WAZIRI NDAKI ATEMBELEA MACHINJIO YA KISASA SHINYANGA, SHAMBA LA MIFUGO ATOA MIEZI MINNE WANANCHI WAHAME


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, (kulia) akiwa katika Machinjio ya kisasa ya Mifugo iliyopo Ndembezi Manispaa ya Shinyanga (kushoto) ni Mkaguzi Mkuu wa Machinjio hiyo Ernest Nigo.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, amefanya ziara katika Machinjio ya kisasa iliyopo Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, na kukumbana na changamoto ya idadi ndogo ya mifugo ambayo inachinjwa kwenye machinjio hiyo kwa siku tofauti na malengo yaliyokusudiwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga John Tesha, akisoma taarifa ya machijio hiyo ya kisasa kwa Waziri Mashimba Ndaki leo April 14, 2022 alisema ilianza kujengwa mwaka 2017 kwa gharama ya Sh.bilioni 5.1 na ilianza kufanya kazi Novemba mwaka jana.

Alisema matarajio ya machinjio hiyo ilikuwa ni kuchinja Ng’ombe 500 na Mbuzi 1,000 kwa siku, lakini hali imekuwa tofauti na kuchinjwa Ng’ombe 38 na Mbuzi 40 tofauti na malengo tarajiwa.

“Mradi wa ujenzi wa machinjio hii ya kisasa lengo lake ni kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na mnyororo wa thamani ya nyama na upatikanaji wa nyama safi na salama na kulinda afya za wananchi, pamoja na kuongeza mapato kwa wadau wote wa mifugo, wafugaji, wafanyabiashara na Serikali, lakini changamoto tuliyonayo ni upungufu wa mifugo,”alisema Tesha.

Aidha, alisema mikakati iliyopo kwa sasa wanatafuta wawekezaj ambao wanafanya biashara ya kusafirisha nyama nje ya nchi, ili watumie machinjio hiyo na kufikia lengo halisi la kuchinja Ng'ombe 500 na Mbuzi 1000 kwa siku.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, aliagiza machinjio hiyo ya kisasa inapaswa kutangazwa zaidi katika mikoa ya jirani, ili itambulike na wafugaji kupeleka mifugo yao hapo na kufikia malengo ya kuchinja mifugo mingi.

Alisema Wizara watakwenda kulifanyia kazi suala la kutafuta mwekezaji kwenye machinjio hiyo, ambaye pia atakuwa akiuza nyama ndani na nje ya nchi na kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuacha kuendelea kuchinja mifugo chini ya wastani.

Katika hatua nyingine akizungumza upande wa shamba la mifugo lililopo Chibe Manispaa ya Shinyanga, ameagiza wananchi ambao wamevamia eneo hilo hadi kufikia Agost 30 mwaka huu, wawe wameshahama kwa hiari yao wenyewe kabla ya Serikali kuwachukulia hatua.

Alisema kwa sasa Serikali inataka kulitumia shamba hilo, kwa kunenepesha mifugo pamoja na kuizalisha, ili kupata mifugo mingi na kutatua tatizo la upungufu wa malighafi ya mifugo kwenye viwanda vya nyama na machinjio za kisasa hapa nchini.

“Wananchi ambao mmevamia shamba hili la mifugo hadi kufikia Agost 30 mwaka huu, nina agiza muwe mmeshahama kwa hiari yenu wenyewe kabla ya Serikali kutumia nguvu, vuneni mazao yenu ambayo mmelima pamoja na kubomoa nyumba zenu, Shamba hili Serikali tunataka kulitumia,”alisema Ndaki.

“Namwagiza Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko ikifika Agost 30 aje kwenye shamba hili na kufanya kazi ya kuwaondoa wananchi wote ambao watakuwa wamekaidi agizo la Serikali la kuhama kwa hiari yao wenyewe,” aliongeza.

Katika hatua nyingine Waziri huyo alitoa wito kwa wafugaji hapa nchini wafuge kibiashara na siyo kienyeji, sababu kwa sasa masoko ya kuuza mifugo yapo na watapata pesa nyingi na kuinuka kiuchumi.

Kwa upande wake msimamizi wa shamba hilo la mifugo Lini Mwala, alisema lina ukubwa wa hekali 5,250 na lilianzishwa na Serikali kwa madhumuni ya kupumzisha mifugo na ukaguzi wa magonjwa ya mifugo ili kutosambaza magonjwa na kusababisha madhara zaidi.

Nao baadhi ya wananchi ambao wamevamia kwenye shamba hilo la mifugo akiwamo Lucas Machibya, walikiri kuvamia eneo hilo huku wakiomba wapewe muda zaidi wa kuhama angalau mwaka mzima, ili wakajenge nyumba kwanza katika maeneo mengine kwa madai bado hawajajiandaa vizuri.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, akizungumza mara baada ya kutembelea Machinjio ya kisasa ya mifugo iliyopo Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga John Tesha, akisoma taarifa ya ujenzi wa machinjio hiyo ya kisasa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, (kulia) akisikiliza maelezo ya hatua za uchinjaji wa mifugo katika Machinjio hiyo ya kisasa, (kushoto) ni Mkaguzi mkuu wa machinjio hiyo Ernest Nigo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, akiendelea kusikiliza maelezo hatua za uchinjaji wa mifugo katika machijio ya kisasa iliyopo Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, akiendelea kusikiliza maelezo hatua za uchinjaji wa mifugo katika machijio ya kisasa iliyopo Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, akiendelea kusikiliza maelezo hatua za uchinjaji wa mifugo katika machijio ya kisasa iliyopo Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, akiendelea kusikiliza maelezo hatua za uchinjaji wa mifugo katika machijio ya kisasa iliyopo Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

muonekano wa machinjio ya kisasa iliyopo Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, (kushoto) akiangalia namna wananchi walivyovamia Shamba la Mifugo lililopo Chibe Manispaa ya Shinyanga, na kufanya shughuli za kilimo na kujenga nyumba za makazi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, (kulia) akiwa ziarani Shinyanga, (kushoto) ni Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga John Tesha.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464