MTOTO ALIYEKUWA AMEKATAZWA NA BABA YAKE KUSOMA, AMUOMBA RAIS SAMIA AWAJENGEE WATOTO WA KIKE MABWENI

 MTOTO ALIYEKUWA AMEKATAZWA NA BABA YAKE KUSOMA, AMUOMBA RAIS SAMIA AWAJENGEE WATOTO WA KIKE MABWENI

Mwanafunzi Neema Mayunga akiwa darasani baada ya kukwepa ndoa   kwa ujasiri wake kupitia barua aliyowandikia waalimu akiomba msaada.


Mwanafunzi Neema Mayunga (katikati) akiwa na walimu wake wa Shule ya Sekondari Itwangi, wilayani Shinyanga. (Picha na Suleiman Abeid)


 

Mwanafunzi Neema Mayunga akipongezwa na mwalimu wake wa darasa kutokana na ujasiri aliouonesha na kuweza kuendelea na masomo yake badala ya kuolewa akiwa na umri mdogo (Picha na Suleiman Abeid) 

Mwanafunzi Neema (mwenye sare ya bluu) akiwa darasa akiendelea na masomo ya kidato cha kwanza. (Picha na Suleiman Abeid)

 

Mwanafunzi Neema akiwa pamoja na Mkuu wake wa Shule ya Sekondari Itwangi, Amos Kilanga (Picha na Suleiman Abeid)

Na Suleiman Abeid,

RAIS Samia Suluhu Hassan ameombwa kuwanusuru watoto wa kike nchini wanaokabiliwa na wimbi la mimba za utotoni na wanaokatishwa masomo na wazazi wao kwa kuwajengea mabweni kwenye shule wanazosoma baada ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Ombi hilo limetolewa na mwanafunzi wa kike anayesoma kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Itwangi, Neema Mayunga (14) ambaye awali alikatazwa na baba yake asijiunge na masomo ya sekondari ili aweze kuolewa.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, Neema anasema changamoto ya ukosefu wa mabweni kwenye shule nyingi za sekondari za kata ni moja ya chanzo cha wengi wao kukatisha masomo yao kutokana na kupata mimba baada ya kushindwa kukwepa vishawishi vya wanaume wanaokutana nao njiani.

Akifafanua anasema shule nyingi za kata zipo mbali kutoka maeneo wanayoishi hivyo kuwalazimu kutembea umbali mrefu kila siku kwenda shule na kurudi nyumbani huku akijitolea yeye mwenyewe kwamba shule yao ipo umbali wa kilometa saba kutoka kijiji wanachoishi.

“Nafikiri ni wakati muafaka sasa wa kumuomba Rais wetu Samia Suluhu  Hassan baada ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule zetu za Sekondari sasa ahamishie nguvu hizo kwa kutujengea mabweni ili watoto wa kike tuweze kuishi shuleni,"

Umbali wa shule ni changamoto kubwa kwetu, mfano mimi nalazimika kutembea kilometa saba ili nifike shule na kilometa saba nyingine kurudi nyumbani, hivyo kwa kila siku za masomo natembea kilometa 14, ni mbali ukilinganisha na umri wangu wa miaka 14,” anaeleza Neema.

Anasema katika kutembea njiani wanakutana na vishawishi vingi hasa kutoka kwa vijana wanaoendesha bodaboda, ambao huwashawishi kwa kuwapatia msaada wa usafiri na kujikuta  baada ya muda wanawaingizia masuala ya mapenzi huku wakitoa vitu vidogovidogo kama kishawishi cha kufanya tendo la ndoa.

“Kwa kweli mtoto wa kike ukiwa na imani ndogo na kukosa uvumilivu, unajikuta umenasa kwenye mtego wa hawa bodaboda, maana wana tabia ya kutuvizia njiani tunapokwenda shule ama kutoka shule wanalazimisha kutupa lifti, sasa kwa vile shule ni mbali inabidi ukubali ili kuwahi masomo,” anaeleza.

Akifafanua kuhusu mkasa uliompata wa kukatazwa na baba yake kuendelea na masomo ya sekondari baada ya kufaulu mitihani ya darasa la saba, Neema anasema uamuzi huo ulimuumiza sana kiasi cha kushindwa kula kwa siku kadhaa.

“Nilipochaguliwa kujiunga na sekondari nilifurahi sana, nilimweleza baba yangu, lakini niliona hakuwa na furaha na taarifa niliyompatia, akanieleza haitokuwa rahisi kwangu kuendelea na masomo kwa vile hana uwezo wa kunisomesha sekondari na badala yake ni vizuri nikae nisubiri kuolewa,”

“Kauli hiyo ilikuwa mwiba mkali kwangu, hivyo niliamua kwenda kwa mama yangu (waliisha tengana na baba yake) nikamweleza maamuzi ya baba, mama alikataa akasema lazima nisome, akawaeleza ndugu zangu wakanitafutia mahitaji yote ili niweze kwenda shule, lakini baba aligoma nisisome,” anaeleza.

Anaendelea kueleza kuwa baada ya baba yake kusimamia uamuzi wake yeye aliamua kuwaandikia walimu wake barua kwa siri ili waweze kumsaidia aweze kuendelea na masomo na kwamba ndoto yake akihitimu masomo yake alitaka awe mwalimu pia.

TAZAMA BARUA YA NEEMA HII HAPA CHINI.


Anasema baada ya walimu wake kupokea baru ile waliifanyia kazi kwa kuwasiliana na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyida pamoja na Ofisaelimu kata ambao walichukua hatua za kumtafuta baba yake na kuagiza apelekwe shule mara moja vinginevyo angechukuliwa hatua za kisheria.

“Kwa kweli nilifurahi sana baada ya kuelezwa na baba mwenyewe kwamba amebadili msimamo wake na amekubali nikaanze masomo ya sekondari kwenye shule niliyopangiwa, Sekondari ya kata ya Itwangi, pamoja na kuchelewa kuanza masomo takrbani mwezi mmoja lakini nilianza masomo,” anaeleza Neema.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Itwangi, wilayani Shinyanga, Amos Kilanga amepongeza msimamo wa mwanafunzi huyo ambapo amesema pamoja na kuchelewa kujiunga na masomo kwa takriban mwezi mmoja lakini ni miongoni mwa wanafunzi wanaofaya vizuri katika masomo yao darasani.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464