Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema
hadi kufikia Aprili 2022, deni la Serikali lilikuwa Sh69.44 trilioni
ikilinganishwa na Sh60.72 trilioni kwa kipindi kama hicho mwaka 2021, sawa na
ongezeko la asilimia 14.4.
Kati ya kiasi hicho, deni la nje lilikuwa Sh47.07 trilioni na deni la ndani
lilikuwa Sh22.37 trilioni
Dk Nchemba amesema hayo leo Jumanne Juni 14, 2022 wakati akiwasilisha hali ya
uchumi wa Taifa na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Amesema ongezeko la deni la Serikali lilitokana na kupokelewa kwa mikopo mipya
kutoka vyanzo vyenye masharti nafuu na ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia
miradi ya maendeleo.
Aidha, ongezeko la deni lilitokana na kutolewa kwa hatifungani maalumu yenye
thamani ya Sh2.18 trilioni kwa ajili ya deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa
Watumishi wa Umma (PSSSF) lililotokana na michango ya watumishi wa kabla ya
mwaka 1999.
SOMA ZAIDI HAPA-chanzo Mwananchi