TAARIFA KWA UMMA JUU YA MATUKIO YA UHALIFU YANAYOENDELEA LOLIONDO

 

 Askari polisi wakiwa wamebeba mwili wa askari polisi Garlius Mwita  aliyeuawa kwa kupigwa mshale eneo la Loliondo wilaya ya Ngorongoro 


TAARIFA KWA UMMA JUU YA MATUKIO YA UHALIFU YANAYOENDELEA LOLIONDO , JUNI 13, 2022

Chama Cha Waandishi wa Habari wa Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (OJADACT) kinalaani matukio ya kihalifu yanayoendelea kwenye zoezi la uwekaji mipaka ya eneo la Loliondo, Mkoani Arusha.

Matukio ya vurugu yanayoripotiwa kupitia kauli za viongozi ikiwemo ile ya Waziri Mkuu aliyoitoa Bungeni, kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella na ile ya Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa pamoja na taarifa zinazozagaa kupitia mitandao ya kijamii, ni wazi kuwa kumekuwa na uhalifu wa kisheria unaovunja haki za binadamu kwa kiasi kikubwa.


Taarifa ya kifo cha Askari wa Jeshi la Polisi Garlus Mwita (36) na taarifa nyingine za matumizi ya nguvu yanayoathiri utulivu na zoezi la uwekeaji mipaka na utulivu wa wananchi wa Loliondo yanapaswa kukomeshwa mara moja.


OJADACT inatoa mapendekezo kama ifuatavyo.

1.Serikali

· Itekeleze zoezi la uwekaji alama za mipaka kwa utulivu na ushirikishi baina yake na viongozi wa kaya za Loliondo.

· Isikilize hoja zinazotolewa kupitia kamati shirikishi za utatuzi wa mgogoro wa Loliondo.

· Ihakikishe ina wajibu wa kulinda amani na utulivu wa eneo la Loliondo.


2.Wakazi wa Loliondo

· Waepuke matumiz ya nguvu na silaha za jadi dhidi ya Maafisa wanaoshiriki zoezi la uwekaji alama za mipaka.

· Watumie njia shirikishi kuwasilisha hoja muhimu walizonazo juu ya utekelezwaji wa zoezi za uwekaji alama za mipaka Loliondo.



3.Jamii

· Iepuke kusambaza taarifa zinazoweza kukuza mgogoro wa Loliondo na kuleta taharuki.


4. Vyombo vya habari

· Vitumie weledi wa kitaaluma kwenye kuandika habari za mgogoro huu ili kuaksi uhalisia unaendelea.

· Viwe makini kwenye kuchangua vyanzo vya taarifa vya mgogoro huu pamoja na matumizi ya picha halisi za mgogoro .

· Vitumie uandishi wa kuleta suluhu (Solution Journalism) kwenye kuandika habari za mgogoro huu.

· Vitoe haki sawa kwenye kuweka mizania ya habari zinazohusu Loliondo

· Vijue vina haki ya kuandika habari za Loiondo kwa kujisimamia bila kuingiliwa kimaudhui.



5. Jeshi la Polisi

· Lihakikishe linachukua hatua za kuwatafuta na kuwakamata wale wote waliohusika kwenye matukio ya mauaji.

· Lihakikishe linatoa ulinzi wa raia na mali zake kama sheria ya uanzishaji wa Jeshi la Polisi inavyoelekeza.

· Lihakikishe linatoa taarifa za mara kwa mara za watuhumiwa linaowashikilia.


Edwin Soko

Mwenyekiti

OJADACT

13.06.2022

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464