Freeman Mbowe: Mwenyekiti wa Chadema aachiwa huru.
Mwendesha mashtaka mkuu wa serikali amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi, katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, hatua ambayo imepelekea Mbowe na wenzake watatu kuachiliwa huru mara moja.
Mahakama hiyo ilikuwa inamshikilia Mbowe na wenzake watatu kwa kesi ya kujibu kuhusiana na tuhuma mbalimbali zikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi.
Taarifa iliowasilishwa na serikali ilisema yafuatayo:
" Taarifa hii tunaiwasilisha kwa njia ya maandishi, kwa maombi hayo ya Kifungu cha 91(1) tunaomba kuondoa mashitaka yote dhidi ya washitakiwa wote sababu zote zipo katika Nole Prosequi {ikimaanisha musimshitaki} ambayo tumeiwasilisha" alisema wakili wa serikali mbele ya jaji Joachim Tiganga ambaye amekua akisimamia kesi hiyo.
Baada ya Mahakama kusikiliza hoja iliyoletwa na wakili mwandamizi wa Serikali kwamba Mkurugenzi wa Mashitaka hana nia ya kuendelea na kesi hii, na upande wa pili wakaridhia, Mahakama inasema shauri hili lililokuwa linawakabili washitakiwa Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling'wenya na Freeman Mbowe linaondoshwa mahakamani na washitakiwa wanaachiwa huru bila masharti.
''Kwa sababu kuna vielelezo vililetwa Mahakamani, naandaa amri ya kuviachia, na hivyo naelekeza Mkuu wa Magereza kuwaachiwa mara moja leo na si vinginevyo'', alisema jaji.
Yafuatayo ni matukio muhimu ya kesi hii iliyokuwa ikifuatiliwa kwa ukaribu ndani na nje ya nchi:
Julai 21, 2021: Mbowe alikamatwa
Kiongozi huyu mkuu wa Chadema alitiwa mbaroni huko jijini Mwanza usiku wa kuamkia tarehe 21 mwezi Julai, 2021. Chama chake cha Chadema, kiliwataka wafuasi wa chama hicho kuingia mtaani kumtafuta baada ya juhudi zake za kumtafuta kukwama na hawajui walipo, baada ya Mamlaka kutosema lolote kwa muda kuhusu kukamatwa kwa Mbowe. Baadae Polisi walikuja kuthibitisha kumkamatwa na kwamba amesafirshwa kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam na kuunganishwa kwenye kesi ya ugaidi.
Taarifa ya Msemaji wa Polisi, David Misime ilisema kuwa Mbowe hakukamatwa kwa tuhuma za kupanga na kuandaa kongamano la Katiba mpya jijini Mwanza bali alifahamu tuhuma zinazomkabili.
Julai 26, 2021: Alifikishwa mahakamani
Julai 26, 2021 na kusomewa mashtaka mawili ikiwemo la ugaidi. Baada ya kusomewa maelezo Mbowe hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka, kesi ikahairishwa hadi Agosti 5, 2021 kusubiri nyaraka ili ihamishiwe Mahakama kuu.
Agosti 6, 2021 Alisomewa Mashitaka
Mbowe ambaye ni kiongozi wa zamani wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB) na wenzake watatu walisomewa mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa kufanya vitendo hivyo.
Mashtaka mengine ni kukusanya fedha kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, kukutwa na silaha aina ya bastola na kukutwa na sare za jeshi kinyume cha sheria. Kati ya mashtaka hayo sita, Mbowe anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi.
Agosti 9, 2021: Rais Samia azungumzia Kesi ya Mbowe
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan licha ya kusema hawezi kuzungumzia zaidi kesi ya Mbowe kwa kuwa iko Mahakamani, aliiambia BBC kuwa mashtaka dhidi ya kiongozi huyo wa Upinzani hayakuchochewa kwa sababu za kisiasa.
Pamoja na mengine kauli yake hiyo iliibua mjadala mzito kwa wafuatiliaji wa kesi hiyo na siasa za Tanzania kwa ujumla.
Septemba 03, 2021: Kuanza kusikilizwa kwa kesi
Kesi hii ilianza kusikilizwa kwenye Mahakama kuu ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ikitokea Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu ambayo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kisheria.
Septemba 6, 2021: Jaji Luvanda ajitoa kusikiliza kesi
Jaji Elinaza Luvanda alijitoa kusikiliza kesi hiyo kufuatia maombi ya Mbowi, kwa niaba ya washitakiwa wenzake kudai kuwa hawana Imani na Jaji huyo kama atatenda haki. Nafasi yake akapangiwa Jaji Mustapha Siyani.
Oktoba 20, 2021 Jaji Siyani ajitoa kusikiliza kesi
Jaji Mustapha Siyani alikuwa jaji wa pili kujitoa kusikiliza kesi hiyo kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Jaji kiongozi. Jaji Joachim Tiganga akachukua nafasi yake
Februari 13, 2022: Ushahidi Kufungwa
Ushahidi umefungwa Wiki hii Februari 13, 2021 kwa mashahidi 13 wa upande wa mashtaka kumaliza kutoa ushahidi wao. Kinachosubiriwa sasa ni uamuzi wa Mahakama Kuu hiyo kuamua leo kama Mbowe na wenzie wana kesi ya kujibu ama la.