaa la wanawake kata ya Masengwa
Suzy Butondo, Shinyanga
Afisa
maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Aisha Omary
amewataka wanawake wa kata ya Masengwa kuchangamkia fursa za kiuchumi
zilizopo kijijini hapo,na kuacha kumtegemea mwanaume peke yake hali
ambayo itaweza kupunguza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Pia
amewataka kina mama waache kuwaogopa watoto wao katika kuwaonya wakati
wanapokosea, badala yake wawafundishe maadili mema, kuacha kufanya
maovu mbalimbali yakiwemo ya kiukatili wa jinsia, ili kuwa na kizazi
chenye amani na utulivu.
Aisha
amesema hayo kwenye semina ya kuwajengea uwezo jukwaa la kina mama wa
kata ya Masengwa ili waweze kujishughulisha na kujipatia kipato, na
kupunguza matukio mbalimbali ya kikatili yanayofanywa na baadhi ya
wanaume, iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Women Elderly
Advocacy and Development Organization (WEADO),la kutokomeza ukatili wa
wanawake dhidi ya watoto.
Amesema matukio ya kupigwa kina mama yamekuwa mengi kutokana na wanawake kuwategemea waume zao kwa kila kitu, ili kuondokana na matukio kama hayo ni vizuri kina mama wakaanza kujishughulisha kwa kulima bustani za mboga mboga na kuzimwagilia kwa sababu wana bwawa ambalo linadumu kwa muda mrefu, kujishughulisha na biashara ndogo ndogo, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha watoto na kuwafundisha maadili mema.
" Matukio matukio ya ukatili wakijinsia yamekuwa yakijitokeza mara kwa
mara kwa sababu mwanamke hana pa kushika lakini kama unajishughulisha
utapata chochote na mme wako atapata, hivyo mtachanganya na kuweza
kufanya chochote cha kimaendeleo hata mwanaume atakuheshimu hawezi
kukupiga tena bila kosa lolote kwa sababu mtakuwa mnaingiza fedha
wote,"amesema Omary.
Afisa
miradi wa WEADO Salome Shangari , alisema wanawake wakichangamkia fursa
ukatili wa kunyanyaswa, kupigwa na kutelekezwa utapungua ama utaisha
kabisa kwa sababu kila mmoja atakuwa anaingiza kipato katika majira yote
si kusubiri wakati wa kiliomo tu, hivyo ni vizuri mafunzo haya
wakayatekeleza wasikae na kusubiri
matumizi kwa wanaume.
Aidha
Afisa tathimini na ufuatiliaji kutoka shirika hilo la WEADO John Eddy
alisema licha ya kuchangamkia fursa pia kina mama wanatakiwa kuwakemea
watoto ili waache kutenda maovu,kwani mara nyingi wazazi wa kike
wanaogopa kuwakemea watoto wanapofanya maovu na kuwaachia wanaume peke
yao, hali ambayo imekuwa ikisababisha mtoto kuharibika na kutokuwa na
maadili mazuri.
"Pia
katika malezi tujitahidi wazazi kuwalea watoto wetu katika maadili mema
watoto wetu ni wajanja sana, ukiangalia na huu utandawazi wa tv simu
kuna vitu vingine hawatakiwi kuviangalia, tuseme nao tusiwaogope ili
wasiige mambo ya wakubwa na kuharibu future yao ya kimaisha"amesema
Eddy.
Baadhi ya wanawake
waliojiunga kwenye jukwaa la wanawake kata ya masengwa Suzana Dotto
amesema wanawake wengi wamekuwa wakiteseka kwa sababu hawana pakushika,
wanafanyiwa ukatili wa kupigwa na waume zao wanavumilia tu,lakini kwa
sasa kutokana na mafunzo haya kila mmoja ataenda kutoa elimu kwa
mwanamke mwenzake ili aweze kujishughulisha kulingana na fursa aliyoko
kwenye kijiji chake.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa jukwaa la akina mama Mwajuma Luchembela mkazi
wa kijiji cha Bubale kata ya Masengwa amesema analishukuru sana shirika
la WEADO kwa kuwaelimisha jukwaa la wanawake kwani elimu walioipata
wanawake itasaidia sana kupunguza ukatili wa kijinsia, wanawake wengi
wamekuwa wakiteseka kwa sababu ya kutokuwa na pakushika anategemea apewe
matumizi na mwanaume.
"Wengi
wetu tunategemea kudaka tu,lakini Mwanamke akiwa na kipato anaweza
kumsaidia mme wake amekwama,atamsaidia mtoto kumnunulia madafutari
kalamu pamoja na mahitaji mbalimba watasaidizana na wataishi kwa amani
na furaha hata chuki hazitakuwepo tena unaamini hilo",amesema Mwajuma.
Leokadia
Masegese mkazi wa kata ya Masengwa ambaye ni muhasibu wa jukwaa la
wanawake kata hiyo, amesema wakati mwingine wanaume wanakuwa na hasira
kwa sababu hawana hela, hivyo anajua nikifika na furaha nyumbani
nitaombwa hela hivyo anakuwa mkali na wakati mwingine kukupiga kwa
kisingizio furani ili usimuombe hela hata ya chumvi.
Hata
hivyo Shirika la WEADO licha ya kutoa mafunzo kwa jukwaa la wanawake,
pia lilitoa mafunzo kwa baraza la watoto kata ya masengwa na kufanikiwa
kuchagua viongozi wa baraza la watoto la kata hiyo,ambapo alichaguliwa
mwenyekiti, katibu, mwasibu na wajumbe wa baraza hilo, ambao waliahidi
kutoa elimu kwa jamii ili kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya
wanawake na watoto.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464