MGODI WA ALMASI WA WILLIAMSON DIAMONDS WATANGAZA KUANZISHA MAHUSIANO MAPYA NA VIJIJI

MGODI WA ALMASI WA WILLIAMSON DIAMONDS WATANGAZA KUANZISHA MAHUSIANO MAPYA NA VIJIJI 

Meneja wa kampuni ya Petra Diamond Mhandisi Ayoub Mwenda akizungumza na wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa mwadui.
Wananchi wa wanaowakilisha vijiji 12 vinavyozunguka mgodi wa mwadui.

Na. Mwandishi Wetu,

Shinyanga

MIGOGORO ya mara kwa mara kati ya Kampuni ya Williamson Diamonds Ltd iliyopo Mwadui wilayani Kishapu mkoani Shinyanga na wakazi wa vijiji 12 vinavyouzunguka mgodi huo hatimaye huenda ikafikia ukomo.

Hali hiyo imebainishwa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya uongozi wa Mgodi wa Williamson Diamonds Ltd unaomilikiwa na mwekezaji Kampuni ya Petra Diamonds  kutangaza rasmi kuanzisha mahusiano mapya na ya karibu kati yake na wananchi wa vijiji hivyo 12.

Akizungumza katika kikao maalumu kilichowashirikisha wawakilishi wa wananchi, viongozi wa kidini na makundi ya kijamii, Meneja kitengo cha mahusiano ya Jamii wa mgodi, Bernard Mihayo alisema kuanzishwa kwa mahusiano mapya kutapunguza matatizo mengi yaliyokuwa yakijitokeza huko nyuma.

Mihayo alisema ili kuweza kuendesha shughuli za Mgodi kwa faida na kwa maslahi ya Taifa uongozi wake umeamua kufungua ukurasa mpya wa mahusiano kati yake na wakazi wa vijiji hivyo 12 vinavyouzunguka hali itakayopunguza matukio yaliyokuwa yakitokea na kusababisha wananchi wa maeneo hayo kuulalamikia mgodi.

Akifafanua Meneja huyo alisema katika kuhakikisha lengo hilo linafikiwa tayari uongozi wa mgodi umeanzisha Kitengo maalumu cha mahusiano ya jamii ikiwa ni idara kamili inayojitegemea ambapo huko nyuma kitengo hicho hakikuwepo.

Pamoja na kuanzishwa idara mpya, lakini hivi sasa tumeweka Ofisi maalumu pale katika lango kuu la kuingilia mgodini itakayowezesha wananchi wenye malalamiko yoyote au mahitaji muhimu, waweze kufika pale bila kulazimika kuomba vibali vya kuingia mgodini na hapo watasikilizwa shida zao au kupokelewa malalamiko yao,” anaeleza Mihayo.

Alisema Mwekezaji anayemiliki mgodi Kampuni ya Petra Diamonds hivi sasa anataka kuona Mwadui inakuwa mpya kwa kuanzisha mahusiano mapya na ya karibu zaidi na jamii inayouzunguka mgodi huo na kuzika tofauti zote zilizokuwa zikijitokeza huko nyuma.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Mgodi huo, Sylvia Mlogo alisema tayari mgodi huo pia umepokea na kuanza kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Mahakama ya Uingereza ambako baadhi wa wafanyakazi waliotendewa vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu walifungua madai yao.

Mlogo alisema baada ya kufunguliwa kwa kesi hiyo, iliamriwa kufanyika mazungumzo nje ya mahakama kati ya walalamikaji na mwekezaji na kuelekeza paanzishwe mfumo mpya wa upokeaji wa malalamiko ya wananchi wanaodai kutendewa vitendo vya uvunjifu wa haki za kibinadamu hapa hapa nchini.

“Kimsingi kama mgodi tumeyapokea vyema maagizo ya Mahakama hiyo, na hivi sasa tunataka kuyatekeleza sambamba na kuimarisha mahusiano  baina ya mgodi na jamii inayotuzunguka, tunaomba jamii iwe na imani na mfumo huu, na sisi tunaahidi kwamba tunaenda kujenga Mwadui mpya ya ujirani mwema,”

Tuwaombe tu wanajamii waelewe kwamba pamoja na mgodi huu kuwa chini ya mwekezaji kutoka nje ya nchi lakini pia unamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania, na ndiyo inayowakilisha wananchi, hivyo mali hii pia ni mali yao, kimsingi wasaidie pia katika kuilinda ili faida iweze kuongezeka,” alieleza Mlogo.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa mgodi huo, Mhandisi Ayoub Mwenda alisema katika kuhakikisha mahusiano yanayokusudiwa yanaimarika, hivi sasa wameanza mchakato wa kuangalia ni maeneo yapi ambayo jamii inapaswa kusaidiwa ikiwemo wachimbaji wadogo ili kukuza vipato vyao.

Hili kundi la vijana linasaidiwaje kama hawana ajira? Tujiulize hapa, Serikali inafanya kila inachoweza kuwasaidia vijana nchini, na sisi je? Wajibu wetu sisi ni kuendelea kushirikiana Serikali katika kuwatafutia hawa vijana kazi za kufanya zitakazowapa vipato, wakiwa na kazi, matatizo mengi yatapungua,” alieleza Mhandisi Mwenda.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464