CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA WILAYANI KAHAMA(KACU) KIMEFANYA UCHAGUZI NA KUPATA UONGOZI MPYA.
Mrajisi msaidizi kutoka makao makuu Dodoma Emanuel Sanka ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo kutoka kushoto ni katibu tawala wilaya ya Kahama Timothy Ndanya na kulia kwake ni mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa Hilda Boniface.
Wajumbe wa mkutano maalum kutoka vyama mbalimbali vya msingi wakisubiri maelekezo ya kupiga kura
Wagombea nafasi ya uenyekiti wa chama kikuu cha ushirika wilayani Kahama mkoani Shinyanga KACU ambapo upande wa kwanza kulia ni Emanuel Nyambi na Hamisi Majogaolo.
Mwenyekiti wa KACU ,Hamis Majogolo aliyesimama akiongea baada ya kupata ushindi.
Na Neema Sawaka
Kahama
CHAMA kikuu cha ushirika wilayani Kahama mkoani Shinyanga (KACU) kimefanya uchaguzi na kumpata mwenyekiti Hamis Majogolo na makamu mwenyekiti Tano Nsabi kwa kuongoza kwa kipindi cha miaka miwili iliyobaki.
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika kutoka makao makuu Dodoma Emanuel Sanka alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo uliofanyika jana na viongozi hao kutangazwa washindi baada ya kupigiwa kura na wajumbe 245 waliohudhuria mkutano maalum kwaajili ya uchaguzi.
Sanka alimtangaza mwenyekiti mpya wa ushirika huo Hamis Majogolo kwa kupata kura 127 na kumzidi mshindani wake Emanuel Nyambi aliyepata kura 117 huku kura moja ikiwa imeharibika.
Sanka pia alimtangaza makamu mwenyekiti Tano Nsabi aliyepata kura 137 baada ya kuwashinda wapinzani wenzake watatu waliokuwa kwenye kinyang’anyiro hicho huku mwakilishi wa vyama vya msingi taifa Daniel Mwita aliyepata kura 102 akitangazwa mshindi kwa kuwazidi wapinzani wenzake wanne katika kinyang’anyiro hicho.
“Kwa mujibu wa sheria na katiba ya ushirika viongozi hao watadumu kwa miaka miwili baada ya miaka mitatu baada ya uchaguzi huo kufanyika mwaka jana mwanzoni na viongozi waliochaguliwa kuondoka na mwingine kufariki”alisema Sanka.
Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Shinyanga Hilda Boniface alisema kuwa maamuzi waliyoyatoa wajumbe kupata viongozi watayazingatia na kuyaheshimu huku akiwataka wajumbe kumpatia ushirikiano wakutosha mwenyekiti ili kufanya ushirika huo kusonga mbele zaidi.
Katibu tawala wilaya ya Kahama Timothy akiwa mgeni rasmi katika uchaguzi huo kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo Festo Kiswaga alisema kuwa viongozi waliochaguliwa wajue wamebeba maisha ya wananchi walioko kwenye maeneo yao kuanzia sasa makundi yaliyokuwepo yavunjwe kazi iendelee.
“Kweli viongozi mmepata tunataka kuona mafanikio yakutosha katika usimamizi wa mazao ya pamba na tumbaku kwa wakulima kwani mafanikio tumeyaona kupitia ushirika msimu uliopita mmeweza kununua pamba kilo moja sh 1500 ndiyo serikali inataka uongozi imara unaowaletea faida wakulima”alisema Ndanya.
Mwenyekiti aliyechaguliwa Hamis Majogolo alishukuru wajumbe kumchagua na kumuamini kwani ameziona changamoto zilizopo kwa wakulima wa zao la pamba na tumbaku atahakikisha anatembelea kila amcos kwa kushirikiana na wataalamu ili kuweza kuwanyanyua wakulima waendane na soko.
Uchaguzi huo umekuja kufuatiwa na aliyekuwa mwenyekiti wa ushirika huo Emanuel Cherehani kuchaguliwa mwaka jana kuwa mbunge wa jimbo la Ushetu na sheria kumtaka kuachia nafasi hiyo huku makamu mwenyekiti Geofrey Mbuto aliyefariki dunia mwezi Janurai mwaka huu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464